Na Mwandishi Maalum
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesisitiza kuwa, Mpango wa Utekelezaji kuhusu Idadi ya watu na Maendeleo (ICPD) unapashwa kuzingatia pamoja na mambo mengine umalizaji wa ajenda ambazo hazijakamilika au kwa maneno mengine viporo vilivyobaki.
Tanzania imevitaja viporo hiyo kuwa ni upunguzaji wa umaskini, tofauti za usawa wa jinsia, elimu kwa watoto wa kike, uimarishaji wa huduma za afya, utokomezaji wa magonjwa mbalimbali yakiwamo malaria, kifua kikuu na maambukizi ya virusi ya Ukimwi.
Msisitizo huo wa Tanzania umetolewa na Bw. Charles Pallangyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katika siku ya tatu ya Mkutano wa 47 wa Tume ya Idadi ya Watu na Maendeleo, (ICPD) unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu Pallangyo anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo ambapo washiriki wanaoziwakilisha Serikali zao , wanafanya tathmini ya hali ya utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo uliofanyika miaka 20 iliyopita huko Cairo, Misri.
“ Tanzania imejitahidi sana na imefanikiwa katika utekelezaji wa Mpango wa Cairo, yapo maeneo ambayo tunajivunia ,nayo ni, upunguzaji wa idadi ya vifo vya watoto wachanga, kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika ngazi za utoaji wa maamuzi kama vile Bunge na taasisi nyingine, fursa sawa za elimu kwa uwiano wa jinsia, uwezeshwaji wa wanawake na haki za binadamu kwa uchache” akasema katibu Mkuu na kuongeza.
Pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, bado kuna maeneo ambayo mafanikio yake si ya kuridhisha sana. Baadhi ya maeneo hayo ni upunguzaji wa vifo vya wanawake wajawazito na utokomezaji wa magonjwa kama vile maambukizi ya virusi vinavyosababisha ukimwi.
“ Ni kwa sababu hiyo basi, sisi ( Tanzania) tunataka kutilia mkazo kwamba, kima ilivyokuwa miaka 20 iliyopita, ICPD ni muhimu sana hasa katika maandalizi ya ajenda za maendeleo endelevu baada ya 2015. ni lazima pia kutilia mkazo utekelezaji wa viporo ambayo havikumalizwa wakati wa utekelezaji Malengo ya Maendeleo ya Millennia ambayo yanafikia ukingoni” akasisitiza Katibu Mkuu Pallangyo.
Akaogeza kwamba, Mpango wa Utekelezaji wa ICPD ni vema pia ukashughulikia changamoto mpya zinazoibuka hivi sasa zikiwamo za uongezeko la idadi ya wazee ,ongezeko ambalo linapita idadi ya watoto wadogo chini ya miaka mitano.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kati ya nchi 47 zilizochaguliwa na Baraza Kuu la Uchumi na Ustawi wa Jamii ( ECOSOC) kuwa mjumbe wa Tume ya Idadi ya Watu na Maendeleo. Wajumbe hudumu wa katika Tume hiyo kwa kupindi cha miaka mine na huchaguliwa kwa mgawanyo wa kijiografia.
Pamoja na wajumbe wanaotoka serikali mbalimbali, mkutano huu unahudhuriwa pia na idadi kubwa ya wajumbe kutoka Asasi zisizokuwa za kiserikali.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa mkutano huu zinazonyesha kwamba kwa ujumla kumekuwapo na mafanikio makubwa katika kipindi hicho cha miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano huo wa Cairo mwaka 1994.
Baadhi ya mafanikio hiyo ni kuongezea kwa umri wa watu kuishi ambapo sasa dunia inasadikiwa kuwa na wazee wengi, kuongezea kwa wakazi wa mijini, kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, wanawake kujipatia fursa ya kimiliki ardhi katika baadhi ya nchi,
Katika Mkutano huo wa Kimataifa wa Cairo ambao unatajwa kuwa ni mkutano wa kihistoria, uliohudhuriwa na nchi 179 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo mkazo ulikuwa kwamba binadamu ndiye mlengwa mkuu katika jitihada za kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii
Ni katika Mkutano huo ambapo suala la upatikaji wa huduma za elimu , afya na haki za binadamu hasa wanawake na vijana kulielezwa kama kungesaidia uchagizaji wa maisha bora kiuchumi na kijamii na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo endelevu na mwenendo endelevu wa idadi ya watu
Aidha wakati wa mkutano huo wajumbe walijiwekea malengo ya utekelezaji katika maeneo ya upunguzaji wa umaskini, utokomezaji wa tofauti za kijinsia, maendeleo ya miji na uhamiaji, maendeleo ya jamii, na haki za wanawake na vijana katika maeneo mbalimbali kama vile haki za afya pamoja na afya ya uzazi.
Chanzo: michuzi matukio blog