Besigye amekuwa akizuiwa kutoka nyumbani
Ubalozi
wa Marekani nchini Uganda umetoa wito kwa serikali ya Rais Yoweri
Museveni kumwachilia huru kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye kutoka
kwa kizuizi cha nyumbani.
Ubalozi huo umesema kiongozi huyo anafaa kuruhusiwa kutembea bila kuzuiwa.
Dkt
Besigye amezuiliwa nyumbani kwake tangu siku ya uchaguzi Alhamisi wiki
iliyopita na hukamatwa na polisi kila anapojaribu kuondoka nyumbani na
kisha kurejeshwa nyumbani jioni.
“Dkt
Besigye amekuwa akizuiliwa na polisi tangu uchaguzi wa tarehe 18
Februari, na hajafunguliwa mashtaka yoyote, na alinyimwa haki yake ya
kikatiba ya kushiriki uchaguzi wa tarehe 24 Februari (uchaguzi wa
serikali za mitaa,” ubalozi huo umesema kupitia taarifa.
Maafisa wa ubalozi huo leo walimtembelea Dkt Besigye nyumbani kwake wakiandamana na maafisa kutoka Umoja wa Ulaya.
Waangalizi wa EU wakosoa uchaguzi Uganda
Baada ya kuzuiwa kwa muda na maafisa wa usalama, mwishowe waliruhusiwa kukutana na kiongozi huyo.
Ubalozi
huo wa Marekani pia umetoa wito kwa serikali kuacha kuhangaisha na
kuwakamata maafisa wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change
(FDC) chake Dkt Besigye.
Aidha, wameeleza wasiwasi wao kutokana na kuchelewa kwa Tume ya Uchaguzi kutoa matokeo kamilifu ya uchaguzi wa urais.
“Hili,
pamoja na kuzuiliwa kwa Dkt Besigye na kukamatwa kwa mawakala wa chama,
kumetatiza uwezo wa raia kutathmini hesabu ya kura na ikiwezekana
kupinga matokeo ya uchaguzi kortini katika kipindi kinachohitajika cha
ndani ya siku kumi,” ubalozi huo umesema.
Dkt Besigye amepinga matokeo ya uchaguzi sawa na wagombea wengine wawili wa urais, Amama Mbabazi na Abed Bwanika.
Mapema leo, mawakili wa Dkt Besigye walisema walikuwa wakitafakari uwezekano wa kupinga matokeo hayo mahakamani.BBC
0 comments:
Post a Comment