David Beckham atupwa nje na Capello
Kocha wa timu ya taifa ya England, Fabio Capello, amesema hatamchagua tena David Beckham kucheza mechi za kimataifa katika mashindano mengine makubwa, na kuashiria mwisho wa kuwika kwenye mashindano kama ubingwa wa Ulaya na Kombe la Dunia kwa mchezaji huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa duniani.
Beckham amepokea habari hizo akiwa ndiyo kwanza karejea katika timu yake ya LA Galaxy ya Marekani ambako ameanza mazoezi baada ya kuwa amejeruhiwa hali iliyomkosesha kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.
Sababu kubwa aliyoitoa Capello ambaye ni raia wa Italia ni kwamba, kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, amekuwa na umri mkubwa wakati kuwa Capello anataka kuunda kikosi chenye wachezaji chipukizi.
"Endapo atakuwa fit, Natumai atacheza mechi moja au zaidi uwanja wa Wembley ili aweze kuwaaga mashabiki."
Fabio Capello
Beckham tayari ana umri wa miaka 35, na Capello amebainisha kuwa anahitaji kufanya mabadiliko makubwa ya kujenga timu ya baadaye, ingawa amemmwagia sifa Beckham kuwa ni mchezaji hodari na mfano wa kuigwa kwa vijana wanaoingia timu ya taifa ya England.
Capello alisema Beckham anaweza kucheza mechi moja au zaidi kwa England kwenye uwanja wa Wembley, ili mashabiki waweze kumuaga nahodha wao wa zamani aliyeachia ngazi hiyo baada ya mashindano ya Kombe la Dunia ya 2006.
Kelele
Hata hivyo, vyombo vya habari vya England vimemkosoa Capello kwa kutangaza kumwacha Beckham kabla ya kuzungumza naye mwenyewe kwanza.
Capello alikuwa akizungumza baada ya kikosi chake kipya chenye wachezaji wengi wachanga kilipoifunga Hungary magoli 2-1 kwenye mechi ya kirafiki iliyofanyika uwanja wa Wembley, mechi ya kwanza tangu matokeo ya kukatisha tamaa kwenye Kombe la Dunia kule Afrika Kusini.
Beckham, aliyejiunga na Los Angeles Galaxy mwaka 2007, amechezea timu ya taifa ya England mechi 115, idadi ambayo ni kubwa kuliko mchezaji mwingine yoyote wa ndani, ukitoa mlinda mlango Peter Shilton aliyepiga jumla ya mechi 125 kabla ya kutundika daluga mwaka 1990.
Inakuwa vigumu kwa mashabiki wengi kuamini, kutokana na Beckham kuwa zaidi ya mcheza soka. Kwa muda mrefu amekuwa nyota aliyetumika katika matangazo ya biashara na udhamini wa bidhaa na huduma mbali mbali za makampuni kama Pepsi, Adidas ambayo yamevuna mamilioni ya dola kwa kutumia kupendwa kwake na mashabiki.
Baadhi ya watu walitokea kumpenda Beckham ingawa hawaelewi lolote kuhusu soka kama mchezo. Kuondoka kwake ni fursa ya vijana wengi kutumia fursa hiyo kujinufaisha kisoka na kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment