SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, June 23, 2014

MAKAMU WA RAIS WA CHINA AWASILI NCHINI TANZANIA LEO JUMAPILI

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Li Yuanchao (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Gharib Bilal akikagua gwaride mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere leo 22 Juni, 2014. 
 Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Gharib Bilal (kushoto) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Li Yuanchao (kulia) alipowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere leo 22 Juni, 2014.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Li Yuanchao akipungia mkono viongozi pamoja na baadhi ya watu waliokuja kumpokea (hawako pichani) wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere leo 22 Juni, 2014.
 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wengine wakati wa kumpokea Makamu wa Rais wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Li Yuanchao alipowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere leo 22 Juni, 2014.
 Vikundi mbalimbali vya ngoma vikicheza mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati alipowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere leo 22 Juni, 2014.

PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO.

======== 

MAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Li Yuanchao, amewasili leo (Jumapili Juni 22, 2014)  nchini  kuanza ziara yake ya siku 5 ya Kiserikali hapa nchini.

Akiwa katika uwanja ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mhe. Yuanchao amepokelewa na Mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohammed Gharib Bilal na Viongozi mbalimbali wa Serikali.

Kwa Mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jumapili Juni 22, 2014 na Ofisi ya Intifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika siku yake ya pili ya ziara yake Jumatatu Juni 23, 2014, Mhe. Yuanchao anatarajia kukutana na Viongozi wa Serikali akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Waziri Mkuu Mizengo Pinda Ikulu Jijini Dar Es Salaam.

Aidha mbali na kukutana na Viongozi hao, Mhe. Yuanchao akiwa na Mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mohammed Gharib Bilal pia anatarajia kufungua mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji baina ya Tanzania na China katika  ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania.

Katika siku ya tatu ya ziara yake Jumanne (Juni 24, 2014), Mhe. Yuanchao, anatarajia kukutana na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM akiwemo Makamu Mwenyekiti, Bw, Philip Mangula katika hateli ya Serena na baadaye kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi Mpya za Ubalozi wa China hapa nchini.

Mhe. Yuanchao katika siku ya nne Jumatano (Juni, 25, 2014) ya Ziara yake anataraji kushiriki katika hafla ya ukataji utepe wa kuzinduliwa kwa vifaa vya kubebea mizigo mizito katika ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Reli wa Tanzania na Zambia (TAZARA) na baadae kusafiri na treni kutokea Kituo cha Tazara hadi Yombo akiongozana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Harrison Mwakyembe.

Aidha katika siku hiyo pia, Mhe. Yuanchao anatarajia kukutana na Wawekezaji kutoka China wanaofanya shughuli zao hapa nchini na baadaye kuelekea Zanzibar ambapo atakutana na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Madaktari kutoka China waliopo katika eneo la Vuga.

Aidha katika siku ya mwisho ya ziara yake hapa nchini Alhamisi (Juni 26, 2014), Mhe. Yuanchao akiwa Zanzibar anatajia kutembelea eneo la makumbusho la Stone Town na kujionea makumbusho mbalimbali ya kihistoria ikiwemo Soko la zamani la watumwa. Makamu huyo wa Rais kabla ya kumaliza ziara yake hapa nchini (Alhamisi Juni 26, 2014) anataraji kukabidhi gari la kurushia matangazo kwa Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC) na baadaye jioni kupanda ndege kurejea nyumbani nchini China.

Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
22. Juni, 2014