Makao makuu ya soka Ghana yazingirwa
Mustakabali wa soka ya Ghana unakabiliwa na giza baada ya
maafisa wa kitengo cha kupambana na rushwa, kuzingira makao makuu ya
chama cha soka cha nchi hiyo (GFA) siku ya Jumanne.
Maafisa wa Kitengo cha kupambana na rushwa wa Ghana, wamewazuia
maafisa wa chama hicho kuingia au kutoka katika ofisi za chama hicho
mjini Accra, wakiwa wanatafuta nyaraka ambazo hazijafahamika.
Maafisa hao wamesema, wamepata kibali cha
upekuzi kutoka mahakamani, wamechukua kompyuta na simu za mikononi
kutoka ndani ya jengo hilo.
Kwa kawaida shirikisho la soka duniani- Fifa
linakuwa na msimamo mkali kutokana na serikali kuingilia mambo ya
uendeshaji wa vyama vya soka vya nchi.
Mashabiki wa soka wa Ghana
Kutokana na hulka hiyo ya serikali, nchi nyingi zimekwishafungiwa na Fifa kujihusisha na masuala ya soka siku zilizopita.
Rais wa GFA, Kwesi Nyantakyi, hakuwepo ndani ya
jengo la makao makuu ya ofisi za chama cha soka, lakini alitarajiwa
kuwasili wakati wowote.
Hatua hiyo imekuja wiki moja baada ya Fifa
kuionya serikali ya Ghana juu ya uwezekano wa kuwekewa vikwazo iwapo
itaingilia uendeshaji wa soka ya nchi hiyo.
Ikiwa imechunguza madai ya kuingilia shughuli za
soka, Fifa iligundua soka ya Ghana inachagizwa na serikali kuhusiana na
masuala yaliyojitokeza hivi punde.
Mfano mmoja ilikuwa ni jaribio la serikali ya
Ghana, kutaka kumuweka madarakani Abedi Pele kuwa mgombea kwa nafasi
iliyowazi ya mjumbe katika Shirikisho la soka barani Afrika licha ya GFA
kupinga wazo hilo.
0 comments:
Post a Comment