Ndugu zangu,
Katika ulimwengu huu kuna tabia na hulka. Hivi viwili vina tofauti. Kuna sifa na uwezo, navyo ni viwili tofauti.
Tabia ya mwanadamu yaweza kubadilika,
lakini si hulka yake. Na mwanadamu anaweza kuwa na sifa za kufanya jambo
lakini akakosa uwezo, na kinyume chake. Na kibaya zaidi ni pale majungu
na fitna yanapogubika sifa na uwezo wa mtu. Kwamba badala ya mwanadamu
kupimwa kwa sifa na uwezo wake, majungu na fitina dhidi ya mwanadamu
huyo yanawekwa mbele na hivyo kufanywa kuwa kipimo.
Ndio, kuna wanadamu wenye kuishi kwa
kupika majungu na fitna dhidi ya wanadamu wenzao. Tofauti na tabia, hizo
ni hulka za wanadamu hao, haziwezi kubadilika.
Ndio, nyani hata akizeeka haachi hulka
yake. Kupalamia miti ni hulka ya nyani. Hivyo, nyani hata akizeeka,
hafikiri hata siku moja kukaa chini ya mti na kupumzika, atahakikisha
anapalamia hata mti mfupi wa mpapai, alimradi akae juu ya mpapai. Hapo
atajiona ametimiza unyani wake.
Naam, Wahenga walitwambia; kiumbe
mzito. Mwenyezi Mungu ametuumba wanadamu kwa usawa kwenye mambo mengi.
Wala hakutaka kubagua; ona unyayo wa mwanadamu, uko sawa, iwe kwa tajiri
au masikini.
Wewe na mimi tumepata, ama wenyewe au
kusikia mtu akilalamika kuwa soli ya kiatu chake imechakaa, kwamba
anakwenda kwa fundi viatu kubadilisha soli. Lakini, wewe au mimi
hatujapata kumsikia mwanadamu mwenzetu akilalamika kuwa unyayo wake
umechakaa, anataka kwenda kwa fundi awekewe unyayo mwingine!
Ndio, wewe na mimi ama tumeshuhudia au
kusikia kuwa upepo umeangusha mti, nyumba, ghorofa, gari na hata meli.
Lakini, jiulize, je, umepata kumwona mwanadamu mwenzako anayetembea kwa
miguu akiangushwa kwa upepo?
Kamwe mwanadamu haangushwi na upepo,
hata awe mwembamba kiasi gani. Na ukimwona mwanadamu mwenzako anayumba
na kuanguka barabarani, basi, ama ni mgonjwa, au ni mlevi. Na hilo la
mwisho haliwezi kuwa na maana ya mwanadamu huyo kaangushwa na upepo,
bali kaangushwa na pombe zake alizokunywa.
Naam, kiumbe mzito.
Ni Neno La Leo.
Maggid.
Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment