Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa limepiga kura ya kuruhusu kuondolewa kwa kiasi cha wanajeshi
wake 2000 wanaolinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hata hivyo, baraza hilo limeahirisha uamuzi
kuhusu kuondolewa kikamilifu kwa kikosi chake chenye wanajeshi 20, 500,
hadi mwaka ujao,kama alivyoagiza Rais wa Congo, Joseph Kabila.
Wajumbe wote 15 wa baraza kwa kauli moja
walipitisha azimio la kuwaondoa wanajeshi hao "haswa katika maeneo
ambayo hali ya usalama inaruhusu".
Umoja wa Mataifa pia uliamua operesheni zake za
kawaida kuendelea nchini Congo hadi mwezi June mwaka wa 2011.
Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Congo ambacho
hujulikana kama MONUC, kuanzia mwezi July kitafahamika kama (UN
Organisation Stabilisation Mission in DR Congo) MONUSCO.
Azimio hilo linaruhusu MONUSCO kuwa na wanajeshi
19,815, waangalizi wa kijeshi wapatao 760, na polisi mchanganyiko
wapatao 1400.
Unyanyasaji wa kimapenzi
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na rekodi
yenye utata katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na madai ya
kuhusika na dhulma za kimapenzi, usafirishaji wa dhahabu kimagendo na
kuwatoroka waasi wakati wa mapigano.
Askari wa kulinda amani waliwasili katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka wa 1999, wakati huo wakianza
kushughulikia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini kote.
Tangu kumalizika kwa mapigano mwaka wa 2003,
wamekuwa wakipambana na wanamgambo wa makundi mbali mbali, ambao
wamekuwa wakiiba madini yenye thamani kubwa mashariki mwa nchi.
Wengi wa wanamgambo hao sasa aidha
wamenyanganywa silaha, au kujumuishwa katika jeshi la Congo, huku
wengine wakibakia kama majangili wenye silaha.
Rais Kabila anaamini kuwa jeshi lake la taifa
lina uwezo wa kushughulikia matatizo yaliyobaki na amesema anataka
wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wawe wameondoka nchini humo mwishoni mwa
mwaka wa 2011.
Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa
eneo hilo baado halina usalama, na halitoweza kuhimili athari za
kuondoka kwa wanajeshi hao wa kulinda amani.
Unyanyasaji wa kimapenzi ni shida ya kipekee,
ambapo zaidi ya wanawake 8,000 walibakwa wakati wa mapigano, mwaka wa
2009, kulingana na repoti ya Umoja wa Mataifa.
Hali hiyo ilisababisha kikosi cha MONUC
kuwasindikiza wanawake wanapokwenda sokoni.
Umoja wa Mataifa umeamua kuwa mustakbala wa
wanajeshi wake utaamuliwa kutokana na mafanikio yatakayopatikana
mashariki mwa nchi na uwezo wa serikali ya Congo wa kuwalinda raia wake,
pamoja kudhibiti nchi nzima.
"Hatua ya kuwalinda raia lazima ipewe umuhimu"
Umoja wa Mataifa ilisema katika azimio lake, na kuongeza kuwa
iliwaruhusu walinda amani wake kutumia "nguvu zao zote" kutekeleza
azimio hilo.
BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment