Mkuu wa Umoja wa Mataifa
amesema, mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) imefanikiwa
kulazimisha serikali kubadili mwelekeo wao tangu iundwe miaka minane
iliyopita.
Ban Ki-moon ameuambia mkutano unaofanyika Uganda
unaojadili kuhusu mahakama hiyo iliyopo Hague kwamba imepunguza
uwezekano wa watu kuepuka adhabu na kuweka misingi mipya juu ya haki za
waathiriwa.
Lakini ametoa wito wa nchi wanachama
kushirikiana.
ICC ina kesi tano zinazoendelea, zote zikiwa
kutoka barani Afrika. Mpaka sasa hakuna aliyepatikana na hatia ya madai
ya kuhusika na uhalifu wa kivita.
Bw Ban aliwaambia viongozi, " Kwa wakati ule
wachache wangeamini kwamba mahakama hii ingekuwa hapa ilipo, inafanya
kazi vizuri, inafanya utafiti na kuendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita
na uhalifu dhidi ya binadamu.
"Katika karne hii mpya ya uwajibikaji, wale
wanaofanya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu watashughulikiwa
ipasavyo."
Bw Ban amesema wakati sasa umepita wa dunia
kuchagua baina ya amani na haki- sasa mataifa yanatakiwa kukabiliana
nayo bega kwa bega.
Lakini mwandishi wa BBC Karen Allen kwenye mji
mkuu wa Uganda, Kampala, amesema hatua ya kutoa hati za kukamatwa dhidi
ya viongozi waliopo madarakani, akiwemo Rais Omar al-Bashir wa Sudan kwa
madai ya uhalifu wa kivita mjini Darfur, imezua wakosoaji wengine
kusema mashtaka kama hayo yanakatisha tamaa harakati za kuleta amani
katika eneo hilo.
Viongozi kutoka zaidi ya nchi 100 wanashiriki
mkutano huo, kujadili mafanikio ya ICC na kutoa mapendekezo ya
kuimarisha sheria zake. BBC swahili.
0 comments:
Post a Comment