Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na
wanachama wa CCM na CUF mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa
Kigoma kuanza ziara ya siku mbili ya kichama Mkoani humo.
****
Tanzania
inahitaji mabadiliko kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa sambamba na
kutoa elimu na huduma bora kwa wakulima ili waweze kuendeleza kilimo
chenye tija.
Hayo
yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim
Lipumba alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho
uliofanyika Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.
Amesema
Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutba inayokubali kuotesha
mazao mbali mbali, lakini bado hakujakuwepo na mikakati imara ya
kuendeleza kilimo, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi kwa maslahi ya
wananchi.
Prof.
Lipumba amefahamisha kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa
inayoweza kufanya vizuri katika kilimo kutokana na kuwepo kwa maziwa na
mito ya kudumu ambayo inaweza kutumika kwa kilimo cha mboga mboga na
umwagiliaji, na kusaidia kukuza kipato cha wakulima.
Sambamba
na hilo Prof. Lipumba amewataka wakulima kutilia mkazo mazao ya nafaka
yakiwemo mahindi na maharage, kutoka na kuongezeka kwa bei ya mazao hayo katika soko la dunia.
Mwenyekiti
huyo wa CUF Taifa pia amesisitiza haja ya kuwepo kwa mikakati ya
makusudi ya kuongeza ajira kwa vijana ili kuwanusuru kujiingiza katika
vitendo viovu.
“Ukosefu
wa ajira unatisha, na ikiwa vijana hawana ajira wanaweza kushawishika
kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuliletea madhara Taifa”,
alifafanua Prof. Lipumba.
Akizungumzia
kuhusu mchakato wa katiba, Prof. Lipumba ametaka katiba mpya ijayo
itamke wazi kuwa maliasili za Tanzania na mali ya Watanzania na iweke
itaratibu ambao Watanzania wataweza kunufaika na rasilimali hizo.
Amesema iwapo wananchi watanufaika moja kwa moja na rasilimali
zao za nchi wataweza kuzilinda na kuziendeleza, lakini vyenginevyo
rasilimali hizo zinaweza kuleta maafa badala ya neema kama zilivyo
baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria na Equatorial Guinea.
Kwa
mujibu wa Prof. Lipumba Tanzania ina utajiri wa rasilimali mbali mbali
zikiwemo madini, mafuta na gesi asilia ambapo katika siku za hivi
karibuni Kampuni moja ya Norway iligundua gesi yenye futi za ujazo
trilioni 5 katika kisima kimoja pekee, ambapo jumla inakisiwa kuwepo na
gesi trilioni 30 futi za ujazo.
Amesema rasilimaji zipo nyingi lakini zinahitaji kuwepo na uongozi wenye dira utakaozingatia mgawanyo wa rasilimali hizo kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema
CUF kitasimamia sera yake ya haki na usawa, ili kuhakikisha kuwa kila
Mtanzania anapata haki zake za msingi zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na
huduma za jamii.
Amesema
tatizo kubwa la Tanzania ni mipango duni ya kiuchumi, na kuwashauri
wananchi kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kurekebisha kasoro
zilizopo na kuimarisha uchumi wa nchi.
Kabla
ya mkutano huo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, aliupongeza uongozi wa Mkoa huo kutokana na ushirikiano mzuri
wanaoutoa kwa vyama vya siasa, na kwamba kufanya hivyo ni kuonesha
ukomavu wa kisiasa.
Katika
uwanja wa ndege wa Kigoma Maalim Seif alipokelewa na viongozi wa mkoa
huo pamoja na wafuasi wa CUF na Chama Cha Mapinduzi.
Mkutano
huo ni sehemu ya Operesheni mchakamchaka hadi 2015 iliyozinduliwa na
chama hicho kwa ajili ya kutembelea mikoa mbali mbali ya Tanzania kutoa
uelewa kwa wananchi ili hatimaye waweze kujiunga na chama hicho.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
0 comments:
Post a Comment