Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
Ban Ki-Moon ametaka upelelezi huru ufanywe nchini Congo kuhusiana na
kifo cha mwanaharakati wa haki za binadamu.
Mwili wa marehemu Floribert Chebeya ulipatikana
ndani ya gari lake baada ya kuitwa na polisi kwa mkutano ambao baadaye
ulisemekana haukufanyika siku ya Jumanne.
Mchunguzi mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyaelezea
mazingira ya kifo hicho kama ya kukanganya na yanaonyesha kuhusika kwa
vyombo vya dola.
Hata hivyo serikali haijatoa kauli yake ingawa
imeitisha uchunguzi ufanywe.
Umoja wa Mataifa una askari wengi wa kulinda
amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaosaidia nchi hiyo
kujikwamua kutoka janga la muda mrefu la vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Marehemu Chebeya aliyefariki akiwa na umri wa
miaka 47 alikuwa kiongozi wa shirika la kutetea haki za binadamu Voice
of the Voiceless na wanaharakati wanasema alikuwa akipokea vitisho kwa
kipindi cha miaka ishirini iliyopita.
Mchunguzi mkuu wa upelelezi wa Umoja wa Mataifa
Philip Alston alielezea mashaka yake juu ya kifo hicho alipohutubia
baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva.
Siku ya Alhamisi asubuhi watu wawili kutoka
familia ya marehemu huyo, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na
wanaharakati wawili kutoka shirika la Voice of the Voiceless
waliruhusiwa ndani ya chumba cha maiti mjini Kinshasa kuuona mwili wa
marehemu.
Waliweza kuona sehemu ya uso kwa sababu sehemu
iliyobaki ya mwili ilikuwa imefunikwa shuka ambayo hawakuruhusiwa
kuiondoa.
Kabla ya hapo mke wa marehemu alisema kuwa
Bw.Chebeya alimpigia simu na kumfahamisha kuwa alikuwa kwenye makao
makuu ya polisi kwenye mkutano na mkuu wa polisi na tangu hapo
hakusikika tena.
Mwanamke amuuza mwanae Bolivia
Mwanamke mmoja mwenye umri wa
miaka 30 kutoka makabila ya wazawa ya Bolivia amekamatwa na polisi
katika mji wa Cochabamba kwa kumuuza mtoto wake mchanga kwa dola za
kimarekani 140.
Duru za polisi kwenye mji wa Cochabamba uliopo
katikati mwa nchi hiyo ya Amerika ya kusini zimesema mwanamke huyo
amekiri kumwuuza mtoto huyo kwa sababu hana uwezo wa kumtunza.Jesusa Molle ameiambia polisi kwamba mume wake alimuacha hivyo hana uwezo wa kumudu gharama za matunzo ya mtoto mchanga.
Baadaye Jesusa alikiri kumwuuza mtoto wake wa kike kwa kiasi cha fedha za Bolivia bolivanos elfu moja, sawa na dola za kimarekani 140.
Polisi hao pia wamemnasa mwanamke aliyenunua mtoto huyo, mwenye umri wa miaka 35 aliyesema kuwa aliamua kumnunua mtoto huyo kwa kuwa hakujaliwa kuzaa watoto wake mwenyewe.
0 comments:
Post a Comment