--
- Kwa kutoa mikopo isiyo kuwa na riba.
- Kurudisha mkopo kwa awamu mbili baada ya mwezi mmoja wa biashara.
Katika kupambana na wimbi la kupunguza umaskini hapa
nchini,Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia mradi wake
wa kuwakopesha wanawake wajasiriamali wadogo ujulikanao kama M-Pesa
Women Empowerment Initiative (MWEI),imewakopesha wanawake wajasiriamali
wadogo zaidi ya 150 wa kijiji cha Luhembe wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro,
wamepatiwa mkopo huo usio na riba wa zaidi ya shilingi Milioni tisa.
Wanawake hao waliodai kutumia fedha hizo kuboresha
mitaji yao kibiashara ili kujikwamua na umaskini, walisema hii ni mara
ya kwanza kupata mkopo wa aina hiyo wenye masharti nafuu, ambapo wanalipa
kiasi kile kile cha fedha ambacho wanakuwa wamekopa.
Baadhi ya wanawake hao wenye mitaji ya kuanzia shilingi
elfu tano hadi laki moja walionufaika na mikopo midogo midogo kupitia
MWEI, walisema wataweza kutumia mikopo hiyo kukuza biashara zao, sambamba
na kubuni biashara mpya kuendana na mazingira yaliyopo ili waweze kuzalisha
zaidi na kulipa mikopo hiyo kwa wakati.
Akizungumzia mkopo huo, Meneja wa Vodacom Foundation,
Grace Lyon,alisema Mradi huo ulioanza miaka mitatu iliyopita unalenga
kuwasaidia wanawake wajasiriamali wadogo wadogo vijijini kwa kutumia
njia ya M-PESA, na kwamba tayari wameshavifikia vijiji 42 hapa nchini,
huku mkoa wa Morogoro Luhembe kikiwa ni kijiji cha nne, vingine vikiwa
ni Mkuyuni, Kimamba na Mkamba.
Meneja huyo alisema mama ndiye kichwa cha familia,
hivyo kumuwezesha mwanamke ni kuiwezesha jamii nzima,pia alitumia frusa
hiyo ya kuwaasa wakina mama hao kutumia mikopo wanayopewa kwa shughuli
za maendeleo ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwani masharti ni nafuu
na mwezi wa kwanza unatakiwa kutumia kwa ajili ya biashara na mwezi
unaofuata utakuwa kulipa nusu ya fedha waliyokopeshwa na nusu nyingine
kumalizia mwezi mwingine bila riba yeyote.
Alisisitiza mkopo huo unalenga kuimarisha biashara
na sio kufungua biashara mpya, na kuwahimiza kurudisha marejesho ili
waweze kupata mkopo mara mbili zaidi ya waliochukua awali.
Akizindua mikopo hiyo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro, Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo aliipongeza Vodacom
kwa hatua hiyo ya kulenga kupunguza umaskini kwa kinamama wajasiriamali,
ambapo kitendo wanachofanya ni kuunga mkono jitihada za Serikali za
kupambana na umaskini.
Aliwaasa wakina mama wanaofaidika na mikopo hiyo
kutambua masharti ya mikopo, ikiwemo kuhakikisha wanarudisha fedha walizokopa
baada ya kuzalisha, ili fedha inayopatikana iweze kusaidia wanawake
wengine wenye mahitaji zaidi kama wao na kujenga uaminifu wa kujiongezea
kupata mikopo zaidi ya awali.
“Hii ni fursa nzuri kwenu ya kuondokana na umaskini,
mikopo ndio chombo pekee cha kuweza kutukwamua na umaskini, muhimu ni
kujipanga ujue unawekeza wapi, shughuli gani, ili mwisho wa siku uweze
kurudisha mkopo na kupata ziada ya kuendeleza biashara zako, jitahidini
mfike mahali msimame wenyewe na hatimaye kuendesha vyema maisha yenu”Alisema
Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake Richard Kigave, afisa mtendaji kata
ya Luhembe,aliwaasa mikopo waliyopewa waitumie kwa malengo yaliyokusudiwa
na iwapo watakiuka kulipa kwa wakati, wataishia kwenye mkono wa sheria.
“Inaonekana Vodacom walitizama wana Luhembe wakaona
kweli tuna shida kubwa na hali ngumu hivyo tunahitaji kujikwamua na
umaskini na wakaamua kutuletea hii mikopo,sasa sitegemei kupokea
mgogoro wowote unaohusu ninyi na kampuni hii iliyokuja kwa nia njema”Alisema
Mtendaji huyo wa kata.
Mwisho ...
0 comments:
Post a Comment