SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, May 13, 2010

Mwanafunzi wa SUA mbaroni kwa tuhuma za mauaji

Imeandikwa na Na Eline Shaidi, Morogoro
POLISI inamshikilia mwanafunzi mmoja kati ya sita wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mlinzi Jafari Thabiti (38) yaliyotokea Mei 11, mwaka huu.
Mauaji hayo yalifanyika katika kampasi ya chuo hicho ya Solomon Mahlangu iliyopo Mazimbu katika Manispaa ya Morogoro.
Mwanafunzi anayeshikiliwa na polisi ametajwa kuwa ni Yona Mahona maarufu ‘Ngosha’ (29) ambaye anasoma shahada ya ufugaji wa samaki mwaka wa pili katika chuo hicho, ambaye alidaiwa kumpiga marehemu na kiti cha mbao sehemu ya kichwani na kumsababishia maumivu makali ambayo yalipelekea kifo chake.
Akithibitisha kukamatwa kwa mwanafunzi huyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye alisema mwanafunzi huyo alikamatwa juzi, majira ya mchana baada ya polisi kufika katika kampasi hiyo na kufanya upelelezi juu ya tukio hilo.
Alisema katika upelelezi uliofanywa na polisi ulibaini kuwa mwanafunzi huyo akiwa na wenzake ndio waliomshambulia mlinzi huyo kwa kumpiga huku wakimtuhumu kuiba simu ya mkononi iliyokuwepo kwenye bweni la wanafunzi wa kike, katika kampasi hiyo.
“Tumefanya upelelezi wa kina na tumefanikiwa kumkamata mwanafunzi mmoja ambapo kutokana na maelezo yaliyotolewa yeye alishiriki kumpiga mlinzi huyo kwa kiti cha mbao, kwa hiyo tumemkamata mwanafunzi huyu na bado tunaendelea na upelelezi zaidi juu ya tukio hilo,” alisema Andengenye.
Katika tukio lingine mtu mmoja ambaye ni Mkazi wa Kihonda katika Manispaa ya Morogoro, anayedaiwa kuwa ni mwizi Ally Ngavuma (20) amenusurika kuchomwa moto na wananchi wenye hasira baada ya kukutwa akiiba mahindi mabichi kwenye shamba lililopo eneo la Kihonda Mbuyuni katika Manispaa ya Morogoro.
Mtu huyo ambaye aliokolewa na polisi waliofika katika eneo hilo mara baada ya kukamatwa kwa mwizi huyo, walimkuta akiwa amepigwa sana na wananchi wa kata hiyo, huku akiwa amelala chini na kufungwa na kamba tayari kwa ajili ya kumchoma moto.

0 comments:

Post a Comment