Msemaji toka Wizara ya Kazi na Ajira Bw.Ridhiwan Wema(Kulia) akieleza
kwa waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Bodi za Mishahara Kisekta kwa mujibu wa sheria
Na. 7 ya Mwaka 2004 ya Taasisi za Kazi katika Sekta Binafsi, wakati wa
Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo jijini Dar
es Salaam. Kushoto ni Mchumi Mwandamizi wa Wizara hiyo Bw. Jofrey Mashafi.
Afisa Kazi Mwandamizi toka Wizara ya
Kazi na Ajira(kulia) akieleza kwa waandishi wa habari(Hawapo pichani) jinsi
ukuaji wa sekta unavyochangia kuanzishwa kwa bodi ya Mshahara kwa Sekta
husika wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) Leo jijini Dar es Salaam. Msemaji Wizara hiyo Bw.Ridhiwan Wema.
Mchumi Mwandamizi toka Wizara ya Kazi na
Ajira Bw. Jofrey Mashafi (kulia) akieleza mipango ya serikali ya kukabiliana
na tatizo la upungufu wa Ajira Nchini ikiwa ni pamoja kuanzisha programu ya
miaka 3 inayoratibiwa na Wizara ya Kazi na Ajira kwa kushirikiana Chuo cha
Sokoine na Bank ya CRDB ya kuwajengea
uwezo wahitimu wa vyuo vikuu, inayotarajiwa kuzalisha ajira 30,000, wakati wa
Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Leo jijini Dar
es Salaam. Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Georgina
Misama. Picha na Frank Mvungi
---
Na Frank Mvungi
WIZARA ya Kazi na Ajira imewaasa waajiri katika Sekta binafsi
kuzingatia Sera na sheria za kazi mahali pa kazi ili kuleta tija na nidhamu
kazini.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara hiyo Ridhiwani Wema wakati wa
mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, akieleza kuhusu
utaratibu wa uanzishwaji wa Bodi za mishahara kisekta ili kusaidia kuboresha
maslahi ya wafanyakazi.
Wema amevishauri vyama vya wafanyakazi kuboresha mishahara na
maslahi ya wafanyakazi kupitia majadiliano ya pamoja sehemu za kazi kwa kuwa sheria na kanuni zinatoa na kuhimiza
haki hizo.
Alizitaja bodi za mishahara zilizoanzishwa kuwa ni kilimo, Afya,
Biashara na Viwanda, Mawasiliano, Madini, Uvuvi na huduma za majini, hoteli na
huduma za majumbani, na ulinzi binafsi.
Wema alifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2011 hadi sasa
ziliundwa bodi 4 za mishahara kufanya jumla ya bodi za kisekta kuwa 12 hadi
mwaka 2013.
“Moja ya majukumu ya bodi ni kufanya uchunguzi kuhusu kima cha
chini cha mishahara na hali ya ajira katika sekta husika ambapo pia humshauri Mhe. Waziri kuhusu kima cha
chini cha mishahara pamoja na masharti ya ajira katika sekta husika”, alisema
Wema.
Alibainisha kuwa Bodi za ajira zimetembelea mikoa ya Daressalaam,
Mororogoro, Pwani, Dodoma, Arusha, Mwanza, Tanga, Manyara, Iringa, Mbeya na
Kilimanjaro ili kijionea mazingira ya kazi na kupata maoni ya wadau kuhusu kima
cha chini cha mishahara katika Sekta husika.
Msemaji huyo aliongeza kuwa vyama vya wafanyakazi vina nafasi
kubwa kusaidia katika kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi kupitia majadiliano
ya pamoja sehemu za kazi kwa kwa kuwa sheria na kanuni zinatoa na kuhimiza haki
hiyo.
Naye Afisa Kazi Mwandamizi Idara ya Ajira, Ayubu Musa alisema kuwa
wizara hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa taratibu, sheria na
kanuni za kazi zinazingatiwa ambapo wamekuwa wakifanya ukaguzi mara kwa mara
ili kuhakisha kuwa kuna mazingira bora na maslahi ya wafanyakazi katika sekta
binafsi.
Bodi
za mishahara kisekta zinaundwa kwa mujibu wa sheria ya Taasisi za kazi namba 7
ya mwaka 2004 ambapo kila bodi inaundwa na wajumbwe 8 akiwemo mwenyekiti na
wajumbe wanaowakilisha maslahi ya Serikali wajumbe 2,waajiri wajumbe2 na
wafanyakazi 2 katika mfumo wa utatu.
0 comments:
Post a Comment