Uholanzi yaingia fainali ya kombe la dunia
Wadachi wakishangilia ushindi wa timu yao dhidi ya Uruguay
Uholanzi ndiyo timu ya kwanza kufuzu
kwa fainali ya kombe la dunia mwaka 2010 kwa kuicharaza Uruguay mabao
3:2 katika mpambano uliochezwa katika uwanja wa Green Point, mjini
Capetown huko Afrika Kusini
Ingawa Uholanzi bado inahitaji kucheza vizuri zaidi kufikia kiwango
kinachostahili sifa ilizomiminiwa, imefaulu kuingia fainali ya kwanza
tangu mwaka 1978, ambapo ilishindwa na Argentina mabao 3:1 katika
kipindi cha muda wa ziada.
Uholanzi sasa inasubiri mchuano kati ya Ujerumani na Uhispania leo
jioni kujua ni timu gani itakayoumana nayo kwenye fainali hiyo,
itakayochezwa Jumapili ijayo mjini Johannesburg.
Mkwaju mkali wa nahodha wa Uholanzi, Giovanni van Bronckhorst, dakika
ya 18 ya mchezo, uliutikisa wavu wa lango la Uruguay, na mchezaji
anayechezea timu ya Bayern Munich kwenye ligi ya Ujerumani, Bundesliga,
Arjen Robben, na mchezaji bora wa mchuano wa jana, Wesley Sneider, kila
mmoja alikomelea msumari wa moto katika jeneza la Uruguay na kuyazika
katika kaburi la sahau matumaini ya Wamarekani Kusini kusonga mbele
katika fainali ya kombe la dunia.
Arjen
Robben, kushoto, akifunga bao la tatu dhidi ya Uruguay
Nahodha wa timu ya Uruguay, Diego Forlan, mara kadhaa aliwatia hofu
Wadachi na alisawazisha bao la kwanza pale mlinda lango wa Uholanzi
aliposhindwa kuuzuia mkwaju wake dakika ya 41 ya mchezo, muda mfupi
kabla kipindi cha mapumziko. Licha ya bao la pili la Uruguay
lililofungwa na Maxi Pereira katika dakika za mwisho, juhudi za
Wauruguay hazikufua dafu kuwawezesha kuwapiku Wadachi na kuingia
fainali.
"Ilikuwa mechi ngumu, lakini hayo yote tumeyasahau sasa tumeingia
fainali. La muhimu ni kushinda mechi yetu ya mwisho, Tuko karibu sana na
hakuna kitu kikubwa zaidi ya kombe la dunia," amesema Wesley Sneider,
ambaye sasa ametia wavuni mabao matano kwenye michuano ya kombe la dunia
huko Afrika Kusini.
Mchezaji wa Uholanzi, Rafael der Vaart amesema anajivunia ushindi wao
ingawa alihofu Uruguay wangeweza kusawazisha.
"Tunajivunia mno. Nadhani mchezo wao umekuwa mgumu, lakini
tumemenyana na tulikuwa na bahati kidogo. Hatimaye tumeridhika
namatokeo. Sijakumbwa na hofu kiasi hiki katika maisha yangu.
Tulikaribia kushindwa kwa sababu Wauruguay walikuwa na nafasi nyingi.
Lakini tumepambana na tumeshinda kwa haki."
Uholanzi haijapoteza mechi yoyote katika michauano hii na
haijashindwa tangu ilipotolewa nje na Urusi kwenye michauno ya kuwania
kombe la Ulaya mnamo mwaka 2008. Sasa ina nafasi ya kuwa timu ya kwanza
kushinda kila mechi kwenye michauno ya kombe la dunia, tangu Brazil
ilipofanya hivyo mnamo mwaka 1970.
Arjen
Robben, kulia, na kocha wa Uholanzi Bert van Marwijk
Kocha wa Uholanzi, Bert van Marwijk, amesema Wadachi wanaweza
kujivunia timu yao. "Inafurahisha kwamba tumeweza kufanya hivi. Ni miaka
32 tangu Uholanzi ilipocheza katika fainali. Tunaweza kujivunia nchi
ndogo kama hii," ameongeza kusema kocha huyo.
Kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez, kwa upande wake amevunjika moyo
kwamba timu yake imeshindwa kidogo tu. "Najivunia wachezaji wangu,
nakubali kushindwa na timu ambayo ilikuwa bora kuliko sisi. Tunahuzunika
kwa sababu tulikuwa karibu kuingia fainali."
Ingawa imeshindwa, Uruguay inaweza kujivunia kocha Oscar Tabarez
ambaye ameingoza timu hiyo kuingia semi fainali baada ya miaka 40. Ni
ufanisi mkubwa kwa nchi yenye wakaazi milioni 3.4, na sasa wachezaji
wanalazimika kuweka kando huzuni yao na kujiandaa kwa mtanange wa
kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu Jumamosi ijayo.
Mpinzani wa Uruguay atajulikana baada ya mechi kati ya Ujerumani na
Uhispania baadaye leo, mpambano ambao ni ni marudio ya fainali ya kombe
la Ulaya mwaka 2008, ambapo Uhispania iliichapa Ujerumani bao 1:0 bao
lililofungwa na Fernando Torres. Ujerumani inapania kulipiza kisasi.
Mwandishi:Josephat Char
0 comments:
Post a Comment