Radiamali ya Waislamu dhidi ya uamuzi wa mahakama ya India kuhusu msikiti wa Babri
Mahakama Kuu ya Allahabad ya India hatimaye umetoa hukumu kuhusu faili la msikiti ulioharibiwa na Wahindu wenye misimamo mikali wa Babri baada ya kupita yapata miongo miwili. Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama hiyo, ardhi ya msikiti ulioharibiwa wa Babri itagawanywa kati ya Waislamu, Wahindu na kundi jingine dogo la kidini la Wahindu. Kwa maana nyingine ni kuwa Wahindu wamepewa thuluthi mbili ya ardhi ya msikiti huo mkongwe huku Waislamu wakibakishiwa moja ya tatu ya ardhi hiyo.
Wakili wa Waislamu wa India katika kesi hiyo Zafaryab Jilani amesema kuwa atakata rufaa kupinga hukumu hiyo. Amesema japokuwa Mahakama Kuu ya Allahabad imekiri kwamba Waislamu wanamiliki thuluthi moja ya ardhi ya msikiti huo lakini kwa ujumla uamuzi wake umekatisha tamaa. Wanasheria wengi wa India pia wanasema kuwa Mahakama ya Allahabad imewapa Wahindu ardhi ya msikiti wa Babri. Msikiti huo ulioko katika mji wa Ayodhya ulivamiwa na kubomolewa na Wahindu wenye misimamo mikali mwaka 1992. Wafuasi wa dini ya Kihindu pia wamefurahishwa mno na uamuzi wa mahakama hiyo ambayo imekubali madai kwamba mungu wao Ram, alizaliwa katika ardhi ya msikiti wa Babri. Sasa Wahindu hao wenye misimamo mikali wameazimia kujenga hekalu katika ardhi ya msikiti wa Babri, suala ambalo linapingwa na Waislamu wa India.
Msikiti wa Babri ulijengwa katika karne ya 16 na ulihesabiwa kuwa miongoni mwa maeneo matakatifu na ya kihistoria ya Waislamu wa India. Mwaka 1992 msikiti huo uliokuwa mkubwa zaidi katika jimbo la Uttar Pradesh ulivamiwa na Wahindu wenye misimamo mikali na kuuvunjwa kwa kisingizio kwamba mungu wao Ram alizaliwa eneo hilo. Waislamu 2000 waliuawa katika ghasia za kuvunja msikiti huo.
Serikali ya India imetangaza kwamba ina wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kutokea ghasia na machafuko baada ya kutangazwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Allahabad. Hata hivyo matamshi yaliyotolewa na wakili wa Waislamu katika kesi hiyo Zafaryab Jilani kwamba atakata rufaa katika Mahakama Kuu ya India yanaonyesha kwamba Waislamu wataendelea kufuatilia kadhia hiyo kupitia njia za kisheria na vyombo vya mahakama. Hii ina maana kwamba Waislamu wa India hawataki kutumia ghasia na mabavu katika kadhia hiyo na kwa msingi huo wanataraji kwamba Mahakama Kuu ya India itatoa uamuzi usiopendelea upande wowote baada ya kupokea rufaa ya Waislamu wa nchi hiyo kuhusu msikiti wa Babri. Kwani kuunga mkono madai yasiyokuwa na ushahidi wowote ya Wahindu kwamba mungu wao Ram alizaliwa katika ardhi ya msikiti wa Babri na kuwanyang'anya Waislamu umiliki wa thuluthi mbili ya ardhi ya msikiti huo ni suala muhimu mno ambalo viongozi wa jamii ya Waislamu wa India wanataraji kwamba litapewa uzito linaostahili katika Mahaka Kuu ya nchi hiyo.
Vilevile Mahakama Kuu ya India inapaswa kuelewa kwamba ujenzi wa hekalu la Wahindu katika thuluthi mbili za ardhi ya msikiti wa Babri hautakomesha ghasia za Wahindu wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu waliopewa thuluthi moja tu ya ardhi ya msikiti wao uliobomolewa na suala hilo linaweza kuwa bomu la masaa linaloweza kulipuka wakati wowote.
0 comments:
Post a Comment