Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akilihutubia na kuzindua Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma leo jioni.
===****===
===****===
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa
ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba
katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja
kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka
za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima,
umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio
yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu
kuongoza Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata
ni kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe
wenzenu kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba
mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa
jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la
Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana
katika historia ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi
yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika
kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na
wengi. Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu
kwa kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo
bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha
umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa
Tanzania, licha ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo
watokako, au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama
vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu nchini.
Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa
sheria, utawala bora na kudhibiti maovu.
Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka
mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika
sawia na maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga
Katiba mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya
Muda na mara ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu
tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato
unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kutoa
maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi
wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata
nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili
Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao
kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo
Tume za Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika
mchakato huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge
Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na
wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi
mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa
sasa utaishia kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa
Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge
Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara
14. Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko
muhimu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa
nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
- Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
- Mabadiliko ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
- Mabadiliko ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
- Mwaka 1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
- Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
- Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali
kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na
kufanya yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai
yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako
watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi
kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa
mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa
imani, eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata
katika mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano,
imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya
Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na
viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati
ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha
mchakato wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika
mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania
kwa makundi yao ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia
riziki na kwa maeneo wanayotoka katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa
kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18
Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo,
mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya
wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na
kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu
ya Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa
na Katiba mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi
kupiga kura ya maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba
mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza
kazi tarehe 2 Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote
zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume
na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa
Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge
hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili,
kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa
kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au
HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti
mengine yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha
20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya
Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila
mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya
Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka
zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya
hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo thabiti
kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba,
Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo
yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph
Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia
ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la
kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele
ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211
kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya
wananchi, kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe
wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba
iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza
kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi
wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana
ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa
la Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume
imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha
Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati
tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu
za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa rahisi
kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na ibara 271.
Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila
kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika
kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura,
ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno. Hamna
budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na
kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au
kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora.
Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu
kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung’unikiwa na
watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda
mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia
balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa
katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile
ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua
inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya
ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni
kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi
ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya
vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko
inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo
kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye
Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable).
Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima
yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba
tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu
kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi
wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza
kuwepo athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2
ya Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo
inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote
la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu
yetu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja?
Je hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora
sehemu zetu hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu
haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo
Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi
ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa na muundo wa
Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni
majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo ya
taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa
malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa
Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi na
maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda,
biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako chini ya
mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali ya Muungano
ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji,
Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa
Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya
Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na
migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua
mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali
ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka
masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka
ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali
mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila ya
matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya
Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo.
Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini
mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa
ambayo yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo
mbalimbali. Nawaomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila
kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa yake.
Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji
mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote.
Niruhusuni nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika
Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d)
inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi
za Mbunge kwa miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi
ndani ya gereza”.
Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama
amepatikana na hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini,
isijekuwa yuko rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija
kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa
jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na
kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo
sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili
lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita mfululizo”
ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili kufanywa na
Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza
kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa
miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika
mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977
tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa
na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli
anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili
aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie
watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema
jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au
hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi
vitatu kwa Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu
mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni
vizuri mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya
hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka
ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini,
kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa
kwanza. Nashawishika kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa
na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za
uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa
kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja
linaonekana kuwa jambo jema lakini naomba athari zake mzitafakari
vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha
Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya
wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa
wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira
hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa
Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya
kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa
thamani inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe
kama jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano
kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia
za karibu watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa
Serikali tatu badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala
mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika
Rasimu ya pili. Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali
kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu
linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi
yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania
anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa
watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio
sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara
kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa
nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na
matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde
Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu
si jambo jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi
zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume
ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia
na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo
mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais
wa Jamhuri ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume,
aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua
kuchagua Muungano wa Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili
kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na
Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa
kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika
mjadala huu. Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu
Nyerere na Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo
kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi
yetu. Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai
kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora
zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe
tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame
hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za
kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa
Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye
uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali
tatu. Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote
Zanzibar na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania
waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3
wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu
ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa
changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na
watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali
katika jamii. Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo.
Wapo wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono
muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki.
Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape
uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo.
Wanasema kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni
yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6
hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia
kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania
wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye
idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia
Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa
kuhusu kufaa kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu
changamoto nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri
changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar
wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano
kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema
mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa
mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia,
wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya
kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar
kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko
kuwa Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa
Tanganyika na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi
yao ndani ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina
bendera yake, wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema
Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua
madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge
lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika
Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki
ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki
hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu
ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu
lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu
badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu
utagawanya vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano.
Unawezesha Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa
kihistoria na kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar
kumezwa na Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha
mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza
ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia
kukuza maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na
kupendekeza kuwa muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua,
Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa na muundo
wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali
mbili unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia
kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya
wananchi wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo;
na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa
kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha
amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa
changamoto za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una
changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa
na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji
Joseph Warioba alitutoa hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu
alikuwa na mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani
kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo,
(Waulizeni Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho
isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la
uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi
washirika. Vilevile, kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au
kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya
washirika wa Muungano na baina ya nchi washirika na Serikali ya
Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za
kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila upande
kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision making)
katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto
hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata
uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana
ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue
Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa
Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto
zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali
tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza maradufu
kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika muundo wa
sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza kushugulikiwa na
kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa
mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia changamoto za
Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda
Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili
mwaka 1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na
Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa
kero zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006
yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
- Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
- Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
- Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
- Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
- Usajili wa vyombo vya moto.
- Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu
wa mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu
yafuatayo:
- Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
- Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
- Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali
kadhalika, katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015
– 2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya
Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa
matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu,
naamini tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11
ya awali, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya
kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa,
ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali ya Muungano
kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na, wala
siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi
yao. La hasha.
Pili, naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya
Mambo ya Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na
iliyokubalika na pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja
lililoingizwa kwenye Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki za kikatiba
na kisheria zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa
uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi
mbili ya kura za kila upande wa Muungano. Kumbukumbu zipo katika
Hansard za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka
kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na undani wa
kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
- Mambo ya Nje,
- Ulinzi,
- Polisi,
- Hali ya Hatari,
- Uraia,
- Uhamiaji,
- Biashara ya nje na mikopo,
- Utumishi katika Serikali ya Muungano,
- Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
- Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi kufikia 22,
kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye
ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano
zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za
kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo
kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
- Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
- Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
(a) Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c) Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27
ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni
pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya
Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara,
Usafiri wa Majini na kadhalika.
- Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
- Tarehe 22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
- Mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
- Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini
kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na
sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na
mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi
yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kila yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa
Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi.
Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo
yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni
rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya
siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba,
iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa
kufanya baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru
wa kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za
Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya
mapato, leseni za biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na
kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na
imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia fursa
ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta
na gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana
tangu wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais
Shein msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka
kwa fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha
Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato
huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka
ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo
ya wahenga ya “subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema
tumefika mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili
zilizotushawishi kuamua kuitoa rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo
hufanywa na makampuni binafsi. Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na
gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye
mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au
kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa upande wa
Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake ya
kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na
kukubaliana tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya
kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi
za nje bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna
mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi
kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa
nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha
kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache
kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo
Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa
ufumbuzi tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano
wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato
huu kuyamaliza mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika
Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili.
Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na
ushirikiano na jumuiya au taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa
mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila
kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza
kutolewa kwa Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali
tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu
yake. Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo
kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba
ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe
kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande
zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali zetu
mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana budi upewe
nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka mambo yote
sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye
Serikali tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri
kuhusu changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya
kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu
na wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito
unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa
mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano inayopendekezwa
haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za kusimama.
Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani
ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa
washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha
mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake.
Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza
mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa
vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake chenyewe cha kukusanya
mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika kuikusanyia na
kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama
wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika
kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za
kuhakikisha kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina
mamlaka ya kuzibana nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha
zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya
Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo
ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa
kama chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini,
kwa sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa
Serikali hiyo kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake
hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo
haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha
misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au
chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la
kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni
wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa
Serikali tatu unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo
wa Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano
yenye nguvu na inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona
kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima
mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu
unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi
kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza
kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili
wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo
ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic sentiments)
wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana
mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu
ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao.
Naona hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa
changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe
mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi
hayakwami kwani yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa
zimekwama. Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano
utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza
kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings)
kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa
sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kidugu
na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi moja yaani
Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa
sensa iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania
waliopo sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni
Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza
kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa
utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao
siyo kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata
waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu
waliokuwa ndugu mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza
kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa
sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao
wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila kitu
walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume
imeziona, ni za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu
wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar
mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa
Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii
yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza
baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na
kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne,
ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu
utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi
wetu, hatuna budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye
uamuzi ulio sahihi. Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu
wanafukuzana, wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo
Muungano kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee
wetu waasisi waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao
na maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu
tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta
tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si
matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu
si kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi
nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko
mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda,
nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia
Rasimu na kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi
iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza,
jukumu lenyewe la kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi
yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi
mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito
wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu
sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni
muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu
na Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa
kujadili Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya
watu wachache, mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza
kupata fursa ya kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo
linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa
ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki
kujadili kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu
mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama
stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya
kutambua kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho,
Spika wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge
hili. Kazi yake haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na
ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili
pongezi zetu sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge
hili bila ya kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa
Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
kwa hatua mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua
ya awali hivyo hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa
mijadala yenu hii inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania.
Wamewekeza sana matarajio yao kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya
uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa lugha na
vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge
hili, baadhi ya wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya
Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia
maneno waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya Watanzania wote
kuwa hali ile haitajirudia tena katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali
Watanzania wakakata tamaa na Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu
sana kwa mustakabali wao na wa nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga
kelele (argue don’t shout) au kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha
isiyokuwa ya staha katika kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi,
kutishiana hili na lile au hata kugombana. Ni utovu wa uungwana
usiotegemewa kutoka kwenu. Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania
wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na
kujali maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi
yenu binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania Kwanza”.
Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo kwa kila
jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au
makundi yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama
misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga. Hata hivyo, mnachotegemewa
kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu mazuri na
ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora.
Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza mawazo ya wengine,
hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho chema kwa
yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni watu usiokubaliana nao au
huwapendi au hampendani.
Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya
hivyo hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya
kuwazidi maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute
namna ya kushirikiana na kuwasiliana na makundi mengine.
Msitafute kushindana, hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa
mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote washinde kwani wao ndiyo
wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na asasi
mbalimbali kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za
mawasiliano, mashauriano na ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta
maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu
nzuri za kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara
zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi
wetu wa dini tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa
kutunga Katiba uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze
kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila
watakaloliamua. Baada ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie
kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya
kulihutubia Bunge Maalum la Katiba.
Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu Libariki
Bunge Maalumu la Katiba! Asanteni sana
kwa kunisikiliza!
Bunge Maalumu la Katiba! Asanteni sana
kwa kunisikiliza!