60 wauawa katika milipuko ya bomu Uganda
Milipuko imetokea Kampala, mji
mkuu wa Uganda, ikilenga mashabiki wa soka waliokuwa wakitazama mechi ya
fainali ya Kombe la Dunia katika televisheni.
Idadi kamili ya waliofariki bado haijulikani
japo awali miili 23 ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti. Duru
zinaarifu kuwa idadi hiyo inahofiwa kufikia zaidi ya watu 60.
Mkuu wa polisi nchini humo, Kale Kaihura,
amesema kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa milipuko hiyo iliyotokea
katika mikahawa ya vyakula na pombe ilinuiwa kusababisha maafa zaidi.
Shaka kuu imetiliwa kikundi cha wapiganaji wa
Al-Shabab nchini Somalia ambako Uganda imetuma majeshi yake kusaidia
katika shughuli ya amani chini ya muungano wa Afrika.
*********************
Liwalo na liwe, sitajiuzulu - Naoto Kan
Waziri mkuu wa Japan Naoto Kan
amesema kuwa hatajiuzulu licha ya kushindwa kwa serikali yake katika
uchaguzi wa bunge la uakilishi.
Matokeo ya awali yameonyesha kuwa serikali hiyo
ya mseto imepoteza viti vingi katika uchaguzi huo na hivyo kutoa
wasiwasi wa kuhujumiwa na upinzani.
Alilaumu matokeo hayo kwa pendekezo alilotoa
awali la kuongeza ushuru wa mauzo nchini humo.
Mwandishi wa BBC anasema kuwa matokeo hayo
yameonyesha changamoto kubwa kwa serikali hiyo iliyochukua madaraka
mwaka jana chini ya chama cha Democratic kwa kuahidi mabadiliko ya
utawala.
bbc swahili
0 comments:
Post a Comment