Mwendesha mashtaka mkuu wa
Mahakama ya Kimataifa anaongeza juhudi kuhusu kesi dhidi ya raia wawili
wa Sudan wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita.
Luis Moreno-Ocampo amelitaka Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa kuiamuru Khartoum kuwakabidhi wanaume hao kwa
mahakam hiyo.
Raia hao wa Sudan walishtakiwa miaka mitatu
iliyopita kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika
jimbo la Darfur, lakini baado wanaendelea kushikilia nafasi za juu
serikalini.
Watuhumiwa walishtakiwa kwa mashambulizi katika
vijiji kadhaa huko Darfur, ambayo yalisababisha mauaji ya watu wengi,
ubakaji na watu kutoroka makaazi yao.
Bw Ali Kushayb ni kiongozi wa wanamgambo
wanaolaumiwa kuhusika na uhalifu huo. Na Bw Ahmed Haroun, waziri wa
zamani wa mambo ya ndani ambaye sasa ni mkuu wa mkoa, anashtumiwa
kupanga mashambulizi hayo.
Mwezi uliopita majaji wa Mahakama ya ICC
walitangaza kuwa serikali ya mjini Khartoum haiwajibiki ipasavyo
kuwakabidhi watuhumiwa hao.
Sasa mwendesha mashtaka mkuu, Bw Ocampo
alilihimiza Baraza la Usalama kushinikiza kwa nguvu ili kuhakikisha
kukamatwa kwa watu hao.
Akijibu wito huo, Balozi wa Sudan katika Umoja
wa Mataifa, Abdalmahmoud Abdalhaleem alimshtumu Bw Ocampo kwa kuwa na
malengo yanayochochewa kisiasa, na kusema mpango huo unalenga kutatiza
juhudi za amani katika jimbo la Darfur.
Bw Ocampo alisema mashambulizi dhidi ya raia
yanaendelea kwa kiwango kikubwa Darfur, licha ya taarifa kusema kuwa
hali imeimarika.
0 comments:
Post a Comment