Meneja wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) kanda ya kaskazini Bw. Cuthbert Mafupa akiwaeleza waandishi wa habari(hawapo pichani) waliotembelea hifadhi ya Chome kujionea hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutunza misitu pamoja na mafanikio yaliyofikiwa katika utunzaji wa hifadhi ya msitu wa Mazingira asilia wa chome (Shengena) ikiwemo kupanda miti katika maeneo yaliyoathika na uvunaji haramu wa rasilimali za msitu huo.
Waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja katika hifadhi ya Msitu Asilia wa Amani, uliopo Muheza Mkoani Tanga wakati wa ziara ya waandishi hao iliyolenga kuwajengea uwezo katika uandishi wa habari za Misitu yenye Mazingira Asilia pamoja na Utalii ikolojia,waliokaa mbele kutoka kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Mvungi, katikati ni Afisa Misitu Mkuu toka wakala wa huduma za Misitu Tanzania Bw. Charles Ngatigwa na kulia ni Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha chanel ten Bw. Kibwana Dachi.
Jengo la kihistoria lililojengwa na wakoloni wa kijerumani mnamo mwaka 1902 katika hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa amani uliopo Muheza Mkoani Tanga, Jengo hilo ni moja ya vivutio vikubwa katika hifadhi hiyo .
Prof. Vicky Mckinley ambaye ni Mtafiti kutoka chuo Kikuu cha Roosevelt kilichopo Chicago,Illinois nchini Marekani akipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutunza hifadhi ya Msitu wa mazingira asilia wa Amani uliopo Wilayani Muheza Mkoani Tanga,wakati wa ziara ya Waandishi wa habari katika Msitu huo hivi karibuni.
Baadhi ya aina za vipepeo wanaopatikana katika hifadhi ya Amani Mkoani Tanga ambao pia wamekuwa moja ya miradi ya kuwaongezea kipato wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kwa kuanzisha vikundi vya kufuga vipepeo hao inayowasasaidia wananchi kujipatia mahitaji yao ya kila siku kwa kuviuza katika nchi za ulaya na Amerika.
Sehemu ya maporomoko ya maji katika hifadhi ya Msitu wa asili ya amani iliyopo Wilayani Muheza Mkoani Tanga ambayo imekuwa kivutio kwa watalii wanaotembelea eneo hilo.
Sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Chome uliopo Same Mkoani Kilimanjaro.
Moja ya Bustani za Miti zilizoanzishwa na wananchi katika kijiji cha Chome ikiwa ni hatua mojawapo ya kupambana na uharibifu wa mazingira na kujiongezea kipato kwa kuuza miti hiyo ambayo huuzwa kwa wastani wa shilingi 300 hadi 500 kwa mti mmoja kutegemea na aina ya mti.
Msaidizi wa Misitu Mkuu ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Zigi katika hifadhi ya Msitu wa asili Amani bw. Mlega Sossele akiwaeleza waandishi wa habari hawapo pichani jinsi wananchi wanavyonufaika na Msitu huo kwa kuwatengea asilimia 20 ya mapato yanayopatikana kwa ajili ya miradi ya maendeleo.Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo.
Serikali yafanikiwa kudhibiti uvunaji haramu wa mazao ya misitu katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia wa Chome (Shengena) Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro kwa kutumia ulinzi shirikishi unaohusisha vijiji 27 vinavyoizunguka hifadhi hiyo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania kanda ya Kaskazini (TFS) bw. Cuthbert Mafupa wakati wa ziara ya waandishi wa Habari waliotembelea hifadhi ya Chome na ile ya Amani iliyipo mkoani Tanga ili kujifunza na kuona hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutunza misitu asilia.
Akifafanua Mafupa alisema kwa kufanya doria shirikishi wamefanikiwa kuondoa wachimbaji wa madini takribani 2000 na kukamata zana mbalimbali kama vile mashine za kusukuma maji (water pump) 20, buleshi 30, sururu 10. “Upasuaji mbao umepungua kutokana na doria shirikishi,na tumefanikiwa kumata misemeno 10 , milango 160 p na vipande 100 vya mbao vilikamatwa” alisema mafupa.
Pia Mafupa aliongeza kuwa Katika Utaratibu wa ulinzi shirikishi idadi ya Mifugo inayoingia katika Msitu huo imepungua toka wastani wa ngombe 50 hadi ngombe 5 wanaoingia ndani ya hifadhi na wahalifu 54 walikamatwa na 16 kati yao wamehukumiwa vifungo na ishirini 29 wamelipa faini, na 9 kesi zao bado zinaendelea.
Katika hatua nyingine Mafupa alisema Wakala wa Huduma za Misitu umewawezesha wananchi kuanzisha bustani za Miti,vikundi vya ufugaji nyuki lengo likiwa ni kuwapa njia mbadala wananchi ili kujipatia kipato na kuondokana na dhana ya kutegemea msitu kujipatia mahitaji yao ya kila siku.
Aliongeza kwa kuwashauri watanzania kutumia fursa ya Utalii ekolijia katika hifadhi za Misitu asilia zilizopo hapa nchini ili kusaidia kuinua pato la Taifa na kuondokana na dhana kuwa Utalii ni swala linalowahusu raia wa kigeni pekee.
Naye Rahel Kisaka mkazi wa kijiji cha Mhero kata ya Chome alipongeza utaratibu ulioanzishwa na Wakala wa Huduma za Misitu kwa kuwajengea uwezo wa kuanzisha bustani za miti ambayo wanauza kati ya shilingi 300 hadi 500 na pia mradi wa kufuga nyuki hali inayochangia kuongeza kipato na kuachana na dhana ya kutegemea msitu huo kwa mahitaji yao ya kila siku.
Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Chome (Shengena) ni msitu wa Serikali kuu unaosimamiwa na wakala wa huduma za Misitu Tanzania kupitia Wizara ya Mali Asili na Utalii na ulitangazwa kwa mara ya kwanza kuwa msitu wa hifadhi mwaka 1951 kwa tangazo la Serikali Na.125 la tarehe 25/5/1951 ambapo katika msitu huo kuna vivutio vya aina mbalimbali wakiwemo ndege,miti na ina ukubwa wa hekta 14,283.