Na Job Ndomba
MAANDAMANO ya wanaharakati
yaliyotakiwa kufanyika jana na kuishia katika Viwanja vya Mlimani city
kunakofanyika mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia kwa Afrika (WEF)
yamefanyika kwa namna yake ambapo yalianzia ndani ya Ofisi za Mtandao
wa Jinsia Tanzania (TNGP) na kuishia nje ya viwanja vya ofisi hizo,
huku Profesa Issa Shivji akimwaga 'cheche' akidai kuwa mkutano wa WEF
ni wa kuendeleza ubeberu wa kibepari.
Hayo yalitokea jana wakati wa jukwaa la wananchi wa Afrika
liliandaliwa na wanaharakati hao ili lifanyike sambamba na Jukwaa la
Uchumi la Dunia kwa Afrika linaloendelea Jijini Dar es Salaam kuanzia
jana.
Akizungumza katika Jukwaa hilo, Prof. Shivji alisema kuwa
mkutano huo wa WEF hauna faida ya kimaendeleo kwa Afrika zaidi ya
kuendeleza mfumo wa kibepari unaoendelea kunyonya nguvu na raslimali za waafrika.
"Kwa
ujumla mkutano huo hauna faida kabisa kwetu zaidi ya kuendeleza
mikakati ya kibeberu na kibepari ya kuwanyonya Waafrika," alisema Prof.
Shivji.
Prof. Shivji alisema mkutano huo ni wa wababe
wanaojiita CEOs wa makampuni ya kimataifa na makampuni ya kibepari na
mashirika ya kimataifa kama benki ya dunia ambao wamejichukulia hatua
ya kujadili hatma ya wengi, bila ya wao kusikilizwa na ndani yao kuna
wapambe wasomi wanaotetea mfumo wao wa kibepari.
"Ukweli wa
mkutano huo ni kwamba, ni wa uchumi wa kibeberu na kibepari na watu wa
Afrika hawana budi kuelewa kwa undani na kwa ufasaha mfumo huo ambao
unatawala duniani na kusimamiwa na hao wanaokutana kule Mlimani City.
"Hatuwezi
kuzungumzia ukombozi wa mnyonge na wazalishaji wadogo bila kuelewa
mfumo huo ambao kihistoria na sura yake mpya ni ubepari mamboleo na
sababu waafrika tunaguswa moja kwa moja na mfumo huo," alisema.
Alisema mfumo huo ni unyang'anyi unaolindwa na sheria iliyowekwa na wenyewe na kwa Afrika kumekuwa na mfumo huo kwa karne tano.
Prof.
Shivji alisema kutokana na mifumo kama hiyo kumekuwa na mpasuko wa
kitabaka ambao umeonekana kukua na kuwa na matabaka mawili katika taifa
moja, yaani waliokuwa nacho na wasiokuwa nacho.
"Mwenyezi Mungu
hakuumba matajiri kwa upande mmoja na maskini kwa upande mwingine, wala
mabepari kwa upande mmoja na wafuta jasho kwa upande mwingine, hayo ni
matokeo ya kihistoria," alisema.
Aliongeza kuwa ukweli ni
kwamba ubepari leo hauhitaji Waafrika bali unahitaji Afrika na kwamba
hawana haja ya watu bali wanahitaji vitu, rasilimali na ardhi.
Akizungumzia
suala la maandamano alisema kuyazuia ni kuwanyima watu haki ya msingi
ya kutakiwa kutoa sauti zao ili ziweze kusikika.
Hata hivyo,
licha ya maandamano hayo kuanza na kuishia katika eneo hilo la umbali
mfupi lakini yalikuwa na mbwembwe za aina yake huku yakiongozwa na
mabango yaliyokuwa yamesheheni ujumbe wa aina mbalimbali.
Mbwembwe
hizo ni pamoja na kuwa na kuongozwa na sanamu lilikuwa limevalia kanzu
kubwa lenye maandishi 'Viongozi wa Afrika ni wazalendo au vibaraka'.
Aidha
mabango mengine yalikuwa yakisomeka 'Ubinafsishaji ni ukoloni
mamboleo', 'wawekezaji hawatufai waondoke', 'Vita barani Afrika ni
mbinu za kuchota rasilimali zetu', na 'wanawake ni wakuzaji wa uchumi
katika jamii'.
Awali akifungua mkutano wa Jukwaa hilo mbadala,
Mkurugenzi wa Action Aid International Tanzania, Bi. Aida Kiangi
alisema lengo kubwa la jukwaa hilo ni kujadili kwa mapana na kutoa
mapendekezo kwa viongozi wa mkutano wa WEF juu ya nini kifanyike ili kuona jamii ya Waafrika inanufaika na uwekezaji pamoja na kuwa na usawa katika ukuaji wa uchumi.
Bi.
Kiangi alisema ni dhahiri kwamba kumekuwa na ukuaji wa uchumi kwa nchi
za Afrika lakini wanaonufaika na ukuaji wa uchumi huo ni wachache na
hivyo ni muhimu kujiuliza
ni nani ananufaika na uchumi huo.
0 comments:
Post a Comment