Swali kwa TPDC: Kwanini Makubaliano ni tofauti na Mkataba Elekezi (Model PSA)?
Baada
ya kuvuja kwa Mkataba wa kutafuta na kuzalisha Gesi Asilia (PSA) kati
ya Serikali kupitia TPDC na Kampuni ya Norway ya StatOil na baada ya
baadhi ya wachambuzi kuhoji kuhusu mkataba huo, Shirika la TPDC limetoa
maelezo yake. Sio mara moja, sasa ni mara ya tatu.
Kimsingi
TPDC wanasema wachambuzi waliochambua nyongeza hiyo ya Mkataba hawana
uelewa wa mambo haya na wanaleta siasa. Nadhani ni muhimu TPDC
wakajikita katika kueleza kwa lugha ambayo wananchi wa kawaida wataelewa
badala ya kusingizia uelewa wa watu katika masuala haya. Wizara ya
Nishati na Madini haina uelewa wa pekee wa masuala ya Mafuta na Gesi
kama wanavyotaka umma uamini.
Kuna
watanzania wengi tu wenye kufuatilia mambo haya na wenye uwezo mpana
hasa katika masuala ya kodi katika tasnia hii. Ni wajibu wa TPDC kutoa
maelezo yasiyo changanya wananchi na bora zaidi waweke mikataba hii ya
Gesi na Mafuta wazi. Maelezo yaliyotolewa na TPDC mpaka sasa hayaeleweki
na yana lengo la kuwachanganya wananchi kama sio kuwaongopea.
Swali la Msingi
Serikali
kupitia “Model PSA” imeweka viwango vya mgawanyo wa mapato kati ya
Mwekezaji na nchi. Viwango hivi ni vya mgawo wa mafuta au gesi asilia
yanayozalishwa kwa siku. Mkataba huu elekezi upo kwenye tovuti ya
Shirika la TPDC na ndio mwongozo wa majadiliano kwa mikataba yote.
Kwa
mujibu wa Mkataba huu elekezi uzalishaji wa gesi asilia unapokuwa wa
chini kabisa (0 –249.999 MMscf kwa siku) mgawo kati ya Tanzania na
Mwekezaji unakuwa ni nusu kwa nusu (50 – 50 ) baada ya mwekezaji kuondoa
gharama zake zote za uzalishaji.
Iwapo
uzalishaji umefikia hali ya juu kabisa ( 1500 MMscf na zaidi) mgawo wa
Tanzania unakuwa asilimia 80 na Mwekezaji asilimia 20. Mwekezaji
anaruhusiwa kuchukua mpaka asilimia 70 ya Gesi iliyozalishwa kufidia
gharama za uzalishaji. Hivyo, kinachogawanywa ni asilimia 30
zinazobakia.
Mkataba
uliovuja ( TPDC na StatOil hawajaukanusha) unaonyesha kuwa kiwango cha
chini kabisa cha uzalishaji Serikali inapata asilimia 30 tu na Mwekezaji
asilimia 70 licha ya kwamba tayari gharama zake keshajirudishia. Vile
vile kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji mgawo unakuwa sawa kwa sawa!
Swali la msingi hapa ni, Kwanini makubaliano na kampuni hii ya StatOil
yanaenda tofauti na Mkataba elekezi? Je, mikataba yote 26 imekwenda
harijojo namna hii? Maswali haya bado hayajajibiwa na TPDC.
Tuelewe
Mkataba
wa Gesi Asilia au Mafuta ni makubaliano ya kugawana mapato yanayotokana
na kiwango kilichozalishwa. Katika maelezo yao TPDC wanaeleza kuhusu
kodi ya mapato, mrahaba na kodi ya huduma. Kodi ya Mapato na kodi ya
huduma ni kodi ambazo kila mfanyabiashara nchini anapaswa kulipa.
Ikumbukwe kuwa imechukua miaka 20 na kelele nyingi sana mpaka kampuni za
Madini kuanza kulipa kodi ya mapato na ushuru wa huduma.
Mpaka
leo hii bado Halmashauri za Geita na Kahama zinahangaika na kampuni za
Madini kulipwa ushuru huu. Kampuni za Madini na za Mafuta hutumia
mikakati ya kupanga kukwepa kodi (tax planning measures) kwa kutumia Tax
Havens na Mikataba ya Double Taxation Treaties. Hivyo TPDC kusema
tutegemee kodi ya Mapato ni sawa na kuimba kama kasuku na baada ya miaka
20 tutajikuta kwenye lawama zile zile za sekta ya Madini.
Kwenye
baadhi ya mikataba, kodi wanayolipa wawekezaji hukatwa kwenye mgawo wa
TPDC na hivyo kodi hiyo hulipwa na TPDC na sio Mwekezaji kama
tunavyoaminishwa na Serikali.
Kuhusu
mrahaba wa asilimia 5 napo kuna tatizo kwani kwenye mikataba ya Gesi
Asilia Mrahaba unalipwa na TPDC maana ndio mwenye leseni na sio
Mwekezaji ambaye ni kandarasi tu.
Mikataba
kadhaa imeandikwa kwa namna ambayo Mwekezaji akilipa mrahaba,
anajirudishia kwenye mapato ya Gesi kama gharama. Hivyo kimsingi mapato
yetu ya uhakika ni kwenye mgawo wa uzalishaji. Ndio maana tunapiga
kelele kuhusu mkataba huu wa StatOil kwenda kinyume na Mkataba mwelekezi
wa Serikali.
Tutaambulia kiduchu sana
Kwa
kuchambua Mkataba huu kati ya Tanzania na StatOil ya Norway hesabu
zinaonyesha kuwa Nchi yetu itapata mgawo kiduchu sana. Chukulia uniti
1000 za gesi asilimia zimezalishwa kwa siku. Uniti 700 zinachukuliwa na
Mwekezaji kufidia gharama za kuzalisha gesi hiyo na Uniti 300
zinazobakia Mwekezaji anachukua uniti 150 kama mgawo wake wa faida
(profit gas).
Hivyo
Tanzania itabakia na uniti 150 tu kama mgawo wake, sawa na 15% tu ya
Gesi Asilia yote iliyozalishwa katika siku hiyo. Iwapo Mkataba elekezi
ungefuatwa Tanzania ingebakia na uniti 240 sawa na 24% ya gesi asilia
iliyozalishwa.
Natoa
rai kwa vyombo vya habari nchini kuandika masuala haya bila kuyumba
maana yanahusu utajiri wa nchi yetu. Dhahabu imebakia mashimo kwa sababu
Tanzania ililala na watawala kuandika mikataba ya hovyo. Tusilale
kwenye Gesi Asilia. Wakati wa kutaka mikataba kuwa wazi ni sasa. Huu
mmoja tu wa StatOil tunaweza kupoteza shilingi 1.6 trilioni, hiyo
mingine 26 je? Nchi itabakia kweli? Tusikubali majibu mepesi. Tutake
mikataba iwekwe wazi. Uwazi huleta uwajibikaji.
Zitto Kabwe, Mb
17 Julai, 2014
0 comments:
Post a Comment