SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, February 5, 2014

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar afanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China

Balozi Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Yunliang akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Yunlia aliyefika Ofisini kwake kusalimiana naye. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imesisitiza kuendelea kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Maendeleo za Wananchi wa Zanzibar kwa kusaidia miundo mbinu sambamba na ufadhili katika miradi tofauti kwa lengo la kustawisha Jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang alipokuwa akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Xie Yunliang alisema Miradi ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Zanzibar kama vile ujenzi wa Hospitali ya Abdula Mzee Mkoani Pemba na Uwanja wa Ngege wa Zanzibar ni uthibitisho kamili wa Ushiriki wa China katika kusaidia maendeleo ya Zanzibar.

Balozi huyo mdogo wa China hapa Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba tayari ameshafanya ziara maalum ya kukagua baadhi ya miradi inayosimamiwa na Nchi hiyo pamoja na kukutana na Taasisi na wahandishi wa miundo mbinu na makampuni ya Nchi hiyo yanayofanya kazi hapa Zanzibar na kuridhika na hatua inayoendelea kuchukuliwa na Taasisi hizo.

Balozi Xie aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha upatikanaji wa eneo lililokubaliwa kutumiwa katika upanuzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba ambalo bado linaonekana kuendelea kuwepo baadhi ya majengo ya ibada na Makazi ya Watu.

Alisema upatikanaji wa eneo hilo utasaidia kurahisisha ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali hiyo kwenda kwa wakati uliopangwa ili kuepuka hasara zinazoweza kuleta usumbufu hapo baadaye.

Akizungumzia suala la uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mtaa wa Kikwajuni Mjini Zanzibar Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang alisema ushauri wa suala hilo tayari limeshawasilishwa kwa Serikali ya China kwa hatua za utekelezaji.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya China inathamini sana uwamuzi wa Zanzibar wa uwanja huo kuitwa jina la Mwenyekiti wa Chama cha Kikoministi cha Nchi hiyo Mao Tse Tung na kuahidi kwamba mipango itaandaliwa katika kuona kiwanja hicho kinapatiwa hadhi kama kilivyo jina lake.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ukarimu wake wa kuuhudumia Ujumbe wa China ulioshiriki maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiongozwa na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ya Nchi hiyo.

Alisema ujumbe huo umefarajika na mapokezi makubwa uliyoyapata ambayo yamethibitisha uhusiano wa Kihistoria na wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa China.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa misaada yake mbali mbali inayotowa kwa Zanzibar ambayo imepunguza kasi ya ukali wa maisha.

Balozi Seif litolea mfano wa Ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Pemba ambao kwa kiasi kikubwa utakapokamilika kwake utapunguza usumbufu kwa Wananchi wa Kisiwa cha Pemba wa kufuata huduma za Afya Kisiwani Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuahidi Balozi Mdogo huyo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili utaendelea kuimarisha kwa faida ya wananchi wake.

China imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kusaidia maendeleo mbali mbali mara tu baada ya Zanzibar kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 y a kuondosha utawala wa kikoloni.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/2/2014.

0 comments:

Post a Comment