Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Dkt, Charles Kimei.
Na Nathaniel Limu, Iramba
BENKI ya CRDB imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja katika bajeti yake mwaka huu kwa ajili ya kuchangia katika shughuli mbalimbali za uboreshaji wa huduma za kijamii nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Dkt, Charles Kimei amesema hayo kwenye hafla ya kukabidhi visima kwa shule tatu za msingi na sekondari mkoani Singida vilivyofadhiliwa na benki hiyo.
Dkt. Kimei amesema fedha zilizotumika kwa shughuli hiyo ni sehemu ya zaidi ya shilingi bilioni moja ikiwa ni asilimia moja ya faida inayotengwa na benki hiyo kila mwaka kusaidia huduma za jamii.
Amesema mwaka jana, benki ya CRDB ilipata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 100 hivyo kulazimika kutenga kiasi hicho cha fedha kama ilivyo sera yake ya kurejesha sehemu ya faida kwa wateja.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Kimei ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za kijamii husani maji safi na salama ambayo bado ni changamoto kubwa Vijijini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Yahaya Nawanda, ameishukuru benki hiyo kwa kufadhili uchimbaji na ujenzi wa visima hivyo husani kwa shule ya msingi Kizege yenye walemavu wa ngozi ambao walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma hiyo.
Hata hivyo watoto hao albino licha ya kushukuru kwa msaada huo wameomba kuunganishiwa maji hadi kwenye mabweni yao badala ya kulazimika kufuata nje suala ambalo ni hatari kwa maisha yao.
Pamoja na kufadhiliwa na CRDB na wadau wengine shughuli za uchimbaji na ujenzi wa visima katika shule tatu za msingi na sekondari mkoani Singida zimefanywa na Shirika la Nkwamira.