Waandishi wa habari kutoka Somalia wameisusia redio moja iliyotekwa hivi karibuni na wapiganaji katika mji mkuu Mogadishu.
Wafanyakazi katika kituo cha redio cha GBC walikataa kupokea amri kutoka kundi la wapiganaji la Hizbul Islam, kwani ilikuwa inaingilia uhuru wa kujieleza.
Awali, Hizbul Islam iliruhusu redio binafsi kufanya shughuli zao kwenye eneo lao, ila tu walizuia kupiga muziki, ambao husema ni kinyume na Uislamu.
Mpiganaji wa Hizbul Islam
Wakati huo huo, kumekuwa na mapigano makali katika mji mkuu kabla ya kuwepo mkutano wa kujadili mgogoro wa Somalia kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa.
Katibu mkuu wa umoja huo Ban Ki-moon aliuitisha mkutano huo mjini New York kujadili mgogoro wa kisiasa na kiusalama unaoongezeka.
Mapema wiki hii, waziri mkuu alijiuzulu kutoka serikali hiyo dhaifu inayoungwa mkono na umoja wa mataifa inayoongozwa na Muislamu mwenye msimamo wa kati Rais Sheikh Sharif Ahmed.
Serikali hiyo, inayoungwa mkono na wanajeshi 6,000 wa Umoja wa Afrika, inadhibiti eneo dogo tu la mji mkuu wa nchi hiyo.
Mwandishi wa BBC Mohammed Olad Hassan mjini humo alisema watu 19 wameuawa katika mapigano yaliyoanza siku ya Alhamis asubuhi.
Takriban watu 68 wamejeruhiwa wakati majeshi ya serikali, yanayoungwa mkono na majeshi ya Umoja wa Afrika, yakipambana na wapiganaji kaskazini na kusini mwa Mogadishu.
Kumekuwa pia na urushaji wa makombora katika soko la Barkara.
Waandishi wanasema vituo vya redio vinatoa taarifa muhimu sana kwa wakazi wa Mogadishu, wanaohitaji kutwa kujua ni maeneo gani hayako salama.
Hizbul Islam na kundi la al-Shabab hudhibiti eneo kubwa la Somalia ya kati na kusini.
0 comments:
Post a Comment