Mzayuni na Mmarekani kizimbani kwa kutaka kutuma silaha Somalia
Raia mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel na rubani wa zamani wa vikosi vya anga vya Marekani wamekiri kuwa walikuwa na mpango wa kusafirisha silaha kupeleka nchini Somalia . Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani imetangaza kuwa Chanoch Miller mwenye umri wa miaka 53 na Joseph O'Toole mwenye umri wa miaka 79 wamekiri mahakamani kuwa waliandaa mpango wa kuuza silaha za bunduki aina ya AK-47 pasina kuomba kibali ambao ni ukiukaji wa sheria za Marekani za udhibiti mauzo ya silaha nje ya nchi. Wawili hao walikuwa na mpango wa kutuma shehena ya bunduki 6,000 kutokea Bosnia kuelekea Somalia na shehena nyingine ya bunduki hizo aina ya AK-47 kutokea Marekani na kupitia Panama kuelekea nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Endapo watapatikana na hatia washtakiwa hao watakabiliwa na kifungo kisichozidi miaka mitano jela.
0 comments:
Post a Comment