Fredy Azzah
RAIS Jakaya Kikwete, amewaagiza Wakuu wa wilaya zote
nchini kuendesha msako wa nyumba kwa nyumba, kubaini watoto waliofaulu
kuingia sekondari mwaka huu, lakini mpaka sasa wameshindwa kuanza
masomo yao.
Amesema katika kazi hiyo, wazazi wote ambao
waliwazuia watoto wao kuanza masomo ya sekondari kwa sababu yoyote ile
wahojiwe kwa nia ya kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao shule mara
moja.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa
jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, maagizo hayo
yalitolewa, mwanzoni mwa wiki hii mjini Masasi baada ya kupatiwa
maelezo ya Maendeleo ya Mkoa wa Mtwara.
“Alitoa maagizo hayo
baada ya kuambiwa kuwa asilimia 35.6 ya watoto wote 12,843 walioshinda
mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kuingia sekondari
katika Mkoa wa Mtwara, hawajaripoti shuleni mpaka sasa,” ilisema sehemu
ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kikwete
aliambiwa kuwa ni asilimia 64 tu, yaani watoto 8,278 walioripoti na
kuanza masomo ya sekondari wakati watoto 4,565 hawajaripoti shuleni na
hawajulikani waliko.
Ilisema katika idadi hiyo, Wilaya ya
Mtwara ndiyo inayoongoza kwa asilimia 54, ikifuatiwa na Nanyumbu
asilimia 48, Masasi asilimia 35, Tandahimba asilimia 32, Mikindani
asilimia 22 na Newala asilimia 21.
“Rais Kikwete aliambiwa na
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Anatoli Tarimo kuwa baadhi ya sababu
zilizowazuia watoto hao kuendelea na shule ni pamoja na baadhi yao
kupata mimba, kuozwa ama kuzuiwa na wazazi wao kwenda shule,”
Ilifafanua sehemu nyingine ya taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa Mara
baada ya kupewa takwimu hizo, Rais Kikwete alisema “Hizi takwimu ni za
juu sana. Haiwezekani tukaendelea kuwadhulumu watoto wetu maisha bora
kwa kuwazuia wasiende shule wakati shule zipo, nafasi zipo na kila kitu
kipo.”:
“Tafuteni majina ya watoto hawa wote, wazazi wao
waitwe, wajieleze na kama hawana majibu wawajibishwe. Afuatwe mtoto
mmoja baada ya mwingine bila kumwacha yoyote. Na njia rahisi ufanywe
msako wa nyumba kwa nyumba, kama ilivyokuwa zamani wakati wa kukusanya
kodi,”.
Taarifa hiyo ilisema Rais alifafanua kuwa Wazazi wa
watoto hao wahojiwe siyo kwa nia ya kutaka kujua sababu gani zinazuia
wasiwapeleke watoto shule, bali kwa nia ya kuhakikisha kuwa watoto
wanapelekwa shuleni mara moja.
“Kazi hii ifanyike katika kila
wilaya nchini na isimamiwe na mkuu wa wilaya katika kila wilaya ambako
yapo matatizo ya namna hii.” Ilisema sehemu nyingine
Rais
Kikwete alipewa ripoti hiyo ya maendeleo ya Mkoa wa Mtwara, ikiwa
sehemu ya shughuli zake wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo.
Friday, May 14, 2010
JK aagiza wanafunzi watoro wasakwe nyumba kwa nyumba
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Friday, May 14, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment