SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, April 17, 2012

Anachokisema Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Julius Mtatiro Juu Ya Katiba Mpya

JULIUS MTATIRO katibu mkuu wa chama CUF Tanazania bara.
****
Pamoja na matumaini makubwa ambayo mkuu wa nchi kupitia CCM alionesha tangu mwanzo kwa kupingana na makada wenzie katika namna nyingi sana, sasa naona ameanza kupotoka na anataka kukitia mchanga kitumbua chake yeye mwenyewe.
Kauli ya kiongozi wa nchi siku chache zilizopita katika sherehe ya kuwaapisha wajumbe wa tume ya katiba iliyonukuliwa akisema "masuala ya kuvunja muungano yasijadiliwe" ni kauli ya kichokozi mno. Kwa taarifa ya bwana mkubwa, katiba inayoenda kutengenezwa ni ya watanzania, siyo yake. Watanzania ndiyo wanahitaji katiba yao, hawahitaji masharti kupata katiba hiyo.
Bwana mkubwa ajue kuwa Tanzania inatokana na muungano wa wazi wa nchi mbili zenye historia na utamaduni tofauti na zilizopata uhuru katika nyakati tofauti. Nchi ya kwanza ni Tanganyika (Iliyofunikwa na jina tanzania hivi sasa) na nchi ya pili ni Zanzibar ambayo bado ina-exist. Mkuu wa nchi atambue kuwa katika katiba mpya lazima tujadili u-tanganyika wetu na u-zanzibari ndani ya muungano na tuondoe tofauti zinazopelekea mizizi ya wao wazanzibari na sisi watanganyika kufufuka kwa nguvu kubwa. Lengo la mjadala lisiwe ni kuvunja muungano, liwe ni kuboresha na kufanyia kazi manung'uniko ya watanganyika na wazanzibari ili wapate muungano thabiti.
Na njia moja ambayo watanganyika na wazanzibari wataihitaji ni mfumo wa serikali tatu. Mfumo huu kuna watu wanaupinga bila sababu na dhana ya mkuu wa nchi kusema muungano usiguswe ni hofu yake kuwa wanachi wakiugusa muungano watataka serikali tatu. Mzee wetu Kikwete muhimu sana umalize muda wako salama salimini ukapumzike. Leo mchele umefikia shilingi 3000 kwa kilo moja, wakati unaingia madarakani mchele ulikuwa shilingi 400 na 500 kwa kweli uchumi wa nchi umekufa kabisa. Kwa sababu hatuwezi kukutoa madarakani kwa nguvu tunasubiri wewe na chama chako muondoke 2015.
Sasa kabla hamjaondoka kwa amani, nakupa ushauri wa bure kabisa, tumia karata ya katiba mpya tupate katiba ya wananchi itakayotatua kila kero yao, katiba bora ambayo itakuwa tunu kwa watanzania ndiyo jambo pekee ambalo watanzania wanaweza kukukumbuka kuwa ulifanya, kwingine umeshindwa na ukitia kitumbua cha katiba mchanga utamaliza urais wako wa miaka 10 bila kujulikana ulisimamia nini. "JACK OF ALL TRADES......MASTER OF....."). Waache watanzania waamue hatma yao, nakusihi usiingilie! Kama watu watataka kuongozwa na wafalme au watemi n.k. waache waamue na waongozwe wanavyotaka.
CUF tunataka serikali tatu, na bila shaka wananchi wengi wanataka serikali tatu kama suluhisho la matatizo ya muungano. Serikali tatu zitatusaidia kuwa na mfumo unaoeleweka ndani ya nchi, zitatusaidia kutenganisha mambo ya zanzibar, mambo ya tanganyika na mambo ya muungano. Yatatufanya tuwe na utaratibu unaoelewaka juu ya serikali ya muungano hasa kujua nani anaiongoza muda gani na anatoka wapi.
Kwa hali ilivyo kama hatupati serikali tatu, muungano utavunjika soon kwa sababu ndani ya muungano wa sasa ni vigumu tena kwa mwananchi kutoka zanzibar kuwa rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania.
Hii ni kwa sababu wapiga kura zaidi ya milioni 18 wanatoka tanganyika na ikiwa chama A kimesimamisha mtanganyika na chama B kimesimamisha mzanzibari. Propaganda zikizungushwa kwa watanganyika kuwa tuchague mtanganyika mwenzetu atatue matatizo ya tanganyika yetu kwa sababu zanzibar wana serikali yao ni rahisi watu kuamini propaganda hiyo na wataipokea kwa mikono miwili.
Hali ikiendela hivyo na kwa sababu ndivyo ilivyo wazanzibari watahoji kwa nini wao hawana fursa ya kuwa na rais wa muungano kwa mfumo ulipo hivi sasa. Kwa sababu hatutakuwa na majawabu wakati huo, wazanzibari watajitoa kwenye muungano. Na hilo likifanyika, wewe rais kikwete ndiyo utakuwa chanzo cha kuvunja muungano.
Kama pana dhamira ya dhati ya kutengeneza muungano bora lazima tuujadili, lazima tuweke serikali tatu, lazima sote kama watanzania tukae chini na kukubaliana na kukubali hali halisi kuwa kinachoungana ni nchi huru, nchi mbili tofauti.
Tuondoe dhana zisizo na maana kuwa kinachoungana ni watu 18 milioni na wanaungana na watu 1.5 milioni. Tusijechukulia ati kinachoungana ni li-nchi limoja kubwa na ka-nchi kengine kadogo, tusijejidanganya ati vinavyoungana ni nchi ya Tanganyika na jimbo la Zanzibar.
Sote katika mioyo yetu lazima tukubaliane kuwa vinavyoungana ni nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar (each of them as a sovereign state), sasa tukilifahamu hilo na kulikubali tutatengeneza muungano wenye usawa wa ki-nchi.
La hatuwezi kutengeneza muungano huru na wa usawa, basi bora tuiweke ajenda hii kando na tuuvunjilie mbali(Na ikumbukwe muungano ni rahisi kuvunjika kwa sababu siyo chakula, kwa sababu siyo maisha yetu, hatuishi kwa sababu ya muungano… hata kidogo…na siyo kweli kwamba muungano chini ya uongozi wa ccm umetuletea maendeleo… la hasha!)
Kwa hiyo, kitisho cha mkuu wan chi ati muungano usijadiliwe naona kama ndiyo filimbi ya kuwajulisha wananchi waukatae muungano lakini wananchi wakiachwa wachague aina ya muungano wanaoutaka kwa uhuru ndiyo itakuwa ponapona yake.
Kupanga ni kuchagua, lazima tupange sasa na tuchague sasa. Tuwe na muungano usiowaibiwa watanganyika na wala usiowaibiwa wazanzibari, tuchague jambo moja, tukome hii tabia ya kuwa kila siku hatuelewi tunasimamia wapi, hatujui dira ya taifa, hatujui falsafa inayoongoza taifa, hatujui chochote.
Tutafakari kwa umakini mkubwa.

0 comments:

Post a Comment