Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amewakosoa
vikali wabunge kwa kupiga kura ya kujiongezea mshahara mikubwa.
Iwapo pendekezo hilo litapitishwa, inamaanisha
kila mmoja atapata malipo ya dola za kimarekani 126,000 baada ya kukatwa
kodi, hivyo kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaolipwa kiwango kikubwa cha
fedha duniani.
Bw Odinga amesema muda mfupi baada ya kutolewa
hospitali, " Si sawa. Inatoa ishara mbaya kwa raia wa nchi hii."
Wiki iliyopita alifanyiwa upasuaji wa kuondosha
maji mazito 'ugiligili' kwenye ubongo.
Kura hiyo iliyopigwa na wabunge imeamsha hasira
kubwa miongoni mwa umma.
Licha ya watunga sheria kupitisha kuongezeka kwa
malipo hayo kwa asilimia 18 wiki iliyopita, bunge linatarajiwa
kulijadili suala hilo siku ya Jumanne.
Vyanzo vya habari vimeiambia gazeti la Kenya
Daily Nation uwezekano mkubwa ni kuwa mawaziri watalikataa pendekezo
hilo.
Bw Odinga amesema ameridhika na mshahara wake wa
sasa na kuwasihi wabunge wajadili mambo mengine.
Katika pendekezo hilo lililotolewa, mshahara wa
waziri mkuu utaongezeka kufikia dola za kimarekani 40,000 kwa mwezi,
ambayo ni theluthi zaidi ya mshahara wa waziri mkuu wa Uingereza na
asilimia 10 zaidi ya Rais wa Marekani.
Hata hivyo, utekelezaji hautoanza mpaka bunge
lijalo, ambapo hata nafasi ya uwaziri mkuu huenda ukawa umefutwa iwapo
katiba mpya itapitishwa katika kura ya maoni mwezi Agosti.
Mshahara wa wabunge hao utakuwa dola za
kimarekani 44,000 kwa mwaka. Lakini pia wana marupurupu chungu nzima,
ikiwemo dola 370 kwa siku kwa kujitokeza tu bungeni.
Mapato ya mwaka kwa wastani nchini Kenya ni
takriban dola za kimarekani 730, huku wengi nchini humo wakitumia kipato
cha chini ya dola moja kwa siku.
Bw Odinga aliondoka hospitalini siku ya Jumapili
na ameambiwa asianze kazi mpaka baada ya wiki mbili.
Alishika nyadhifa ya uwaziri mkuu miaka miwili
iliyopita alipojiunga na serikali ya kugawana madaraka iliyoundwa ili
kumaliza ghasia za kisiasa zilizoendelea kwa miezi kadhaa baada ya
wafuasi wake kusema alifanyiwa hila katika uchaguzi wa Desemba 2007.
bbc swahili.
0 comments:
Post a Comment