Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano inapenda kutaarifu Umma kuwa Daraja la kigamboni litaanza
kutumika siku ya Jumamosi tarehe 16, Aprili, 2016 kuanzia saa 12:00
asubuhi.
Katika siku za mwanzo, magari
yatapita bila kulipia tozo hadi Serikali itakapokamilisha taratibu na
kutangaza utaratibu wa kulipia. Aidha, watembea kwa miguu na waendesha
baiskeli watavuka bure katika Daraja la Kigamboni. Hata hivyo maguta na
mikokoteni haitaruhusiwa kutumia daraja hilo kutokana na sababu za
kiusalama.
Magari yatakayoruhusiwa kupita
katika Daraja la Kigamboni katika siku hizo za mwanzo ni yale yenye
uzito usiozidi tani 10, hatua ambayo itasaidia kufuatilia mwenendo wa
upitaji wa magari katika daraja, barabara za juu (Interchange) katika
eneo la Kurasini, pamoja na kuhakikisha kwamba magari yanayotoka au
kuingia katika daraja hayasababishi msongamano wa magari katika Barabara
ya Nelson Mandela, Barabara ya Kilwa na maeneo mengine ya jiji. Baada
ya utaratibu kukamilika magari ya aina zote yenye uzito unaoruhusiwa
kisheria yataruhusiwa kupita katika daraja.
Mambo muhimu ambayo madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatakiwa kuzingatia ni:-
- Kuzingatia sheria ya Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kufuata mwendo kasi unaotakiwa ili kuepuka ajali na kuepuka uharibifu miundombinu ya daraja
- Kufuata alama za barabarani zilizowekwa katika ‘Interchange’ ya Kurasini ili kwenda kwenye uelekeo sahihi.
- Kuzingatia alama zilizowekwa kwenye milango (Toll Gates) ya Kituo cha kulipia tozo (Toll Plaza) ili kuepuka uharibifu wa miundombinu ya kituo hicho.
- Madereva na watumiaji wa barabara wengine watakaosababisha uharibifu wa aina yeyote wa miundombinu ya daraja watatozwa faini au kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
- Kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa takataka katika eneo la daraja.
Aidha, Wizaraya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano inawataka madereva wa magari ya mizigo wanaoegesha katika
barabara ya Nelson Mandela wakisubiri kuingia bandarini watafute eneo
stahiki la maegesho na kuyaondoa magari hayo kwani hatua za kisheria
zitachukuliwa kwa wale watakaoenda kinyume na agizo hili.
Msongamano wa magari hayo husababisha uharibifu wa barabara na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara katika eneo hilo.
Imetolewa na;
Eng. Joseph M. Nyamhanga
Katibu Mkuu (Ujenzi)
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
14 Aprili, 2016
0 comments:
Post a Comment