Imeandikwa na Na Eline Shaidi, Morogoro
POLISI inamshikilia mwanafunzi mmoja kati ya sita wanaosoma katika Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya
mlinzi Jafari Thabiti (38) yaliyotokea Mei 11, mwaka huu.
Mauaji hayo yalifanyika katika kampasi ya chuo hicho ya Solomon Mahlangu iliyopo Mazimbu katika Manispaa ya Morogoro.
Mwanafunzi anayeshikiliwa na polisi ametajwa kuwa ni Yona Mahona
maarufu ‘Ngosha’ (29) ambaye anasoma shahada ya ufugaji wa samaki mwaka
wa pili katika chuo hicho, ambaye alidaiwa kumpiga marehemu na kiti cha
mbao sehemu ya kichwani na kumsababishia maumivu makali ambayo
yalipelekea kifo chake.
Akithibitisha kukamatwa kwa mwanafunzi huyo Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Morogoro, Thobias Andengenye alisema mwanafunzi huyo alikamatwa
juzi, majira ya mchana baada ya polisi kufika katika kampasi hiyo na
kufanya upelelezi juu ya tukio hilo.
Alisema katika upelelezi uliofanywa na polisi ulibaini kuwa
mwanafunzi huyo akiwa na wenzake ndio waliomshambulia mlinzi huyo kwa
kumpiga huku wakimtuhumu kuiba simu ya mkononi iliyokuwepo kwenye bweni
la wanafunzi wa kike, katika kampasi hiyo.
“Tumefanya upelelezi wa kina na tumefanikiwa kumkamata mwanafunzi
mmoja ambapo kutokana na maelezo yaliyotolewa yeye alishiriki kumpiga
mlinzi huyo kwa kiti cha mbao, kwa hiyo tumemkamata mwanafunzi huyu na
bado tunaendelea na upelelezi zaidi juu ya tukio hilo,” alisema
Andengenye.
Katika tukio lingine mtu mmoja ambaye ni Mkazi wa Kihonda katika
Manispaa ya Morogoro, anayedaiwa kuwa ni mwizi Ally Ngavuma (20)
amenusurika kuchomwa moto na wananchi wenye hasira baada ya kukutwa
akiiba mahindi mabichi kwenye shamba lililopo eneo la Kihonda Mbuyuni
katika Manispaa ya Morogoro.
Mtu huyo ambaye aliokolewa na polisi waliofika katika eneo hilo
mara baada ya kukamatwa kwa mwizi huyo, walimkuta akiwa amepigwa sana
na wananchi wa kata hiyo, huku akiwa amelala chini na kufungwa na kamba
tayari kwa ajili ya kumchoma moto.
Thursday, May 13, 2010
Mwanafunzi wa SUA mbaroni kwa tuhuma za mauaji
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Thursday, May 13, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment