MUENDELEZO wa Jeshi la Polisi nchini kuwanyanyasa, kuwatisha
waandishi wa habari na kuwafanya wasitekeleze wajibu wao ipasavyo,
ilijidhihirisha wazi jana makao makuu ya jeshi hilo, baada ya waandishi
kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue taarifa za kuhojiwa kwa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe.
Tukio la kupigwa na kudhalilishwa kwa waandishi wa habari lilitokea
jana, limetokea ikiwa ni siku moja baada ya Makamu wa Rais, Dk. Mohamed
Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kushirikiana
na waandishi wa habari katika kufanya kazi kwa ajili ya kulinda amani ya
nchi.
Waandishi waliyopigwa na Polisi hiyo jana ni Josephat Isango
anayeandikia gazeti hili, huku Yusuph Badi ambaye ni mpiga picha wa
magazeti ya serikali, akipigwa na ‘kusakiziwa’ mbwa ili wamuume.
Dalili za waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi yao, zilianza
kujionesha mapema jana wakati Mbowe alipowasili katika makao makuu ya
Jeshi la Polisi, ambako waandishi walizuiwa wasiingie katika eneo hilo
kwa ajili ya kuchukua picha na maelezo ya kiongozi huyo.
Akiwa anawaongoza askari wake katika amri ya kushambuliwa kwa
waandishi wa habari hiyo jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul
Chagonja, alisikika mara kwa mara akiwaagiza vijana wake wawaondoe
waandishi na hata kuwasakizia mbwa.
Chagonja, alisikika mara kadhaa akitoa amri kwa askari kuwa
wawafungulie mbwa ili waweze kujeruhi angalau mtu mmoja kutoa funzo ili
wafuasi wa CHADEMA waliokuwa kwenye lango kumsubiri Mbowe waondoke.
“Waondoeni wote msiwaruhusu hata hao waandishi kuingia humu, ninyi
askari wa mbwa mnafanya nini hapo wakati watu wamejazana mlangoni
wapelekeeni hao,” alisikika akisema Kamishna Chagonja.
Mara baada ya maelekezo hayo ya Kamishna Chagonja, askari waliokuwa
na mbwa walianza kuwakimbiza wafuasi wa CHADEMA na waandishi wa habari.
Katika hali ya kustaajabisha, askari watatu kwa pamoja walimfuata
Josephat Isango, aliyekuwa akitoka katika lango kuu na kuanza
kumshambulia kwa rungu na mateke hali iliyowafanya waandishi wa habari
kuingilia kati kwa ajili ya kumnusuru.
Baada ya waandishi kumnusuru Isango, kipigo kiligeukia kwa Mwandishi
Yusuph Badi, ambaye wakati akishambuliwa alianguka chini huku askari
wenye mbwa wakiwaachia kwa ajili ya kumshambulia.
Kilichomnusuru Badi asiumwe na mbwa hao ni kamera aliyoishika mkononi
na kujikinga ili asidhurike, kitendo hicho cha kujikinga kilisababisha
kuharibika kwa kifaa hicho.
Wakizungumza baada ya hali kutulia, Badi na Isango, walieleza kuwa
kilichofanywa na jeshi la Polisi ni kuminya uhuru wa utendaji kazi wa
waandishi katika kuuhabarisha umma wa watanzania juu ya mambo yaliyokuwa
yakitokea.
“Ni jana tu wameambiwa namna ya kutoa ushirikiano na vyombo vya
habari, lakini leo wanatupiga na kutusakizia mbwa hii si haki na
viongozi wetu wanapaswa waangalie mara mbili mbili namna ya kushirikiana
na jeshi hili,” alisema Badi.
Jeshi la Polisi limekuwa na kawaida ya kuwanyanyasa, kuwapiga na hata
kuwaua waandishi wa habari pale wanapotekeleza wajibu wao wa kukusanya
habari.
Tukio linalokumbukwa zaidi la ukatili wa askari wa jeshi hilo kwa
waandishi wa habari ni mauaji ya Mwandishi wa kituo cha Televisheni ya
Chanel ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, mauaji yaliyotokea Septemba 2
mwaka juzi katika Kijiji cha Nyololo Mufindi mkoani Iringa wakati
mwandishi huyo akiwajibika kukusanya habari.
CGHANZO: BOFYA HAPA
0 comments:
Post a Comment