Katika taarifa ya pamoja vyama
vikuu vinane vya kisiasa nchini Burundi vimesema chama tawala cha
CNDD-FDD kulitumia ukosefu wa umeme uliokumba nchi hiyo mnamo Jumatatu
kujaza masanduku kutumia kura bandia.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha FNL, Agathon
Rwasa, ameaiambia BBC kwamba kulikuwa na dosari tele katika shughuli
yote ya upigaji kura ikiwa ni pamoja na hitalafu nyingi zilizotokea,
kukosekana kwa kadi za wapigaji kura na makaratasi ya wagombea.Pia amedai kuwa idadi ya waliopiga kura ni zaidi ya ile iliyoandikishwa.
Kutokana na hayo upinzani sasa unataka uchaguzi huo kufanyika sambamba na uchaguzi wa Urais hapo Juni 28.
Makundi hayo ya upinzani yanasema kuwa Tume ya Uchaugizi isipofutilia mbali matokeo hayo watachukua hatua za amani kuhakikisha kuwa uchaguzi umerudiwa.
Malalamishi haya juu ya matokeo ya uchaguzi wa Udiwani uliofanyika Jumatatu, ambayo ni awamu ya kwanza tu ya mfululizo wa mwezi mmoja wa Uchaguzi Mkuu, huenda yakazusha wasiwasi juu ya uwezekano wa kuzorota kwa amani katika Taifa hili ambalo lingali linauguza vidonda vya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka kadhaa.
Ingawa ni vyama vinane vilivyotia saini taarifa hiyo ya kulalamikia wizi wa kura ni chama cha FNL kinachoongozwa na Agathon Rwasa, kinachotajwa kuwa na ushindani mkali dhidi ya chama kinachotawala cha CNDD-FDD kinachoongozwa na Rais Pierre Nkurunzisa.
Kulingana na makisio ya matokeo yaliyotolewa jana na Tume ya Uchaguzi chama tawala cha Rais Pierre Nkurunziza kilipata asilimia 70 ya kura zote za udiwani katika maeneo 57 kati ya 70 yanayowakilishwa Bungeni.
BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment