CHENGE AJIPALIA MAKAA
Mbunge mteule wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
TUHUMA zilizotolewa na mbunge mteule wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, dhidi ya uongozi wa Bunge la Tisa uliokuwa chini ya Spika Samuel Sitta, zimewachefua wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida ambao kwa nyakati tofauti wamesema mwanasheria huyo wa zamani wa serikali hakustahili kutoa shutuma hizo kwa madai kuwa si msafi.
Juzi, Chenge aliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza sababu zilizomsukuma kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Muungano na "makandokando" yanayozunguka jina lake na akatumia nafasi hiyo kumshambulia Sitta kuwa aliongoza Bunge kinafiki, kizandiki na kwa lengo la kupakana matope na kutaka mbunge huyo wa Urambo Mashariki aogopewe kama ugonjwa wa Ukimwi.
Chenge, ambaye amekuwa akihusishwa kwenye tuhuma kadhaa za ufisadi, ikiwa ni pamoja na sakata la ununuzi wa rada, alisema akipewa kiti cha ubunge atahakikisha anarejesha dhana ya wengi wape kwa kuwapa nafasi zaidi wabunge wa chama tawala chenye wabunge wengi, lakini bila ya kuathiri haki za wachache kutoa maoni yao.
Lakini, badala ya ufafanuzi wake kusafisha picha yake mbele ya jamii, kitendo hicho kimewachafua watu wengi waliosoma taarifa za vyombo vya habari vikimkariri Chenge ambaye alilazimika kujiuzulu uwaziri wa Miundombinu baada ya kutajwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada.
Katika kashfa hiyo, kitengo cha uchunguzi wa makosa makubwa cha Uingereza, SFO kilibaini akaunti moja ya Chenge iliyo nje ya nchi ikiwa na takriban Sh1.2 bilioni wakati kikichunguza mzunguko wa fedha ambazo serikali ya Tanzania ilitoa kununua rada. Uchunguzi huo ulikamilika Februari mwaka huu kwa kampuni ya BAE System kukiri makosa ya kutotunza rekodi zake na kukubali kulipa fidia.
Chenge pia anatuhumiwa kuuingiza nchi kwenye mikataba mibovu na makamapuni ya madini wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ununuzi wa ndege ya kifahari ya rais, mambo ambayo yamewafanya wananchi wengi walioongea na gazeti hili kumshambulia mbunge huyo mteule wa Bariadi Magharibi.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana na wengine kuandika maoni yao kwenye tovuti, watu wengi walionyeshwa kuchukizwa na kauli hizo za Chenge wakisema kuwa bado ana madoa mengi ya tuhuma za ufisadi ambayo anapaswa kujisafisha kabla ya kushambulia wengine.
Mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari aliizungumzia mashambulizi ya Chenge dhidi ya Sitta kuwa ni ukosefu wa ustaarabu.
"Madai ya Chenge kwamba atatoa fursa zaidi kwa wabunge wa CCM kwa sababu ni chama tawala, yanaashiria kuwa atakuwa na upendeleo na hilo linamwondolea sifa kuu ambayo spika anatakiwa kuwa nayo," alisema Prof Safari alipozungumza na Mwananchi kuhusu tamko la Chenge.
Harod Tairo, mhadhiri wa sheria kwenye Chuo Kikuu cha Tumaini, alienda mbali zaidi na kuielezea mashambulizi ya Chenge kuwa yanatoa taswira kwamba waziri huyo wa zamani wa miundombinu anataka kiti hicho ili akalipize kisasi bungeni.
Tairo alisema uongozi wa Sitta, ambaye uongozi wake ulilifanya Bunge lake kuingia kwenye historia kama chombo kilichotekeleza wajibu wake wa kuiwajibisha serikali, ulifanya kazi kama ilivyostahili.
“Pamoja na dhamira yake, anatumiwa na wanaodhani hawakutendewa haki kwenye bunge lililopita; anatumiwa kulinda maslahi ya wabunge mafisadi… angekuwa na nia ya kuutumikia umma, angeeleza hoja zinazokubalika tofauti na alivyofanya,” alieleza Tairo.
Mbunge mteule wa Jimbo la Kilindi mkoani Tanga, Beatrice Shelukindo alisema haungi mkono uamuzi wa Chenge kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uspika kwa kuwa anakabiliwa na kesi mahakamani. Hadi sasa Chenge anakabiliwa na kesi ya kuendesha gari kizembe na kusababisha vifo vya watu wawili jijini Dar es salaam na pia kuendesha gari akiwa na bima iliyoisha muda.
Shelukindo, mmoja wa wabunge waliojipambanua katika Bunge la Tisa kama mpambanaji wa ufisadi, alisema pamoja na kuwa ni haki ya kila mbunge kuwania nafasi hiyo, kuna mambo ya msingi ambayo hayana budi kuangaliwa kabla ya kufikia maamuzi kama huo ili Tanzania isionekane kutofuata sheria katika kutekeleza mambo yake.
Kwa mujibu wa Shelukindo, Watanzania wa leo ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuelewa mambo na hawatawaelewa wabunge iwapo watampitisha Chenge kuwa spika wakati anazungukwa na tuhuma za ufisadi.
“Watanzania wa leo sio wale wa juzi. Wanao uelewa mkubwa na wanajua misingi ya sheria na wajibu wa vyombo kama Bunge. Sasa sisi tukijifanya kumchagua eti kwa sababu ni wa wabunge, wananchi watavunjika moyo na hawatatuelewa,” alisisitiza Shelukindo.
Kuhusu madai ya Chenge kuwa kulikuwa na ombwe la uongozi kwenye Bunge lililopita, Shelukindo alisema mwanasheria huyo mkuu wa zamani hakustahili kuzungumza maneno mengi kiasi kile kwa kuwa hakuna asiyefahamu kwamba Bunge lililopita lilikuwa la vyama vingi hivyo lilipaswa kuendeshwa kwa kanuni za kibunge na siyo kupendelea vyama.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo alieleza kukasirishwa na malumbano aliyoyaibua Chenge hata kabla ya kuingia bungeni, akisema hiyo inatoa taswira mbaya kuwa huenda akawa ni mtu wa kulipiza visasi.
“Yoyote atakayechaguliwa au hata kama wote hawatachaguliwa, mimi nafikiri si sahihi kuanza kumsakama Spika aliyepita kwa sababu ukianza hivyo Bunge linaweza kuwa forum (jukwaa) la kulipiziana visasi,” alisema Kisumo.
Msomi wa shahada ya uzamivu (Phd) kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Gasper Mpehongwa alilisifia Bunge lililopita kwamba lilikuwa bora na lenye uhuru wa kutosha kwa maslahi ya taifa.
“Ninaposema lilikuwa safi namaanisha hata Spika alikuwa safi. Ningepewa nafasi ningemchagua tena (Sitta),” alisema Mpehongwa.
Mwanafunzi mwingine wa Phd chuoni hapo, akizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, alisema Chenge ana nguvu ya fedha inayoweza kumpatia kiti hicho na kwamba hilo likitokea, wengi wataumia.
Mkazi mmoja wa Moshi aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Mfinanga alisema: “CCM na serikali yake wasifikiri Watanzania ni mbumbumbu… tunafahamu uadilifu. Sasa kabla ya kumpitisha Chenge watuambie sababu zilizomfanya ajiuzulu ni zipi na kama sasa ametakasika.”
Mfinanga anayejihusisha na biashara ya huduma ya internet, alisema Chenge alijiuzulu uwaziri wa miundombinu baada ya kuhusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada, hivyo hakupaswa kujitakasa mwenyewe bali vyombo vya dola.
Mfanyabiashara huyo alimsihi Rais Jakaya Kikwete na CCM kutoingia katika mtego wa kutompitisha mtu mwenye sifa na uadilifu na kuitaka Taasisi ya Makosa Makubwa Duniani(SFO) kutamka kama change ni mtuhumiwa wao au la.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Patrick Boisafi alisema Watanzania wanaufahamu utendaji wa Chenge na wa Sitta hivyo wanaiachia CCM kuwaweka katika mizani na kuwapatia mtu safi.
“Tunafahamu Chenge ana haki ya kikatiba kuwania nafasi hiyo, lakini shaka yetu inaegemea katika maneno yanayosemwa juu yake… cha kujiuliza ni je sasa amesafishika? na ni chombo gani kimemsafisha," alihoji Boisafi.
Wakili mmoja wa kujitegemea aliyeomba jina lake lihifadhiwe aliilaumu moja kwa moja Takukuru kwa kulifanya suala la Chenge kuwa siri licha ya kuhojiwa na kila Mtanzania.
“(Takukuru) Wanaweza wakajitetea kuwa Chenge anachunguzwa na SFO, lakini tuhuma nzito kama hiyo ya rada haiwezi kuachiwa taasisi za kimataifa kana kwamba sisi hatuna uwezo... tungeshirikiana nao,” alidai.
Hata hivyo, Takukuru ilitoa taarifa jana ikieleza kuwa uchunguzi wa SFO umebaini kuwa Chenge hakuhusika kwenye sakata hilo. Taarifa hiyo haikufafanua sababu za Takukuru kutoa ufafanuzi sasa wa jambo ambalo uchunguzi wake ulikamilika Februari mwaka huu.
Mwanasiasa mkongwe nchini na muasisi wa Chadema, Edwin Mtei alishangazwa na hatua ya Chenge kuchukua fomu ya kuwania kiti hicho huku na kuhoji uadilifu wa kada huyo akisema unatia shaka kutokana na kukakabiliwa na tuhuma za kashfa mbalimbali za ufisadi.
Mtei, ambaye pia aliwahi kuwa gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), alisema endapo chama chake (CCM) kitadiriki kumpatia wadhifa huo, nchi itakuwa njia panda.
‘Hata mimi ndio nilikuwa nashangaa na wenzangu hapa na tunajadili kuwa itawezekanaje mtu kama Chenge achukue fomu ya kuwania kiti cha uspika na CCM wanamuangali tu. Huyu mtu ana tuhuma nyingi za ufisadi... hii nchi tutaiweka pabaya sana,” alisema Mtei.
Naye Profesa Mwesigwa Baregu alisema amestushwa kusikia CCM imempa fomu Chenge kugombea kiti cha spika.
“Bunge letu lina hadhi, haliwezi kuongozwa na Chenge… kwanza amalize tuhuma zake kwenye mahakama mbalimbali na ile ya rada sijui aliifikisha wapi. Nadhani anatafuta kujisafisha ila amekosea. Njia pekee ni yeye kukaa kando,” alisema Prof Baregu ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino.
Profesa Baregu alisema Sitta alisimamia Bunge kwa kuzingatia kanuni na kwamba kama Chenge anamtuhumu kupendelea wabunge wa upinzani, aeleze wabunge waliokaripiwa bungeni kwa kutozingatia taratibu na kanuni za Bunge ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kuhudhuria vikao vya bunge, walikuwa wa kambi gani.
Alisema kumbukumbu zinaonyesha, John Cheyo (UDP) mwaka 2008 alikaripiwa na Sitta wakati wa kikao cha Bunge kutokana na kukiuka kanuni na taratibu. Pia Zitto Kabwe (Chadema) mwaka 2009 aliadhibiwa kwa kuzuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa miezi mitatu kwa kilichoelezwa kukiuka taratibu za bunge.
Kada mmoja wa CCM aliyezungumza na gazeti hili kwa ombi la kutotajwa jina alisema kauli ya Chenge ni miongoni mwa mikakati mingi inayolenga kuhakikisha Bunge lenye msisimko kama lililopita, halitokei tena.
“Leo ameibuka Chenge na hizo kauli zake; kesho mtasikia wanaodai spika awe mwanamke. Sioni sababu ya kampeni kufanywa kwenye vyombo vya habari wakati mchakato wake ni wa ndani ya vyama, kisha bungeni,” alieleza.
Kada huyo alisema wanaotumia vyombo vya habari wangekuwa na dhamira nzuri, wangeeleza sifa, majukumu na wasifu wao ili wananchi wawajue na kujenga imani nao.
Kutoka Mtandaoni, Wasomaji wa Mwananchi wamekuwa na maoni tofauti juu ya kauli hiyo, lakini wengi wamechukizwa na kitendo cha Chenge kutumia lugha kali wakimtaka akae kimya kwa kuwa hana sifa.
"Tunamshauri huyu mzee 'visenti' asilete utani mbele ya safari kwani ataanguka kwa aibu mbele ya jamii na amwogope Mungu, mikataba mibovu aliyopitisha kinyemela inatosha," alisema Estomihi Lyimo.
Msomaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mchungu wa Bongo alisema "kama umetumwa na hao watuhumiwa wa ufisadi na kama kuna mbunge atapokea pesa ili awasaliti Watanzania... basi mbunge huyo na afe na watu wote waseme amen".
Msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Deobern alisema: "Nilisikitika sana niliposikia kuwa Chenge ambaye sistahili hata kumwita mheshimiwa, amechukua fomu ya kugombea uspika. Sishangai kwa sababu, inawezekana nikawa namwonea Chenge ilhali ametolewa sadaka kumfunga paka kengele.
"Asante Chenge kwa kujitokeza kuwania uspika. Hivi kweli hujioni umechafuka? Ondoa jina lako haraka utaaibika.Wewe nadhani uroho wako wa madaraka unataka kuimaliza sisiem na pia kuichafua inji hii."
0 comments:
Post a Comment