MGAWO WA UMEME WASITISHWA
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Angalau Watanzania wanaotumia nishati ya umeme watakuwa na ahueni sasa baada
ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutangaza kusitisha mgawo wa umeme uliodumu kwa zaidi ya wiki mbili.
Mkoa wa Dar es Salaam ulianza na mgawo huo kabla ya kuikumba mikoa mingine yote inayopata umeme kutoka Gridi ya Taifa, hali ambayo iliyafanya maisha ya Watanzania wengi kuwa katika hali mbaya.
Lakini jana Tanesco imetangaza kusitisha mgawo huo wa umeme ikieleza hali hiyo imetokana na mvua kuanza kunyesha na maji kuongezeka kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Mtera na Kihansi katika mikoa ya Morogoro na Iringa.
Umeme wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unazalishwa kwa kutegemea maji. Lakini pia Tanesco imesema inasitisha mgawo huo baada ya mashine moja kati ya nne zilizoharibika za Songas kupona.
Akizungumza na waandishi wa habari walioko katika ziara ya kuzungukia mitambo ya Kihansi na Mtera, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alisema kwa sasa hali ya uzalishaji umeme inatia matumaini.
Badra alisema tatizo la mgawo wa umeme pamoja na kuharibika kwa mashine nne, lilisababisha kiwango cha maji katika mabwawa hayo kupungua kutokana na ukame.
“Hali ya uzalishaji umeme kwa sasa inaendelea vizuri, mvua kubwa zimenyesha na
mabwawa yetu ya Kihansi, Mtera na Kidatu yameingia maji ingawa si mengi, lakini yanatosheleza kusitisha mgawo uliodumu kwa takribani wiki mbili sasa,” alifafanua Badra.
Hata hivyo, alisema pamoja na Tanesco kusitisha mgawo huo, hali inaweza kubadilika
wakati wowote na mgawo kurudi kama mabwawa hayo yasipoingiza maji ya kutosha.
Naye Kaimu Meneja wa Mtambo wa Kihansi, Patrick Lwesya, alisema awali maji katika bwawa la Kihansi, maji yalipungua na kufikia matumizi yake yashuke hadi lita za ujazo 8.8 kwa sekunde katika uzalishaji umeme.
“Kwa kawaida mtambo wa Kihansi huzalisha umeme kwa kutumia lita za ujazo 16.2 kutokana na mvua za leo (jana) zimeongezeka na kufikia lita za ujazo 10.27,” alisema Lwesya.
Alisema hali ya uzalishaji katika mtambo huo unaochangia asilimia 25 katika Gridi ya Umeme ya Taifa mara nyingi hutegemea kiwango cha maji kinachokuwepo.
Alisema kwa sasa mtambo wa Kihansi uko kwenye mchakato wa kuzalisha megawati 120 nyingine na hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 300 pindi awamu ya pili ya ujenzi wa mtambo huo itakapokamilika.
Alisema ujenzi huo wa awamu ya pili utahusishwa na uwekaji wa transfoma mbili ambapo moja tayari imeshawekwa ili kuongeza nguvu ya umeme huo.
Mgawo wa umeme ulianza wiki mbili zilizopita baada ya kupungua kwa maji katika mabwawa ya New Pangani na Kihansi sambamba na kuharibika mashine nne ikiwamo ya Songas inayozalisha megawati 35.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema kupatikana kwa umeme wa uhakika kunategemea kukamilishwa kwa matengenezo ya mitambo iliyoharibika.
Ngeleja alisema hayo Dar es Salaam jana baada ya kutembelea mitambo ya kuzalisha umeme kwa lengo la kujua hali yake na jinsi ambavyo inaweza kupunguza mgawo wa umeme nchini.
Mitambo aliyotembelea ni pamoja na Songas, Kituo cha kuzalisha umeme cha Tanesco Ubungo, IPTL na Tegeta.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Ngeleja alisema mgawo wa umeme ulioanza takriban wiki mbili zilizopita, ulisababishwa na uharibifu wa mitambo kadhaa nchini ikiwemo ule wa Songas wa kuzalisha megawati 35, Kipawa wa megawati 32, mtambo mmoja wa Ubungo na upungufu wa maji.
Kuhusu mtambo wa Songas, alisema mtambo namba tatu ulioharibika tayari wamefunga mwingine ambao umeanza kuzalisha umeme, ila kuna mtambo mwingine wenye uwezo wa
kuzalisha megawati 35 ambao upo katika matengenezo ya kawaida.
“Mtambo unatakiwa kufanyiwa matengenezo ya kawaida kwa kuwa ulifanya kazi kwa muda mrefu na kwa mujibu wa vifaa hivyo usipofanyiwa matengenezo hayo unaweza kulipuka,” alisema Ngeleja.
Hata hivyo, aliwataka watendaji wa Songas kufanya kazi kwa saa 24 wakishirikiana na wataalamu kutoka Kampuni ya Marekani ya General Electric ili kukamilisha kazi hiyo kesho ambapo watendaji hao walikiri kukamilisha kazi hiyo kwa muda huo.
Kwa upande wa IPTL, alisema hadi jana walikuwa wakiingiza umeme megawati 70, hivyo kuchangia kusitishwa kwa mgawo wa umeme.
“Tatizo kubwa kwa IPTL ni kukosa mafuta ya kutosha kwa wakati unaotakiwa wa kuendesha mitambo hiyo, ambapo kwa siku malori 17 humwaga mafuta huku upakuaji wa lori moja kuchukua saa mbili,” alisema.
Kuhusu ongezeko la maji alisema kwa mabwawa ya Kidatu na Mtera kutokana na mvua
iliyonyesha juzi iliongeza kiwango cha mita 1.3 ya maji.
0 comments:
Post a Comment