SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, May 25, 2014

WAPAMBE WAIGHARIMU NDOA YA VICK KAMATA, NDOA YAOTA MBAWA, UKWELI WA HAYA YALIYOTOKEA ANAO KAMATA MWENYEWE

Mbunge wa Viti maalumu CCM, Vicky Kamata, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Tabata General, jijini Dar es Salaam baada ya juzi kupatwa na ugonjwa ghafla wakati akijiandaa kuelekea Kanisani kwa ajili ya kufunga ndoa. Picha na Florence Majani 
HABARI zilizizoufikia mtandao huu zinasema kuwa Kilichotokea na kusababisha Bibi Harusi mtarajiwa Vick Kamata, kuanguka  na kuugua ghafla ni mshituko baada ya Bwana harusi kughaili ghafla kuendelea na wazo lake la kufunga ndoa.
Mtonyaji wa habari hizi ametonya kuwa ikiwa imebaki siku moja tu kufungwa ndoa hiyo, wapambe waliibuka na kumtafuta Bwana harusi na 'kumuuma sikio' yaani kumpa umbea ambao haukuweza kufahamika mapema kuwa ulikuwa ni wa aina gani huku ikidaiwa kuwa Bwana harusi alibadilika ghafla baada ya kukutana na watu hao na kuanza kuonyesha msimamo wake.
Wakati akiendelea na msimamo wake huo, ndipo ikamfikia Bi harusi na kushindwa kufikia muafaka huku Bwana harusi akiombwa kutoendelea na msimamo wake lakini hakuweza kubadili maamuzi, na ndiyo sababo hasa ya Bi harusi huyo kupatwa na mshituko.
Harusi hiyo iliyokuwa ifungwe jana Jumamosi, ilikuwa ni moja kati ya harusi zilizokuwa gumzo kubwa na ikitumia gharama kubwa zaidi jijini dar na hata nchini kote kuwahi kufungwa.
Cha kujiuliza ni kwamba hao wapambe hawakuweza kufanya umbea wao hadi ikiwa zimebaki dakika za majeruhi, na hata kama ni kweli hayo waliyomueleza Bwana harusi kama yalitokea huoni kama yalikuwa ni mchongo laamumu ulioandaliwa maalum???
Pamoja na haya yote lakini bado ukweli atabaki kuwa nao Bibi harusi na Bwana harusi kwa kile alichoelezwa na wapambe hao.
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
KWA UFUPI
  • Augua ghafla, alazwa hospitali, daktari asema  hataweza kuhimili mikiki ya harusi.
  • Ndoa yake gizani, ilikuwa ifungwe leo(Jana) jijini Dar es Salaam
  • Paroko Kanisa Katoliki asema hakukidhi vigezo vya kufunga ndoa
Dodoma/Dar es Salaam. Ni matukio nadra kutokea katika maisha, lakini haya ndiyo yaliyomkuta Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata, baada ya kuugua ghafla saa 36 kabla ya harusi yake.
Kuugua kwa bibi harusi huyo mtarajiwa, kumezua gumzo katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na maeneo mengine nchini, kutokana na kile kilichoelezwa kwamba harusi hiyo ilipangwa kuwa ya kifahari ikitarajiwa kutumia Sh96 milioni.
Kamata ilikuwa afunge ndoa leo katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza Dar es Salaam na tayari kadi za mialiko zilishasambazwa kwa watu mbalimbali wakiwamo wabunge.
Habari za kuugua ghafla kwa mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa muziki aliyetamba na kibao chake cha ‘Wanawake na Maendeleo’ zilianza kuzagaa kwa kasi juzi jioni nchini.
 Kamata ambaye pia ni mtetezi wa haki za wanawake,  aliugua usiku wa kuamkia jana na kupelekwa katika Hospitali ya Tabata General, iliyopo Segerea ambapo amelazwa.
“Niliugua tumbo ghafla, nilipata maumivu makali sana nikampigia daktari wangu na nilipomweleza jinsi ninavyojisikia, aliniambia niende hospitali haraka na kutokana na hali ilivyo, waliamua nilazwe,” alisema Kamata akiwa kitandani katika hospitali hiyo.
Kamata alifafanua kuwa, pamoja na mambo mengine, hali yake ya ujauzito imekuwa ikimsumbua na kuchangia yeye kulazwa kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha wiki mbili. Mbunge huyo ambaye alitakiwa kufunga ndoa leo, alisema kuwa kutokana na maradhi hayo, haelewi hatima ya ndoa yake, ingawa wanafamilia na wanakamati wanaendelea na mipango ya harusi kama ilivyopangwa.
“Mama anaenda nyumbani sasa hivi kuniandalia nguo na kila kitu, lakini sijui itakuwaje kwa sababu daktari amesema kutokana na hali yangu ilivyo, itakuwa vigumu kuvaa viatu virefu na kupata usumbufu wote wa purukushani za harusi,” alisema.
Aliongeza kuwa mipango yote ya harusi ipo tayari kinachosubiriwa na siku yenyewe, lakini kwa bahati mbaya jambo hilo limetokea na haliwezi kuepukika.
Vicky alisema wanakamati wa Dar es Salaam na wale wa Dodoma, wanaendelea na vikao ingawa, wamechanganyikiwa  kutokana na sintofahamu iliyopo, kama harusi itafanyika au haitafanyika.
 Ndugu wa mbunge huyo akiwemo mama yake mzazi Kamata walionekana hospitalini hapo  wakiendelea kumfariji na kujadili kuhusu hatima ya harusi hiyo, iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na wanafamilia wote.
Daktari wa Kamata, aliyefahamika kwa jina la Diwani Msemo, alieleza kuwa mbunge huyo alifika hospitalini hapo akiwa na maumivu makali ya tumbo yaliyofanana na uchungu wa kuzaa, hali iliyoonyesha kuwa ujauzito wake unatishia kutoka.