SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, October 9, 2013

Kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR):Matokeo ya tafiti za NIMR kuendelea kuwanufaisha watanzania.

 
 Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Dr. Julius Massaga akieleza kwa waandishi wa Habari jinsi wanavyoshirikiana na Taasisi za kimataifa katika kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa Malaria,wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam.

 Mtafiti Mkuu na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano  kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Bw. Leonard Mboera(kulia) akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu Mifumo mbalimbali ya utoaji taarifa za Tafiti zinazofanywa na Taasisi hiyo,wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Afisa Hbari wa Idara ya Habari(MAELEZO) Bw. Frank Mvungi.Picha na Hassan Silayo

--
 TAASISI YA TAIFA YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU
 KUKUZA MATUMIZI YA MATOKEO YA TAFITI ZA AFYA

---
UTANGULIZI
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu ilianzishwa kwa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Namba 23 ya mwaka 1979. Makao makuu ya Taasisi yako Dar es Salaam. Taasisi ina vituo vikuu saba (Amani, Mbeya, Muhimbili, Mwanza, Tabora, Tanga, Tukuyu na Ngongongare) na vituo vidogo saba (Amani Hill, Gonja, Handeni, Haydom, Kilosa na Korogwe).

Majukumu ya Taasisi
1. Kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti wa afya Tanzania
2. Kufanya utafiti wa afya ili kupunguza magonjwa yanayosumbua jamii ya Watanzania
3. Kufaya utafiti wa tiba asilia na tiba mbadala
4. Kusajili tafiti za afya zinazofanywa nchini
5. Kuwapa uwezo Watanzania katika kufaya tatifi wa afya
6. Kukuza matumizi ya matokeo ya tafiti za afya
 
Taratibu za Kitafiti
Mzunguko mzima wa utafiti unahusisha mambo yafuatayo:
1. Maandalizi ya Rasimu
2. Maombi ya Kibali cha Kufanya Utafiti kinachozingatia maadili ya utafiti unaojumuisha binadamu
3. Maandalizi ya Utafiti
4. Ukusanyaji wa takwimu
5. Menejimenti ya takwimu na mchanganuo wake
6. Matayarisho ya Taarifa ya Utafiti
7. Uwasilishaji wa matokeo kwa wadau mbalimbali (Mikutano, Warsha, Kongamano, Tovuti)
8. Uchapishaji wa Taarifa ya Utafiti katika Ripoti na Majarida ya Sayansi
9. Uandaaji wa muhtasari wa utafiti kwa ajili ya sera na uboreshaji wa utendaji

UWASILISHAJI WA MATOKEO YA UTAFITI
Taasisi inatumia njia mbalimbali kuwasilisha matokeo ya tafiti kwa walengwa. Njia hizo ni pamoja na zifuatazo:

Warsha, Semina, Makongamano na Mikutano
Ni utaratibu wa Taasisi kuwataka watatifi wote kuhakikisha kuwa mrejesho wa matokeo ya utafiti unawashirikisha wananchi walioshiriki katika utafiti huo na Kamati ya Menejimenti ya Afya ya Halmashauri husika. Taasisi ina utaratibu wa kutoa mrejesho wa matokeo ya tafiti zake katika ngazi za jamii, wilaya na Taifa ili walengwa waweze kujua matokeo ya tafiti zilizofanywa katika maeneo yao.

Matokeo ya utafiti huwa yanatolewa kwa wadau wengine kupitia makongamano, warsha, mikutano na semina zinazoandaliwa hususani, katika ngazi ya Kitaifa. Wadau wakuu wa utafiti wa afya, ikiwemo watunga sera na watoa maamuzi hualikwa katika warsha hizo. Katika siku za karibuni, matokeo ya utafiti yamekuwa yakitolewa kupitia Kalenda na Maonesho ya Wazi.

Taasisi huandaa Kongamano la Sayansi la kila mwaka linalokutanisha watafiti, watunga sera, waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Madhumuni ya Kongamano hili ni kuwasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali za Afya; kubadilishana uzoefu katika tafifi za Afya na kupanga vipaumbele vya tafiti za Afya. Hadi kufikia 2013, makongamano 27 yameandaliwa na Taasisi.

Mikutano na Waandishi wa habari nayo imekuwa ikitumika katika kuwasilisha taarifa mbalimbali za matokeo ya tafiti.


Majarida ya Kisayansi
Jarida la Utafiti wa Afya Tanzania
Taasisi inachapisha matokeo ya tafiti mbalimbali katika jarida lake la Utafiti wa Afya Tanzania (Tanzania Journal of Health Research) linalochapishwa mara nne kwa mwaka (Januari, Aprili, Julai na Oktoba). Jarida hili lililoanzishwa mwaka 1997, huchapishwa kwa njia ya nakala za karatasi na kwa mtandao wa ki-elektroniki kupitia tovuti ya taasisi (www.nimr.or.tz).

Malengo ya kuanzishwa kwa jarida hili ni kutoa tarifa za kitafiti kwa wakati kwa watafiti, watoa maamuzi, watunga sera, wahudumu wa Afya na Jamii nzima kwa ujumla. Lengo kuu ni kuwezesha wadau wa tafiti waweze kujua tafiti zilizonyika na matokeo yake, katika kipindi husika. Hili ni jarida lenye hadhi ya kimataifa na linapatikana katika tovuti kubwa duniani zikiwamo PubMed, African Journal on Line na Bioline International.
Majarida mengine
Pamoja na kutumia Jarida la Tanzania, watafiti wetu huchapisha makala za utafiti katika majarida mengine mbalimblai ya kimataifa. Hadi kufikia Septemba 30, 2013 takribani makala za kitafiti 863 zimechapishwa katika majarida ya kimataifa ya sayansi yakiwemo Lancet, Science na New England Journal of Medicine. 3

Taarifa za Utafiti
Taarifa kamili za kitaaluma za utafiti huwasilishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya. Nakala za Taarifa hiyo husambazwa kwa Shirika la Afya Ulimwenguni na Mashirika Wahisani waliotoa mchango katika utekelezaji wa utafiti husika.
Taasisi pia huandaa Taarifa fupi kwa Watunga Sera (Policy brief) ambazo hufanya mchanganuo wa matokeo mbalimbali ya tafiti katika eneo husika kutoa mwongozo kwa watunga sera kufanya maamuzi sahihi yenye ushahidi katika maswala ya afya.
Siku Maalum za Utafiti kwa Umma
Kuanzia 2010, Taasisi imeanzisha utaratibu wa kufanya maonesho ya kazi zake kwa umma katika siku maalum (Open Days). Katika siku hizi ambazo huwa ni mwezi Oktoba kila mwaka, Taasisi kupitia vituo vyake huuandaa siku maalumu kwa hadhara ili kuwapa fursa Watanzania walio karibu na vituo vyake kutembelea na kujionea baadhi ya kazi zake za utafiti na huduma. Vituo hivyo ni Amani, Tanga, Muhimbili, Mbeya, Tukuyu, Mwanza na Tabora. Hatua hii huwapa fursa wananchi kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya. Pamoja na maonesho hayo, Vituo vyetu hutoa huduma mbalimbali za uchunguzi wa afya na tiba kwa wananchi wenye uhitaji.
Tovuti ya Taasisi
Tovuti ya taasisi (www.nimr.or.tz) inatumika kutoa habari/taarifa mbalimbali zinahusu majukumu na kazi za Taasisi. Taarifa zifuatazo zinapatikana katika tovuti ya Taasisi:
Vipaumbele vya taifa vya tafiti za afya
1. Orodha ya machapisho yote ya Taasisi
2. Miongozi ya Utafiti na Maadili ya Utafiti
3. Mihutasari ya tafiti katika lugha za Kishwahili na Kiingereza

MATUMIZI YA MATOKEO YA TAFITI
Uelewa wa ukubwa na mtawanyiko wa magonjwa
Matokeo ya tafiti za kiepidemiolojia yameliwezesha taifa (serikali na Jamii) kuwa na uelewa wa viwango vya maambukizi na mtawanyiko wa magonjwa mbalimbali nchini. Hii ikiwa na maana ya ugonjwa fulani uko wapi, unaadhiri watu wangapi, watu wa jinsi gani, wa umri gani, na walio katika mazingira gani. Takwimu hizi zinatumiwa na Wizara ya Afya na programu zake katika kupanga mikakati ya udhibiti wa magonjwa hayo na utoaji wa huduma za afya.
Ugunduzi
Taasisi imeshiriki katika ugunduzi wa vimelea na visababishi vya maradhi mbalimbali.
Malaria: Uwepo wa koo mbalimbali za mbu waenezao malaria wa Jamii ya Anopheles gambiae
Homa ya papasi: Uwepo wa aina mpya ya vimelea vinavyoambukiza homa ya papasi
Tiba asili: Dawa mbalimbali zinazotumika katika tiba asili 4

Mifumo ya Taarifa:
1. Mfumo wa kieletroniki wa Taarifa wa Ufuatiliaji wa matukio ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele
2. Mfumo wa Taarifa za Kijiografia – Taasisi imeandaa mfumo wa Kijiografia wa unaojumuisha taarifa za Vituo vyote vya kutoa huduma za Afya nchini. Mfumo huu hutumiwa na Serikali katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo

Mabadiliko ya Sera
 
 
1. UKIMWI na Magojwa ya Ngono
i. Matumizi ya elimu shirikishi kwa vijana katika kupunguza maambukizi ya UKIMWI
ii. Tohara ya wanaume katika kupunguza maambukizi ya UKIMWI,
iii. Tiba ya mangonjwa ya ngono kwa kutumia matokeo ya dalili za ugonjwa
iv. Matumizi ya njia mpya na ya muda mfupi katika kuanisha maambukizi ya kaswende kwa wakina mama
v. Matumizi ya chanjo dhidi ya kirusi kinachosababisha saratani ya shingo ya kizazi.

2. Malaria
i. matumizi ya vyandarua vilivyosindikwa viautilifu;
ii. mabadiliko ya sera ya tiba ya malaria kutoka matumizi ya Klorokwini, SP na dawa mseto ya ALu;
iii. matumizi ya takwimu kutabiri milipuko ya malaria
iv. Ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika kamati za ushauri za malaria

3. Kifua Kikuu
i. Tiba ya Kifua Kikuu kwa kutumia mfumo wa kumeza dawa mbele ya mtoa huduma
ii. Utaratibu wa mgonjwa wa Kifua Kikuu kuchagua mahali pa kupatiwa tiba (aidha apate tiba nyumbani kwake au katika kituo cha huduma za afya)

4. Magonjwa yasiyopewa kipaumbele
i. Mpango shirikishi wa jamii katika utuoaji wa tiba ya kutokomeza matende na usubi
ii. Kichocho – matumizi ya dawa ya tiba

5. Mifumo ya Utoaji Huduma za Afya

Taasisi imewezesha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa kutoka ngazi za vituo vya huduma, wilaya na taifa
6. Tathmini ya utekelezaji wa programu na mipango mikakati

Taasisi hufanya tathmini ya Utekelezaji wa mipango mikakati ya Serikali na Programu za huduma mbalimbali za Afya. Kwa siku za karibuni, Taasisi imekamilisha tathmini ya Awamu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya (2009-2015). 5

CHANGAMOTO
Lugha ya maswasiliano
Uwezo mdogo wa watafiti wengi kuwasilisha matokeo ya utafiti kwa lugha rahisi na rafiki.
Ufinyu wa bajeti
Katika miradi mingi ya utafiti, bajeti ya uwasilishaji wa matokeo hupewa uzito mdogo na hivyo haitoshelezi mahitaji – kutoa nakala nyingi za tarifa za utafiti, kulipia gharama za kuchapisha matokeo katika vyombo mbalimbali vya habari na kuwafikia wadau wote katika maeneo utafiti ulikofanywa.

Mbinu za kuwasilisha matokeo ya utafiti
Upo ukosefu wa njia mahsusi za kuwafikia watumiaji wa matokeo ya utafiti. Taarifa za utafiti huwasilishwa Serikalini kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Hata hivyo, Afya ni swala mtambuka, na baadhi ya tafiti zinatoa matokeo ambayo yanahusisha sekta nyingine. Kwa utaratibu wa sasa, ni vigumu matokeo haya yakawafikia watoa maamuzi walio katika sekta nje ya Afya.

Upokeaji wa matokeo chanya au hasi
Wadau wengi, ikiwa ni pamoja na watunga sera na watoa maamuzi, hawafurahishwi na matokeo ya tafiti yaliyo kinyume na matarajio yao (hasi).
Tafiti kuchukua muda mrefu
Tafiti bora duniani huchukua muda mrefu. Hivyo kuwafanya watunga sera au watoa maamuzi kukosa subira – hivyo kupendelea tafiti zile zinazochukua muda mfupi kukamilika.

MATARAJIO
1. Taasisi itaendelea na utaratibu wa kujenga uwezo wa Watafiti, Watunga Sera na Waandishi wa Habari katika uchanganuzi nawa matokeo ya utafiti na sera za afya. Tayari semina chache zimefanyika katika eneo hili. Kwa siku za karibuni, tumeandaa semina kuhusu tafiti mpya za UKIMWI. Semina hii iliwashirikisha Watafiti, Watunga Sera na Waandishi wa Habari.

2. Taasisi itaboresha uhusiano wake na Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili matokeo ya tafiti yaweze kufikishwa kwa walengwa wengi zaidi kwa kutumia mifumo mbalimbali ya mawasiliano

3. Ili kuboresha matumizi ya matokeo ya tafiti, Taasisi itaendelea kuwashirikisha Watunga Sera na Watoa Maamuzi katika tafiti tangu hatua za awali.

Kwa Mawasiliano:
Mkurugenzi Mkuu,
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu,
Simu: + 255 22 2121400
Baruapepe: hq@nimr.or.tz
©Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Oktoba 9, 2013

0 comments:

Post a Comment