Interpol yatoa picha za watu wanaoshukiwa kutekeleza mauaji ya Kampala
Polisi ya Kimataifa Interpol imechapisha picha mbili zinazodhaniwa ni za watu waliohusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyouwa watu 73 katika mji mkuu wa Uganda, Kampala. Interpol imetangaza kuwa imechapisha picha hizo kwa matarajio kwamba baadhi ya watu watawatambua na kutoa habari zao zaidi. Interpol imetangaza kuwa picha za washukiwa hao wawili zilichapishwa baada ya kuunganisha mabaki ya miili yao iliyopatikana mahala mashambulizi ya Jumapili ya wiki iliyopita yalipofanyika. Kundi la al Shabaab ambalo limetangaza kwamba lilihusika na mashambulizi hayo ya mabomu yaliyolenga watu waliokuwa wakitazama fainali ya soka ya Kombe la Dunia, limekanusha kwamba mashambulizi hayo yametekelezwa na watu waliojitoa mhanga. Hata hivyo Inspekta wa Polisi ya Uganda Kale Kayihura anasema kuwa mashambulizi hayo yalitekelezwa na watu waliojitoa mhanga na kwamba mmoja wa washukiwa hao alikuwa na asili ya Somalia.
0 comments:
Post a Comment