Kampeni za uchaguzi mkuu kuanza Rwanda
Kinyang'anyiro cha kuwania urais wa Rwanda kinaanza rasmi hii leo ambapo kampeni zinazinduliwa kote nchini humo. Wagombea wanne wanawania wadhifa huo akiwemo rais wa sasa Paul Kagame.
Hata hivyo uchaguzi huu utakaofanyika chini ya siku ishirini zijazo umekumbwa na walakin kufuatia madai kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani kuwa wanahangaishwa na serikali.
Pia baadhi ya wapinzani wakuu wanavutana na kesi mahakamani akiwemo mpinzani wa kike Victoire Ingabire anayetuhumiwa kuchochea chuki za kikabila na kupuuza kuwepo mauaji ya kimbari.
Saa kadhaa kabla ya wafuasi a rais Kagame kukusanyika kwenye uwanja wa Amahoro wafuasi wa kiongozi wa upinzani nao watakuwa wakiomboleza wakati wakimzika mwenda zake. Wiki iliyopita Andre Kagwa Rwisereka naibu kiongozi a chama cha Green Party alipatikana akiwa ameuawa katika eneo la Butare kusini mwa Rwanda.
Kando na hujuma za kisiasa kumekuwa pia na matukio ya kutia wasi wasi yakiwemo mauaji ya mwandishi habari mashuhuri na jaribio la mauaji dhidi ya Jenerali wa kijeshi aliyekimbilia uhamishoni Afrika Kusini.
Utawala wa Kigali umekanusha kuhusika na matukio hayo na kusema yametumiwa kuharibu sifa yake. Umoja wa Mataifa umetaka kuwepo na uchunguzi dhidi ya mauaji hayo ambayo makundi ya kibinadamu yamesema yamesababishwa na uhasama wa kisiasa.
Miaka saba iliyopita Paul Kagame alishinda urais kwa asilimia 97, na hata wakati huu anatarajiwa kushinda kwa urahisi. Kagame amekuwa kipenzi cha jamii ya kimataifa inayomsifia kwa kuijenga upya nchi ya Rwanda kufuatia mauaji ya Kimbari ya 1994.
Baadhi ya wafuasi wake wanamuona kama kiongozi anayefuata sera kali za kijeshi kwa minajili ya kulinda usalama wa kitaifa. Hata hivyo malalamiko ya unyanyasaji na kuzima wakosoaji yanatilia shaka majaaliwa ya udhibiti kamili wa Rwanda.
0 comments:
Post a Comment