SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Saturday, April 30, 2011

WHO Watua Samunge

Wanasayansi wa ndani wathibitisha uwezo wake.
Mussa Juma, Samunge
Wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na taasisi mbalimbali za afya nchini, jana walifika Samunge kuanza mchakato wa kutafiti dawa inayotolewa na Mchungaji, Ambilikile Mwasapila kama inatibu magonjwa sugu au la.Wataalamu hao walifika Samunge majira ya saa sita mchana na kusababisha kusitishwa kwa muda utoaji wa tiba ili kuwapa nafasi ya kufanya mahojiano na Mchungaji Mwasapila, kuchukua sampuli za dawa na mti ya mugariga. Baada ya mahiojiano, nao pia walipata kikombe cha tiba.
Wataalamu hao ni pamoja na Profesa Charles Wambebe wa WHO Marekani, Dk Budeba Sylvester wa Wizara ya Afya na Dk Georges Shemdowe kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia.Ujumbe wa huo pia ulimjumuisha, Mkemia kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Hamis Malebo.
Profesa Wambebe ambaye ni raia wa Nigeria na mtaalamu bingwa mwenye uzoefu na masuala ya tiba za asili, alisema amefika Samunge kutokana na maombi ya Serikali ya Tanzania iliyoomba msaada wa WHO, kufanya uchunguzi wa dawa ya Mchungaji Mwasapila.
''Tumekuja hapa Samunge, kufuatilia tiba hii jinsi inavyotolewa na WHO kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania itaendesha utafiti kwa kuhusisha watu waliotumia dawa, Mchungaji Mwasapila na wadau wengine ili kuona inaponyesha kiasi gani," alisema Profesa Wambebe.
Alisema wanatarajia kuwa ndani ya miezi 12 watakuwa wametoa majibu juu ya ubora wa dawa hiyo na katika kipindi cha miezi mitatu ijayo watatoa maendeleo ya utafiti ambao utakuwa unafanywa.
Alisema baada ya kukamilisha utafiti, Serikali ya Tanzania ndiyo itakayoachiwa jukumu la kutangaza dawa hiyo kama inatibu kiasi gani na kama itahitaji kuboreshwa ili iwe katika mazingira ya kisasa ni nini kifanyike.
Wagonjwa wa kisukari kuanza
Dk Sylvester alisema uchunguzi huo utaanzia kwa wagonjwa wa kisukari hasa kutokana na vipimo vyao kuwa rahisi na kufuatilia hali zao pia itakuwa ni rahisi tofauti na magonjwa mengine.
Alisema wizara ya afya inakusudia kupeleka Samunge, maabara kubwa ya kisasa ambayo wagonjwa watapimwa kabla ya kunywa dawa na baada ya kunywa watafuatiliwa kitaalamu hadi hapo itakapothibitika ubora wa dawa.
"Tunaomba wananchi wasubiri watafiti kufanya kazi kwani tayari taarifa ilitolewa kuwa dawa hii haina madhara kwa binadamu na kazi inayofuatia sasa ni kutazama ubora wake katika kutibu maradhi mbalimbali," alisema.
Babu atoa shukrani
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila jana alitoa shukrani kwa serikali kuanzia ngazi ya Kijiji hadi wilaya kutokana ushirikiano waliompa katika msiba wa mtoto wake, Jackson (43) ambaye alifariki wilayani Babati baada ya kuugua malaria.
"Napenda kushukuru Serikali Wilaya ya Ngorongoro na Babati kwa msaada mkubwa ambao wamenipa katika msiba na kuniwezesha kufika kwa wakati na kurejea hapa, pia nawashukuru wananchi wote kwa ushirikiano walionipa," alisema Mwasapila.
Habari zaidi: Bofya Hapa

0 comments:

Post a Comment