Prof.Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba ametangaza nia ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia chama chake.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Profesa Lipumba kujaribu kuingia Ikulu. Kwa mara ya kwanza, aligombea kiti hicho mwaka 1995 na kushinda nafasi ya tatu nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM na Augustine Mrema, aliyegombea kupitia NCCR-Mageuzi.
Hata hivyo, alimuacha nyuma John Cheyo wa UDP. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Profesa Lipumba alipanda chati kwa kushika nafasi ya pili, akimfuatia Benjamin Mkapa wa CCM na kuwaacha nyuma Augustine Mrema wa TLP na John Cheyo wa UDP.
Profesa Lipumba alitetea nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 baada ya kuibuka mshindi wa pili nyuma ya Rais Jakaya Kikwete wa CCM na kuwaacha nyuma Freeman Mbowe (Chadema), Augustine Mrema (TLP), Dk. Sengodo Mvungi (NCCR-Mageuzi), Mchungaji Christopher Mtikila (DP), Profesa Leonard Shayo (Demokrasia Makini), Paul Kyara, (Sau), Anna Senkoro (PPT-Maendeleo) na Dk. Emmanuel Makaidi (NLD).
Lakini baada ya kuteleza mara tatu, jana wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la CUF ambalo linajadili hali ya kisiasa nchini, Prof. Lipumba alisema kuwa amefikia uamuzi wa kujitosa tena kuwania urais kutokana na kile alichokiita Taifa kulegalega.
“Napenda kulieleza Baraza, pamoja na kila mwananchama wa chama chetu kuwa nina haki ya kuchukua fomu na kugombea nafasi ya uongozi na nafasi ya urais katika kukiwakilisha chama.
“Lakini katika ombi hili la uongozi na kuongezeka kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira na sera zisizotekelezeka kwa kweli naona ninawajibu kwa Taifa langu kusema na mimi nitakuwa mmoja wa wanachama wa CUF watakaochukua fomu kuomba ridhaa ya Mkutano Mkuu wa CUF ili niwe mgombea wa urais”.
Aliongeza: “Sababu iliyonisukuma ni huu mkutano wa World Economic Forum (Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi kuhusu Afrika), badala ya sisi kuwa na mkutano wa Tanzania Economic Forum (Mkutano wa Uchumi wa Tanzania) ili tukajadili mikakati ya kuondoa umasikini, lakini tumekuwa tukikimbilia ya kimataifa,” alisema.
Kutangaza kwa Lipumba kuwania tena urais kunakamilisha ndoto ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye Machi 15 mwaka jana, akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Viwanja vya Temeke Mwisho, Dar es Salaam alimpigia debe Profesa Lipumba na kusisitiza lazima agombee urais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Jana, Profesa Lipumba alisema CUF itahakikisha inaweka bajeti na kuwekeza kwenye kilimo akisisitiza mapinduzi ya kilimo ndiyo yatakayochochea mapinduzi ya kweli na kuwa katika vipindi vijavyo watahakikisha bajeti ya kilimo inakuwa kati ya asilimia 10 hadi 15 ya bajeti yote.
Aliongeza pia kwamba, kuna haja ya kuwapo utaratibu wa kuongeza ajira kwa vijana, kufufua Reli ya Kati, kutumia bandari zilizopo na kutumia jiografia katika kutoa ajira na kukuza uchumi kwa vijana kwa kuanzisha shughuli za biashara.
“Serikali inajisifu kuwa imeongeza ajira katika sekta isiyo rasmi, lakini nadhani zilizoongezeka ni zile za wauza karanga na maji kwenye mabasi na waokota chupa za maji zilizotupwa, lakini ajira zinazomletea mwananchi uwezo wa kumudu maisha hazijaongezeka.
Katika hali hiyo, mwananchi ana kila sababu ya kuangalia chama gani kitakachoweza kuleta dira ya mabadiliko.”
Aliongeza kuwa: “ Huwezi kuwa na viwanda kama huna umeme na maji ya uhakika, kilimo kinaweza kuwa malighafi ya kiwanda kutoa ajira kwa vijana, pia kuweka bodi za kitaalamu na si zile za kisiasa na kuwapo wawekezaji wa kweli, na haya yanawezekana kama tutakuwa na uongozi bora.”
Alitumia nafasi hiyo kuzungumzia suala la maridhiano kwa upande wa Zanzibar, akisema: “Kwa upande wa Zanzibar, pamoja na kuwa na maridhiano, tunashukuru kwamba Rais Karume, amejirudi na kufikia maridhiano baada ya mazungumzo, lakini bado kuna wananchi wenye haki ya kuwepo kwenye daftari la kupiga kura hawajaandikishwa kutokana na kutopewa vitambulisho vya ukazi au sababu zingine, na hili ni lazima lishughulikiwe ili haki iweze kutendeka.”
Hakuliacha suala la mgomo wa wafanyakazi, akidai amesikitishwa na uamuzi wa Rais Kikwete wa kushindwa kusikiliza madai ya wafanyakazi yaliyopelekea kutaka kusitisha mgomo kwa kuhofia Mkutano wa Kimataifa.
“Ametoa vitisho kuwa wafanyakazi watarejea kwenye meza ya majadiliano wakiwa na plasta zilizotokana na kupigwa virungu na polisi, amefikia kutishia matumizi ya risasi za moto, badala ya kuwasikiliza wafanyakazi amesikiliza watendaji. Badala ya kuzungumza na wenye matatizo unakwenda kuzungumza na watu wasio na kazi.”
Aidha, CUF imetoa dira ya mabadiliko watakayoitumia kuingia madarakani. Dira hiyo imelenga kumpatia Mtanzania milo mitatu na kujenga Umoja wa Kitaifa.
Pia katika dira hiyo itahakikisha kila mtoto wa Tanzania anapata elimu bora na kutoa elimu kwa wasichana na wanawake kutumia soko la ajira, kufanikisha mabadiliko ya uchumi na kujenga uchumi wa kisasa.
Kwa ujumla, Profesa Lipumba ameonekana kurejea sera zile zile alizozitumia katika kujinadi kwa urais katika chaguzi tatu zilizopita
Sunday, May 9, 2010
Mambo yameiva Lipumba ajitosa tena urais 2010!!
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Sunday, May 09, 2010
Email This
BlogThis!
Share to Twitter
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment