SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, May 14, 2010

JK aagiza wanafunzi watoro wasakwe nyumba kwa nyumba

Fredy Azzah
RAIS Jakaya Kikwete, amewaagiza Wakuu wa wilaya zote nchini kuendesha msako wa nyumba kwa nyumba, kubaini watoto waliofaulu kuingia sekondari mwaka huu, lakini mpaka sasa wameshindwa kuanza masomo yao.

Amesema katika kazi hiyo, wazazi wote ambao waliwazuia watoto wao kuanza masomo ya sekondari kwa sababu yoyote ile wahojiwe kwa nia ya kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao shule mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,  maagizo hayo yalitolewa, mwanzoni mwa wiki hii mjini Masasi baada ya kupatiwa maelezo ya Maendeleo ya Mkoa wa Mtwara.

“Alitoa maagizo hayo baada ya kuambiwa kuwa asilimia 35.6 ya watoto wote 12,843 walioshinda mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kuingia sekondari katika Mkoa wa Mtwara, hawajaripoti shuleni mpaka sasa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,  Kikwete aliambiwa kuwa ni asilimia 64 tu, yaani watoto 8,278 walioripoti na kuanza masomo ya sekondari wakati watoto 4,565 hawajaripoti shuleni na hawajulikani waliko.

Ilisema katika idadi hiyo, Wilaya ya Mtwara ndiyo inayoongoza kwa asilimia 54, ikifuatiwa na Nanyumbu asilimia 48, Masasi asilimia 35, Tandahimba asilimia 32, Mikindani asilimia 22 na Newala asilimia 21.

“Rais Kikwete aliambiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Anatoli Tarimo kuwa baadhi ya sababu zilizowazuia watoto hao kuendelea na  shule ni pamoja na baadhi yao kupata mimba, kuozwa ama kuzuiwa na wazazi wao kwenda shule,” Ilifafanua sehemu nyingine ya taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa Mara baada ya kupewa takwimu hizo, Rais Kikwete alisema “Hizi takwimu ni za juu sana.  Haiwezekani tukaendelea kuwadhulumu watoto wetu maisha bora kwa kuwazuia wasiende shule wakati shule zipo, nafasi zipo na kila kitu kipo.”:

 “Tafuteni majina ya watoto hawa wote, wazazi wao waitwe, wajieleze na kama hawana majibu wawajibishwe. Afuatwe mtoto mmoja baada ya mwingine bila kumwacha yoyote. Na njia rahisi ufanywe msako wa nyumba kwa nyumba, kama ilivyokuwa zamani wakati wa kukusanya kodi,”.

Taarifa hiyo ilisema Rais  alifafanua kuwa Wazazi wa watoto hao wahojiwe siyo kwa nia ya kutaka kujua sababu gani zinazuia wasiwapeleke watoto shule, bali kwa nia ya kuhakikisha kuwa watoto wanapelekwa shuleni mara moja.

“Kazi hii ifanyike katika kila wilaya nchini na isimamiwe na mkuu wa wilaya katika kila wilaya ambako yapo matatizo ya namna hii.” Ilisema sehemu nyingine

Rais Kikwete alipewa ripoti hiyo ya maendeleo ya Mkoa wa Mtwara, ikiwa sehemu ya shughuli zake wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo.

0 comments:

Post a Comment