Ndugu zangu,
Machi 6 niliandika mtazamo wangu juu
ya namna ya kwenda mbele kwenye Bunge Maalum la Katiba. Maana,
zilishaonekana ishara mbaya, kuwa tuliowatuma Dodoma wako katika hatari
ya kukwamisha mchakato mzima kwa kujikita kwenye kupigania kisicho na
maslahi ya nchi hii kwa miaka 50 au 100 ijayo.
Wanapigania yaliyomo kwenye kanuni 36
mpaka 37 . Inahusu namna watakavyofikia maamuzi, kuwa iwe ni kwa kura za
faragha au dhahiri. Ndio, inahusu kura za siri au kura za wazi. Ni
kanuni hizi ndizo kimsingi zitakazoamua, kwa namna moja au nyingine,
uhai wa mchakato mzima wa kuitafuta Katiba.
Tuliowatuma Dodoma wamejigawa katika
makundi ya ' Sisi' na ' Wao'. Wanatafuta kushindana na kupata mshindi
badala ya kutafuta muafaka wa Kitaifa. Na hakika, kama alivyopata kusema
Rais wa Nchi, Jakaya Kikwete, kuwa kwenye kushindana huko hakuna
atakayeshinda. Tutashindwa Sote. Na huo ndio UKWELI.
Hakika, huu ni mtihani mgumu ulio
mbele yao tuliowatuma Dodoma. Wakishindwa mtihani huu, basi, ishara
zinazoonekana ni za mkwamo wa jumla wa mchakato mzima. NI AIBU.
Tuliowatuma Dodoma hawajachelewa
kuitafuta hekima na busara kutunusuru na aibu kubwa ya taifa iliyo mbele
yetu. Tuliowatuma Dodoma wawafikirie pia watoto wa kesho na wa vizazi
vijavyo katika nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda.
Nilishauri hapa, kuwa ni heri
kukubaliana kutokubaliana, na hivyo, kusitisha kwa muda mchakato huo,
kuliko kulazimisha kwenda mbele. Ni ushauri pia, kuwa ni heri kuyatafuta
maridhiano kwanza kabla ya kuingia kwenye majadiliano, kuliko
kuyatafuta maridhiano baada ya kuingia kwenye mapigano na kujeruhiana.
Ni busara basi, tuliowatuma Dodoma wakaunda Kamati Maalum ya kuyatafuta
maridhiano . Na ifahamike, kuwa MARIDHIANO ndio msingi wa UHALALI wa
mchakato na hata Katiba yenyewe.
Ni jambo zuri kuona kuwa Mwenyekiti
Kificho naye alishaliona hilo, na kuwa suala la kanuni za 36 na 37
ameliundia Kamati ya maridhiano. Ni njia sahihi na iliyojaa busara na
hekima anayowapitisha Mwenyekiti Kificho.
Maana, tusipotanguliza busara, hekima
na maslahi ya taifa, yumkini yaweza ikawa kama yale aliyopata kuyasema
miaka 60 iliyopita, mwandishi yule mahiri, Mtanzania mwenzetu Shaaban
Robert, aliandika; " Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya
kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka wa matendo yetu mabaya ya
zamani.
Nyoka mwenyewe amekwishakimbia.
Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika
jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema ni kuzuia sumu hii isienee
miilini mwetu ikaleta kifo.
Maovu yana hatari kubwa kukaa kati
yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea faida ila hasara,
huzuni na kilio siku zote."- Shaaban Bin Robert.
Maggid Mjengwa,
0754 678 252
0754 678 252
0 comments:
Post a Comment