SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, April 15, 2014

TBS YAJIWEKEA MIKAKATI YA KUDHIBITI UBORA WA BIDHAA ZA NDANI NA NJE YA NCHI

 Mkurugenzi Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Tumaini Mtitu akiwaeleza waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam mikakati ya kudhibiti ubora wa bidhaa za ndani na zinazotoka nje ili kuepuka madhara kwa watumiaji  wa bidhaa hizo. Kushoto ni Afisa Uhusiano wa shirika hilo Bi Roida Andusamile.
Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mkutano wa Shirika la Viwango Tanzania uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. PICHA ZOTE NA FATMA SALUM 
 
****
Na Frank Mvungi-Maelezo
Serikali imedhamiria kuwainua wajasiriamali wadogo hapa nchini ili kuongeza uzalishaji wa Bidhaa za ndani zitakazosaidia kuimarisha uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shirika la viwango hapa nchini (TBS)  Tumaini Mtitu wakati wa Mkutano na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam.
Alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) kuwajengea uwezo wajasirimali wadogo ili hatimaye wazalishe bidhaa zenye ubora na hivyo kupata cheti cha ubora kinachotolewa na shirika hilo.
Mtitu aliongeza kuwa wajasiriamali wote wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa hapa nchini wanatakiwa kuthibitishwa na shirika hilo ili kuwalinda watumiaji wa bidhaa hizo kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa kwa mujibu wa  sheria.
Aliwataka Wajasiriamali hao kupitia SIDO ili waweze kujengewa uwezo wa kuzalisha bidhaa bora na baada ya hapo bidhaa zao ziweze kukaguliwa na kama zikikidhi vigezo wapate cheti cha ubora ambapo mchakato huo unaweza kuchukua mwezi mmoja.
Akizungumzia faida za Wajasiriamali kupata cheti cha ubora baada ya bidhaa zao kukidhi vigezo vilivyowekwa na shirikika hilo, Mtitu alisema unawawezesha wajasiriamali kupanua wigo wa soko la bidhaa zao na kuwa  wa kimataifa.
Wakati huo huo Mtitu aliwataka watanzania wote kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia shirika hilo ili waweze kupata cheti cha ubora  na kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.
Utaratibu wa kupata alama ya ubora ni kwanza kuwasilisha maombi kwa mkurugenzi Mkuu wa TBS, ukaguzi wa awali na upimaji wa Sampuli za bidhaa husika na hatimaye kutolewa kwa cheti cha ubora baada ya bidhaa husika kukizi vigezo.