Vijana wa Scout wakimvisha skafu
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete muda mfupi baada ya kuwasili katika
uwanja wa ndege wa Mafia jana asubuhi ambapo alifungua uwanja wa ndege wa
Mafia na kuzindua Gati la Mafia.Rais Kikwete yupo katika ziara ya
kikazi ya mkoa wa Pwani.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete
akifunua kitambaa kuashiria kuzindua rasmi uwanja wa Ndege Mafia
uliojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na mfuko wa
Millenium Challenge Corporation (MCC), Kulia ni Mratibu wa shughuli za
MCC nchini Bwana Bernard Mchomvu na katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi
Mwantumu Mahiza na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete
akisalimiana na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mafia muda mfupi kabla
ya kuzindua rasmi Gati la Mafia jana asubuhi.Picha na Freddy Maro-IKULU
---
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Ni kero za miaka mingi
za wananchi wa Mafia
·
Awaambia kuwa Serikali
sasa imetimiza ahadi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Alhamisi, Oktoba 3, 2013 amezindua miradi
miwili mikubwa ya maendeleo Kisiwani Mafia ambayo inamaliza kero za miaka mingi
za wakazi wa Kisiwa hicho.
Rais Kikwete amezindua
Uwanja wa Kisasa wa Ndege wa Mafia na pia amefungua Gati ya Mafia, miradi
mikubwa ya miundombinu iliyoko mjini Kilindoni na ambayo inamaliza malalamiko
ya miaka mingi ya usafiri ya wakazi wa Mafia.
Ndege iliyombeba Rais Kikwete
imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mafia kiasi cha saa 5:35 asubuhi na kuanza
mara moja shughuli ya kuzindua Uwanja huo ambao umejengwa kwa gharama za dola
za Marekani milioni 13.57.
Uwanja wa Ndege wa Mafia
ni moja ya miradi mingi na mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa nchini
chini ya misaada ya Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC)
na ambayo katika Tanzania utekelezaji wake uko chini ya Akaunti ya Changamoto
za Milenia Tanzania ya Millennium
Challenge Corporation Tanzania (MCA(T).
Hiyo ndiyo imekuwa
shughuli ya kwanza kufanywa na Rais Kikwete ambaye ameanza ziara ya siku tano
ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Pwani kwa kutembelea
Kisiwa cha Mafia.
“Bado tunayo kazi ya
kufanya kuhusu uwanja huu wa Mafia ikiwa ni pamoja na kuuwekea taa, ili uweze
kutumika hata usiku, na pia kujenga jengo jipya la kisasa la abiria ili
kuongeza uwezo wa usafiri wa Kisiwa cha Mafia kuliko ilivyo sasa,”
amesema Rais Kikwete na
kusisitiza:
“Najua kuwa wakazi wa
Mafia, kwa miaka mingi mmekuwa na vilio viwili vikubwa vinavyohusiana na
miundombinu, usafiri na mawasiliano ya usafiri – yaani uwanja wa ndege na gati.
Yote mawili sasa tumeyafanikisha na kuyatekeleza kama tulivyoahidi kwenye Ilani
ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2013. Ndugu zangu wa Mafia kimebakia nini sasa?” amesema Rais Kikwete na kuelezea jitihada za
Serikali za kujenga viwanja vya ndege nchini.
Kwenye Bandari ya
Kilindoni, Rais Kikwete amezindua Gati ya Mafia ambayo ina urefu wa kilomita
1.3, uwezo wa kubeba magari yenye tani zisizozidi 10 na yanayokwenda kwa kasi
ya maili 15 kwa saa, mradi ambao umegharimu kiasi cha Sh. bilioni 20.
Baada ya kuzindua rasmi
Gati hiyo, Rais ametembea urefu nzima wa daraja hilo ambako aliwapokea abiria
wa kwanza kutumia Gati hiyo na kuwasalimia wafanyakazi wa Meli ya F.B. Khadija
ambayo itakuwa inatoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati, Mkoa wa Pwani pia.
Akizungumza na mamia ya
wananchi waliohudhuria shughuli za ujenzi huo, Rais Kikwete amefurahi kuwa
Serikali yake imeweza kumaliza kero mbili kubwa na za muda mrefu ambazo
zimekuwa zikiwakabili wananchi wa Mafia.
Rais Kikwete ameitaka
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambayo imejenga na inamiliki Gati hiyo kuweka
usafiri wa kuwavusha wasafiri kutoka Gatini hadi meli zinapoegeshwa na kutoa
changamoto kwa Mamlaka hiyo sasa kujenga Bandari kamili hapo hapo Mafia.
Rais Kikwete amerejea
Dar es Salaam jioni ya leo na kesho ataendelea na ziara ya Mkoa huo wa Pwani
kwa kutembelea Wilaya ya Mkuranga.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
3 Oktoba, 2013
CHANZO: HAKI NGOWI
CHANZO: HAKI NGOWI
0 comments:
Post a Comment