Picha
juu na chini ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa
Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Bw. Mohamed Tibanyendera (wa pili
kushoto) akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusiana maadhimisho ya
siku ya uhuru wa vyombo vya habari yatakayofanyika wiki hii duniani
kote. Kushoto ni Meneja wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Allan Lawa, Afisa Habari wa kituo cha Habari cha Umoja
wa Mataifa (UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama (wa pili kulia) na Makamu
Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC),
Jane Mihanja (kulia).(Picha na Zainul Mzige).
=====
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Zaidi
ya washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria
kwenye matukio ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani,
inayotarajiawa kuadhimishwa nchini hapa mnamo Mei 3, jijini Arusha,
imeelezwa.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari
Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Bw. Mohamed
Tibanyendera, amesema kwamba maadhimisho hayo yenye lengo kuu la kulaani
maovu wanayofanyiwa waandishi wa habari barani Afrika na duniani kote,
yatafunguliwa na Jaji Mstaafu Mark Bomani.
Tibanyendera
amesema kwamba, pamoja na mambo mengine maalum ambayo yatakuwa
yameandaliwa, matukio ya mwaka huu yataambatana pia na uzinduzi wa
kitabu kiitwacho “Hii Ndiyo Demokrasia, Toleo la 20”, kitachokuwa na
taarifa muhimu kuhusu waandishi wa habari walionyanyaswa na kufanyiwa
vitendo vilivyokiuka haki za binadamu, barani Afrika.
Meneja
wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Allan Lawa
(kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar kuhusu
siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari itakayofanyika jijini
Arusha.
“Tunategemea
kuwa na wageni zaidi ya 200, kwa siku hiyo pia tuazindua kitabu
kitachozungumzia waandishi walionyanyaswa na kufungwa katika maeneo
mbalimbali ya Kusini mwa Afrika pamoja na hali ya vyombo vya habari na
uhuru wa habari katika nchi hizo ikiwemo Tanzania,” amesema
Tibanyendera.
Tibanyendera
ameongeza na kusema kwamba maadhimisho hayo ya siku mbili,
yatakayofanyika kuanzia Mei 2 hadi 3, yataambatana pia na utolewaji wa
semina za kuwaelimisha washiriki kuhusu mambo mbalimbali ya habari na
uhuru wake, kutoka kwa wataalam wakiwemo wahadhiri watakaotoka vyuo
mbali mbali hapa nchini na kwingineko, ambao wameandaliwa rasmi kwa
ajili ya shughuli hiyo.
Wakati
huo huo, Meneja wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT) ambao pia ni moja ya taasisi zitakazoshiriki kwenye maadhimisho
hayo, Bw. Allan Lawa, amesema kwamba MCT itazindua katika maadhimisho
hayo machapisho matatu yatakayohusu masuala ya habari ikiwepo ripoti ya
uvunjifu wa uhuru wa habari nchini ambayo yatapatikana katika ofisi zao.
Mwakilishi
wa Umoja wa Mataifa ambao ni mmoja wa wadhamini wa siku ya uhuru wa
vyombo vya habari duniani, Bi. Usia Nkhoma Ledama (wa pili kulia),
ambaye alisisitiza kwamba uhuru wa vyombo vya habari nchini ni muhimu
kusaidia nchi zinazoendela kufika malengo ya milenia.
“Sisi
kama MCT tumeandaa machapisho matatu ambayo yatazinduliwa siku hiyo
yanayogusia hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania 2013,
ripoti ya utafiti wa uvunjifu wa uhuru wa habari katika mwaka 2013, na
ripoti ya ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
“Tuna
furaha kuwaambia kwamba machapisho yote haya yatapatikana siku hiyo na
wote mnakaribishwa kujipatia nakala zenu,” amesema Lawa.
Akimalizia,
Bw. Lawa alisema waandishi wa habari wanapaswa kufika katika ofisi za
Makao Makuu ya MCT zilizopo jijini Dar es Salaam kuchukua machapisho
hayo ili waweze kuyasoma kwa kina na kuweza kutambua haki zao za msingi.
Alisema pia kwamba muda si mrefu, nakala za machapisho hayo
zitasambazwa na kupatikana kwenye vilabu vya vyombo vya habari (Press
Club) vya mikoani ili waandishi ambao wako nje ya Dar es Salaam nao
waweze kunufaika na machapisho hayo.
Maadhimisho hayo yamembeba kauli mbiu ya “Uhuru wa vyombo kwa Maendeleo ya Utawala Bora”.
Makamu
Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC),
Jane Mihanja ambaye amesema mwandishi wa habari yoyote akizuiwa kuingia
kwenye mkutano ambao ni wawazi anatakiwa kutoa taarifa katika juhudi za
kuhamasisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Pichani juu ni chini ni baadhi ya waandishi wa habari na wadau wa tasnia hiyo waliohudhuriwa mkutano huo.