Ni Jumatatu asubuhi. Hali ya hewa ya joto la kadiri ilikuwa ni kitu cha kawaida kwa maeneo haya ya Dar es Salaam kipindi cha miezi hii ya mwisho wa mwaka. Tupo darasani kwenye presentation ya somo linalohusu magonjwa ya figo. Mada ilihusu kushindwa kufanya kazi ghafla kwa figo au Acute Renal Failure kwa lugha ya wenzetu. Lilikuwa somo refu lililozungumzia kwa undani tatizo hilo. Baada ya mwenzetu mwasilishaji kumaliza kuwasilisha somo lake kikafuata kipindi cha maswali na majibu na masomo zaidi kutoka kwa Profesa aliyekuwa anasimamia ile mada.
Mada ilikuwa moto. Maswali yetu pamoja na uzoefu wa yule profesa ulitosha kuibua somo na majibu yaliyotosheleza kiu zetu za kujifunza zaidi. Kisha baada ya somo akauliza swali kwa hali ya utani kidogo, nani kati yenu anapenda kuwa Nephrologist (daktari bingwa wa magonjwa ya figo). Wote tulibaki kimya tukitazamana kisha mwanafunzi muwasilisha mada huku akitabasamu alininyoshea kidole akasema Fabby huyo. Profesa aliniangalia kisha akainamisha kichwa chini kwa masikitiko akasema “I feel sorry for you my friend (nakuonea huruma rafiki yangu)”. Sikuelewa kwanini alisema vile nikashtukia tu namuuliza “why Professor?” Huku bado akiendelea kunitazama akanijibu “because you will be seeing your patients dying everyday”. Jibu lake ghafla likanirudisha nyuma kama mwaka mmoja hivi nikiwa nafanya kazi hospitali moja ya Mission iliyopo mkoa fulani kusini mwa nchi.
Ilikuwa siku ya Jumatano asubuhi. Hali ya kaubaridi baridi iliyokuwepo siku hiyo iliashiria kuanza kwa siku njema. Ninaingia wodini na kusalimiana na wauguzi wa wodi yangu kabla ya kuingia ofisini kujiandaa na round. Nilikuwa na kawaida ya kuanza siku kwa kufanya round kwa wagonjwa waliolazwa kabla ya kuingia ofisini kuwaona wagonjwa wengine wapya na wale wanaokuja kwa ajili ya follow up.
Baada ya kuwaona wagonjwa kadhaa, nikakifikia kitanda cha mgonjwa mpya aliyekuwa amelazwa usiku wa kuamkia siku hiyo na kuonwa na Clinical officer aliyekuwa zamu. Ni binti wa miaka takribani 20 (kwa sababu za kimaadili sitataja jina, umri wake halisi, mahali anapoishi wala details zake nyingine).
Hali yake ilikuwa mbaya maana alikuwa amenyong’onyea na alikuwa akipumua kwa shida sana. Mpira wa mkojo ulikuwa ukining’inia pembeni ya kitanda lakini hakukuwa na kitu ndani yake. Uso wake ulionekana kuvimba kwa mbali na alikuwa akizungumza kwa shida. Midomo ilikuwa mikavu na hata ngozi yake ilionekana iliyosinyaa na kavu kuliko kawaida. Nilimuita mwangalizi wake na kuanza kuchukua upya historia ya mgonjwa maana yeye mwenyewe alikuwa akizungumza kwa shida sana.
Mwangalizi aliniambia kuwa mgonjwa wake, alianza kupata tatizo la kukosa mkojo kwa ghafla kama siku saba zilizopita. Hawakujua sababu hivyo wakadhani ni mambo ya ushirikina wakaamua kumpeleka kwa mganga wa kienyeji ambaye alikaa naye siku tatu huku akimnywesha kila aina ya miti shamba lakini bila mafanikio.
Akasema, “tulipoona hali yake bado ipo vile vile tukaamua kumkimbiza hapa ili tujaribu huduma za kizungu. Kwahiyo kwa ujumla ana siku kama kumi tangu tatizo lilipojitokeza. Wakati tupo kwa mganga angalau hali yake ilikuwa siyo mbaya sana lakini jana usiku ndiyo hali ikabadilika tukaamua kumkimbiza huku. Sasa hivi hali chochote maana analalamika kichefuchefu muda wote, na akijaribu kula tu anatapika chote. Wakati mwingine anaongea vitu havieleweki basi baba ndiyo hivyo hivyo tu”.
Baada ya kuuliza maswali zaidi kulingana na taratibu zetu, kwa muonekano wa mgonjwa na historia yake harakaharaka niliweza kuhisi ni kitu gani kitakuwa kinamsumbua huyu mgonjwa. Niliamua kumfanyia uchunguzi wa mwili (physical examination) ili kuona vishiria vingine vya ugonjwa. Alikuwa na dalili zote za mtu mwenye matatizo ya figo, na mbaya zaidi alikuwa katika hali ya hatari zaidi ya ugonjwa.
Uchunguzi ulionesha, pamoja na dalili nyingine, kuwa alikuwa amevimba miguu (pedal edema) kwa kiasi fulani, tumbo lake lilishaanza kuvimba (ascites) na alikuwa akipumua kwa shida sana (dysponea), alikuwa na dalili za upungufu wa damu (anemia) na ngozi kavu kuliko kawaida kuonesha kuwa alikuwa amepungukiwa maji mwilini (dehydrated).
Nikaagiza tufanye vipimo kadhaa kama vile vya kuchunguza utendaji kazi figo, vya kuchunguza uwiano wa madini/chumvi mwilini (electrolytes analysis), ultrasound ya tumbo, vipimo vya moyo na vipimo vingine kadiri nilivyoona inafaa.
Ingawa vingi ya vipimo nilivyoagiza vilishindikana kufanyika ama kwa vile hakukuwa na vifaa vya kufanyia vipimo hivyo au hatukuwa na wataalamu wa maabara wenye ujuzi wa kufanya vipimo hivyo pamoja na kuwepo kwa mashine, bado niliweza kupata jawabu la tatizo lililokuwa linamsumbua mgonjwa wangu ingawa nakiri sikuweza kufahamu chanzo hasa cha ugonjwa wake ni nini kwa vile hatukuwa na vipimo vya kufanya hivyo. Alikuwa akisumbuliwa na kushindwa kufanya kazi ghafla kwa figo yaani Acute Renal Failure (ARF) na kwa dalili zake tayari alishafikia hatua ya kuwa na kiasi kikubwa cha madini ya potassium katika damu (hyperkalemia) na kwamba mrundikano wa uchafu mwilini ulikuwa katika kiwango cha hali ya juu kwa sababu figo zilishaacha kufanya kazi zake inavyotakiwa.
Pamoja na kumuanzishia matibabu, katika hali aliyokuwa nayo matibabu sahihi ilikuwa kwanza kufahamu chanzo cha tatizo ili kukitibu, kumfanyia dialysis ili kutoa uchafu mwilini na hatimaye kama ikionekana figo zimekufa kabisa basi afanyiwe upandikizaji wa figo mpya.
Nilipowaeleza yeye na mwangalizi wake kuhusu matokeo ya vipimo, hatua ya ugonjwa iliyofikiwa na nini cha kufanya ghafla niliona machozi yanamlengalenga mwangalizi. Kwa kweli alistahili kuwa vile. Kwa unyonge akaniuliza, “sasa baba hayo matibabu mnaweza kuyafanya hapa.” Nilimtazama tena na kwa kujitutumua ilibidi nimueleze tu ukweli kuwa hatuna uwezo wa kufanya dialysis pale kwetu, na wala hospitali ya karibu ya mkoa haina uwezo wa kufanya hivyo mjipigepige mumsafirishe mgonjwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Kama aliyekuwa anasubiri bomu zaidi nikamtajia na gharama za kufanya hayo matibabu na muda anaotakiwa kufanyiwa. Mama mwangalizi alinyamaza kwa sekunde kadhaa kama mtu anayefikiria kitu kisha kwa unyonge akasema , “baba kwa umaskini wetu huu hali yenyewe hii unaiona nilivyo.
Naomba chonde chonde ujitahidi kufanya lolote lile hapa kama Mungu akipenda kumchukua basi mapenzi yake yafanyike maana hatuna uwezo wa kumsafirisha siyo tu kwenda huko Dar es Salaam bali hata hapo mkoani hatuwezi kufika”. Sikuwa na jinsi zaidi ya kuendelea na matibabu na kufanya kwa kadiri ya uwezo wangu kuokoa maisha ya mgonjwa wangu.
Nasikitika kuwa baada ya masaa kadhaa mgonjwa yule alifariki kwa mshtuko wa moyo kama complication ya hypekalemia. Nilihuzunika sana lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kuendelea kuchapa kazi kuhudumia wagonjwa wengine.
Kwanini nimekikumbuka hiki kisa?
Hiki ni kisa kimoja tu kati ya visa vingi vingi ambavyo madaktari wanakutana navyo kila siku katika utendaji wao wa kazi. Kushuhudia uhai ukipotea wakati ungeweza kuokoa maisha lakini huna vifaa au wataalamu wa kusaidiana nawe ni jambo linaloumiza sana kwa daktari na watoa huduma ya afya kwa ujumla wake.
Nawafahamu wenzangu waliowahi kufanya operesheni kwa kutumia mwanga wa tochi za simu baada ya umeme kukatika hospitalini kukiwa hakuna jenereta wala taa hata ya kandili, wapo waliolazimika kubuni mbinu mbadala baada ya kukosekana maji ya drip (iv fluids) kwa ajili ya matibabu.
Hapa majuzi tumesikia kuhusu watumishi wa hospitali moja ya misheni huko mkoani Manyara wanaolazimika kutumia vipande vya nguo na mashuka kama gloves wakati wa kuhudumia wagonjwa, ipo mifano mingi mingi inayoonesha uzembe wa watendaji wanaotakiwa kuboresha mazingira ya kazi ili watoa huduma ya afya waweze kutoa huduma katika mazingira salama kwao wenyewe na kwa wagonjwa wao na hivyo kuokoa maisha yao.
Kifo cha mgonjwa yule kingeweza kuzuilika au hata kucheleweshwa kwa mfano kama hospitali ya mkoa ingewezeshwa kutoa huduma ya dialysis kiasi cha kuweza kumkimbiza mgonjwa hospitalini hapo haraka. Lakini pia ingewezekana kuwa katika wakati mzuri wa kutambua chanzo cha ugonjwa wake kama hospitali ile ingekuwa na vifaa vya uhakika vya vipimo na pengine kulipatia ufumbuzi bila hata kuhitaji kumpa referral. Ipo mifano mingi yenye kufanana na hiyo.
Mgogoro unaondelea hivi sasa nchini kati ya madaktari kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine ni jambo linalosikitisha kutokana na jinsi suala hili lilivyoshughulikiwa na watendaji wakuu wa wizara pamoja na kuwa madai ya madaktari hawa ni ya msingi sana. Moja ya madai ya madaktari ni kutaka uboreshaji wa hospitali na vituo vyetu vya afya kwa maana ya vitendea kazi na mazingira ya kufanyia kazi. Dai hili siyo tu lina nia njema ya kuwahakikishia madaktari wanafanya kazi katika mazingira bora yenye vitendea kazi vya uhakika bali pia linahusu afya njema kwa ajili ya wananchi wenyewe. Kwa maneno mengine madai ya madaktari yanahusu pia ustawi wa afya za wananchi wengine na siyo maslahi yao tu binafsi.
Ni aibu sana kwa hospitali ya Taifa, kwa mfano, kukatikiwa umeme bila kuwa na chanzo kingine mbadala cha umeme huku ukitegemea watoa huduma hawa kuacha kunung’unika. Haiingii akilini hospitali ya Wilaya kukosa hata strips za kupimia sukari mwilini na kisha ukategemea wafanyakazi wawe na furaha na kazi yao. Haingii akilini wauguzi wafurahie kufanya kazi kwenye wodi ambayo wagonjwa wamelala watatu watatu kwenye kitanda kimoja. Ni aibu, ni aibu, ni aibu.
Pamoja na nia njema ya madai hayo, bado inasikitisha kuona jinsi ambavyo serikali kupitia kwa Waziri Mkuu walivyoona kuwa hakuna njia ya kuweza kushughulika na madai hayo zaidi ya KUAMURU madaktari kurudi kazini kana kwamba AMRI inaweza kuboresha mazingira ya kazi. Kumlazimisha tabibu pamoja na watoa huduma wengine wa afya kurudi katika mazingira yale yale wanayoyapigia kelele siyo tu hakutatui tatizo bali kunaongeza ukubwa wa tatizo.
Hakuna tabibu na muuguzi atakayefanya kazi kwa moyo mmoja huku akiwa na hasira na kinyongo kwanza kwa kuamrishwa bila kusikilizwa anachodai lakini pili kwa kulazimishwa kurudi katika mazingira yaleyale anayodai yarekebishwe. Hatari ninayoina ni kwa wagonjwa kuzidi kupoteza maisha na wengine kuishia kupata vilema kutokana na matibabu butu watakayopewa na wahudumu wasioridhika. Na haya yakitokea wahudumu wa afya kamwe wasilaumiwe!
Amri, vitisho, ubabe wala kamata kamata ya madaktari siyo suluhisho la matatizo. Ni matumaini yangu, wale wenye mamlaka wataona uzito wa madai ya madaktari na kuyapatia ufumbuzi wa kweli badala ya kuyapatia majibu ya kisiasa yenye vitisho na nia ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
Kinyume na hapo ni kuahirisha matatizo na kuendelea kuhatarisha afya za wananchi wengi masikini na wengine kufa kama yule binti. Lakini pia ni matumaini yetu, wananchi watatambua nia njema ya madaktari ya kutaka kuboreshewa mazingira yao ya kazi ili wananchi nao waweze kupatiwa huduma bora zaidi na uhakika tofauti na sasa.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA FABIAN P. MGHANGA
0 comments:
Post a Comment