Rais wa Chama cha Wafanyabiashara,Wenyeviwanda na Kilimo (TCCIA) Injinia Peter Chisawillo akizindua rasmi utafiti utakaohusisha ukusanyaji wa maoni kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS Mobile System) kuhusu madhara yatokanayo na urejeshwaji wa ada za biashara kila mwaka kwa lengo la kuishawishi serikali kuweka sera, sheria na taratibu rafiki kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini leo jijini Dar es salaam.
******
TCCIA YAZINDUA UTAFITI KUKUSANYA MAONI YA WAFANYABIASHARA KUHUSU ATHARI ZA UREJESHWAJI WA ADA YA LESENI ZA BIASHARA.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
16/5/2014, Dar es salaam.
Chama cha Wafanyabiashara,Wenyeviwanda na Kilimo (TCCIA) kimezindua rasmi utafiti utakaohusisha ukusanyaji wa maoni kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS Mobile System) kuhusu madhara yatokanayo na urejeshwaji wa ada za biashara kila mwaka kwa lengo la kuishawishi serikali kuweka sera, sheria na taratibu rafiki kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Akizungumzia utafiti huo leo jijini Dar es salaam Rais wa cha hicho Injinia Peter Chisawillo amesema kuwa mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 serikali ilitangaza urejeshwaji wa ada ya leseni za biashara nchi nzima na kuongeza kuwa utaratibu huo unaomlazimu mfanyabiashara kukata leseni na kuilipia kila mwaka unakwenda kinyume na sheria ya leseni ya mwaka 1972.
Amesema kuwa sheria hiyo na hasa marekebisho yake ya mwaka 2004 yaliwezesha leseni za biashara kutolewa bure na mara moja tu kwa kipindi cha maisha yote ya biashara jambo ambalo linakiukwa.
“Tayari kuna malalamiko mengi kwa jumuiya ya wafanyabiashara yanayotufikia kutoka kuanzia ngazi za wilaya na mikoa juu ya urejeshwaji wa ada hiyo, sekta binafsi inailalamikia serikali kwa kutoishirikisha katika urejeshaji wa utaratibu huu ambao unaiathiri sekta hii moja kwa moja” amesema Injinia Chisawillo.
Ameeleza kuwa sekta binafsi inaamini kuwa serikali imeamua kuongeza mapato bila kuzingatia nia ya urasimishaji wa sekta isiyo rasmi kwa lengo la kuharakisha uchumi kwa ujumla na kuongeza kuwa hakuna mwongozo maalum uliotolewa na serikali kuelekeza namna maombi ya leseni yatakavyoshughulikiwa.
Amesema sekta binafsi inaamini kuwa ili kuondoa urasimu na usumbufu kwa wafanyabiashara pindi wanapoomba leseni kila mwaka , serikali itumie kumbukumbu zilezile kila mwaka bila kulazimu mfanyabiashara kufuata mlolongo wa taratibu za kuomba leseni kila mwaka kwa lengo la kuokoa muda na kupunguza kupanda kwa gharama za uendeshaji wa biashara.
Aidha Injinia Chisawillo amesema kuwa utafiti huo unaofanywa na TCCIA) utafanyika kwa muda wa wiki 4 ukiwahusisha wanachama wote takribani 22,000 (Elfu Ishirini na mbili) na wale wasio wanachama na unafadhiriwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la BEST –AC ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu zao kwenda namba 15539 na kutoa maoni kuhusu urejeshwaji wa ada hiyo
0 comments:
Post a Comment