KWANZA nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha leo kuwa nanyi katika safu hii ambayo huwa natoa mawazo yangu nikiamini kwamba yeye muumba ndiye anayeniongoza kuandika haya kwa manufaa ya umma wa Watanzania.
Nimekuwa nikitafakari kuhusu elimu inayotolewa katika shule mbalimbali hapa nchini, hasa shule za msingi na zile za sekondari. Baada ya kutafakari sana nikaamua kupekua hotuba au vitabu kadhaa vya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Nimegundua kuwa mawazo yake kuhusu msingi wa elimu ya kujitegemea ililenga zaidi vijana kujifunza kazi za uzalishaji mashuleni, kujitegemea kutokana na uzalishaji ule na shule kuweza kujiendesha.
Mbali na shule kujitegemea, mwanafunzi aliweza kujengwa kifikra na kisaikolojia kuhusiana na falsafa ya kujitegemea kwa faida yake na pia kuleta mabadiliko katika jamii kufuatana na ujuzi alioupata. Mwanafunzi alipata elimu ya darasani na elimu ya stadi za maisha kwa vitendo.
Kimsingi elimu ya kujitegemea ilitazama udhaifu na upungufu wa elimu ya kikoloni pia iliainisha aina ya jamii ya Kitanzania aliyokuwa anaijenga, kwa kujikita zaidi ukuaji wa uchumi vijijini.
Kwa mujibu wa Mwalimu, mfumo wa elimu ya kikoloni uliegemea zaidi katika jamii ya kibepari na uliwaandaa watu kutawaliwa na siyo kujitawala na ulijenga matabaka na kasumba ya kuuabudu utamaduni wa kigeni, kutokuwa na usawa, ubinafsi, urasimu na kutegemea kuajiriwa kuliko kujiajiri.
Elimu ililenga kuwapa watu mbinu na mikakati ya kuweza kuukabili umaskini pamoja na maisha ya kijijini kwa kutegemea kilimo.
Enzi ya Mwalimu elimu ya kujitegemea pamoja na uzalishaji viliendana na vilikuwa ni sehemu ya mtaala wake uliotoa maana chanya ya uzoefu wa kujifunza kujitegemea kwa nadharia na vitendo.
Elimu ya msingi ilikuwa ni lazima ijitosheleze na siyo njia kuu au nyenzo kuelekea elimu ya juu. Wanafunzi walitakiwa kujiamini, kushirikiana na kuanzisha changamoto mbalimbali kupitia nguvu ya hoja jadidi yenye kuleta mtazamo chanya kwenye maendeleo ya nchi yao.
Mwalimu pia alichangia ukuaji wa elimu ya juu kwa misingi ya kuwa chachu ya maendeleo na fikra. Wakati anakifungua Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka 1970 alisema, Namnukuu: ”Chuo kikuu ni taasisi ya elimu ya juu ambayo kwayo watu wanapata mafunzo ya kupanua wigo wa uelewa wao, fikra huru na sahihi, uchambuzi wa matatizo na kuyatatua kwa kiwango cha juu.”
Kwa nukuu hiyo ni wazi kwamba Nyerere aliona kwamba vyuo vikuu vya ndani vilikuwa muhimu kuanzishwa kwani vina jukumu kubwa la kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazoikabili nchi yetu kama vile ujinga, maradhi na kujikwamua na umaskini, vitu alivyovipa kipaumbele katika utawala wake.
Mwalimu alijenga mfumo wa elimu ya juu ambao unamwezesha Mtanzania kupata uwezo na ujuzi wa kutoa huduma kwa jamii, usawa katika kupata elimu ya juu bila kujali tabaka kama ilivyo sasa ambapo wenye fedha tu ndiyo watoto wao wanaipata elimu hiyo.
Kabla ya vijana kwenda vyuo vikuu walipitia katika operesheni maalum katika Jeshi la Kujenga Taifa ikiwa ni njia mojawapo ya kuwajenga kinidhamu, kizalendo kwa kuzingatia masilahi ya taifa.
Mwalimu alitoa elimu bure kwa watu wote na viongozi wengi wa kitaifa tunaowaona leo walipata elimu ya bure mpaka chuo kikuu enzi ya Mwalimu. Leo hii waliofaidi matunda ya elimu ya bure wamegeuka mabwanyenye wanaojaribu kuifanya elimu iwe chombo cha anasa na cha gharama kubwa ili iwe ya kwao na familia zao huku watoto wa walalahoi wakiumia na kuisotea kwa jasho jingi.
Hakuna siri kwamba viongozi wetu wamegeuza elimu kuwa biashara na kusababisha ubora wa elimu kushuka kwa kiasi kikubwa kwani mtoto badala ya kufaulu kwa akili yake, anafaulu kwa kuuziwa mitihani!
Ni wazi kwamba Watanzania tumerudi nyuma sana kielimu. Kingine ni serikali kutokuwa na mfumo imara wa kuwatunza wataalamu wetu waliosomeshwa kwa gharama kubwa na hivyo wengi wao kukimbilia katika nchi za nje kwa ajili ya masilahi zaidi. Hii siyo haki na huku ni kumsaliti Mwalimu.
Kama siyo juhudi za Mwalimu Nyerere, nina hakika leo hii tusingekuwa na mawaziri, wakurugenzi, makatibu wakuu au hata marais tulio nao leo ambao baba zao ni maskini.
Tusipoangalia tunapokwenda wenye vyeo katika taasisi za umma watakuwa ni watoto wa wenye uwezo tu kwa kuwa elimu ya juu wengi wao wanaipata. Hii ni hatari sana.
Ni wazi mikopo, rushwa ya ngono katika elimu na rushwa kwa ujumla, ukabila na matabaka ni vitu vinavyoshusha elimu siku hizi nchini. Hii bila kuficha ni aibu kwa watawala wetu.
Suala la bodi ya mikopo katika elimu bado ni changamoto kubwa kwa mtoto wa mlalahoi kwani inayotolewa haitoshelezi mahitaji, wakati mwingine kutokwenda kwa wakati na kumsababishia usumbufu mkubwa mwanafunzi awapo chuoni.
Nashauri kwamba serikali sasa iache kujiingiza katika mambo ya kifahari kama vile kuwanunulia watendaji wake magari ya gharama kubwa na iwekeze katika elimu.Waheshimiwa wabunge wanapaswa kuliangalia hili katika bajeti ijayo ya elimu vinginevyo itatufanya tulio wengi tumkumbuke Mwalimu kila tunapoona elimu inavyodidimia nchini!
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
CHANZO: HIKI HAPAGPL
0 comments:
Post a Comment