Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Bw Ramadhan Masele akifunga ziara ya kimafunzo ya siku tatu kwa kutoa shukrani kwa maafisa toka mashirika matano ya mikoa ya kanda ya ziwa (hawapo pichani) pamoja na maafisa toka Mfuko wa Msaada wa kisheria (LSF) na Foundation for Civil Society kwa ziara hiyo ya mafunzo.
Mwanakijiji wa kata ya Mwamala Wilaya ya Kwimba Bi. Grace Masanja akieleza msaada wanaopata juu ya elimu na ushauri wa kisheria toka kwa msaidizi wa kisheria katika kata yao, Bi. Grace alitanaibisha kwamba bado kuna tatizo kubwa la unyanyasaji wa kijansia unaofanywa na wanaume dhidi ya wanawake licha ya elimu ya haki za kila jinsi zinatolewa kila siku na kuwaomba wadau wa sheria. kuzidisha nguvu kuweza kukomesha tabia za wanaume kupiga wanawake.
Mwanakijiji wa kata ya Mwamala Bw. James Ngosha akiwashukuru wageni toka KIVULINI pamoja na washirika wengine kwa msaada wa kuwapatia muelimishaji wa haki na sheria katika kata yao kwani amekuwa akiwasaidia sana katika kutatua migogoro ya ardhi kijijini kwao.
Baada ya kumaliza ziara ya kutembelea kata za Ngudu, Mwamala na Hungumalwa katika wilaya ya Kwimba maafisa toka Asasi tano za kanda ya ziwa pomoja na wawezeshaji wa KIVULINI, LSF na Foundation for Civil Society wakifanya tathmini ya ziara yao nzima ya siku tatu katika kijiji cha Mwamala.
*************************************************************
Maafisa Miradi pamoja na Maafisa Wakaguzi na Tathmini Miradi toka mashirika matano ya Kiraia yanayopata ruzuku kutoka Mfuko wa Msaada wa Kisheria (LSF) Tanzania, yamemaliza ziara ya kimafunzo ya siku tatu katika Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na wasichana Tanzania, KIVULINI la jijini Mwanza, ziara iliyolenga kujifunza na kuboresha ufanyaji kazi wa mashirika hayo kupitia Miradi mbalimbali inayoendeshwa na KIVULINI.
Mashirika hayo matano toka mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mara, na Tabora yalianza mafunzo hayo Jumatatu ya tarehe 28 Aprili, 2014 na kumaliza mafunzo hayo tarehe 30 Aprili, 2014 kwa kutembelea Wasaidizi wa Kisheria wanaofanya kazi ya kutoa elimu na ushauri wa kisheria katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba chini ya shirika la KIVULINI kupitia mradi wa Msaada wa Kisheria unaofadhiliwa na LSF.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa Ziara hiyo Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Bw. Ramadhan Masele aliwashukuru maafisa wote toka mikoa hiyo mitano ya kanda ya ziwa kwa kuhudhuria mafunzo hayo lakini pia aliwashukuru Mfuko wa Msaada wa Kisheria kwa heshima waliyowapa KIVULINI kuwa kituo cha mafunzo kwa asasi nyengine.
“Ziara hii imetoa hamasa nzuri hasa kwa upande wa kimahusiano baina ya Asasi zinazotekeleza mradi wa msaada wa kisheria kwa kanda ya ziwa, pia uzoefu tuliobadilishana kwa siku zote tatu za mafunzo naamini utaenda kuimarisha utendaji kazi wa asasi zetu na kuinua hali ya maisha ya Watanzania kupitia sisi” alisema Mkurugenzi wa KIVULINI Bw Ramadhan Masele.
“Lakini pia tuwashukuru wadau wetu wakubwa katika mradii huu wa msaada wa kisheria, LSF, kwa ubunifu waliouleta wa kutuwezesha kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi, na hivyo hivyo shukrani zetu ziende kwa Foundation for Civil Society kwa kushirkiana na SLF kuwa pamoja nasi, tunaomba huu uwe ni mwanzo tu na usiwe mwisho” alimalizia Bw Masele
Ziara hiyo imeratibiwa na LSF kwa kushirikiana na Foundation For Civil Society kutoa hamasa na kuinua utendaji kazi wa Asasi za Kiraia nchini katika kuhakikisha asasi hizo zinatoa matokeo bora katika mradi wa Msaada wa kisheria.
Mashirika yaliyohudhuria ziara hiyo ya Kimafunzo ni Jamii Salama Development Volunteers (JSDV) toka Tabora, Centre for Widows and Children Assistance (CWCA) la mkoani Mara, Mama’s Hope Organization for Legal Aid (MHOLA), Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESHI), Sheria na Haki za Binadamu (SHEHABITA) la mkoani Mara.