Aliyekuwa muasi kutoka Sierra
Leone amekana kumpa aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor "almasi
haramu zinazotumika kugharamia vita" katika kesi ya uhalifu wa kivita.
Issa Sesay, anayetumikia kifungo cha miaka 52
gerezani, amesema Bw Taylor hakuwa kiongozi wa kundi la waasi la
Revolutionary United Front (RUF) wakati wa vita.
Bw Taylor anatuhumiwa kutumia almasi kuchochea
ghasia huko Sierra leone zilizosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Amekana mashtaka 11 yanayomkabili.
Mahakama ya uhalifu wa kivita huko the Hague
inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imetumia zaidi ya miaka miwili
kusikiliza kesi hiyo, Bw Taylor mwenyewe akiwa amesimamishwa kizimbani
kwa miezi saba katika kipindi hicho.
Sesay, mwenye umri wa miaka 40, alihukumiwa
Octoba 2009 na mahakama hiyo hiyo maalum, iliyoundwa mahsusi
kuwashughulikia washukiwa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mauaji na ubakaji
Bw Taylor, mwenye umri wa miaka 62, anashukiwa
kuuza almasi na kununua silaha kwa ajili ya waasi wa RUF wa Sierra
leone, waliokuwa wakijulikana sana kwa kukata mikono na miguu ya raia
wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1991-2001.
Maelfu ya watu walifariki dunia katika mgogoro
huo baina ya nchi mbili za Sierra Leone na Liberia.
Sesay, shahidi muhimu kutoa ushahidi kwa utetezi
wa Bw Taylor, amesema hakuwahi kumpa Bw Taylor madini.
Ameiambia mahakama, " Hapana, sikumbuki kumgawia
almasi Bw Charles Taylor."
Amekana pia kupokea silaha au risasi kutoka kwa
Bw Taylor, na kwamba mara yake ya kwanza kumwona ni mwezi Mei 2000.
Sesay, amekiri kuwa baadhi ya makomando wa waasi
walihusika na mauaji na ubakaji wakati wa mgogoro huo, na ukataji wa
viungo ulitokea kweli.
Amesema, lakini haikuwa sera ya kundi hilo la
waasi kufanya hivyo.
0 comments:
Post a Comment